Vyama vya upinzani ni vichanga? -3

Katika sehemu ya pili ya makala haya wiki iliyopita, nilizungumza kuanzishwa vyama vingi vya siasa na malengo yao. Pia niligusia kauli iliyotolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa Uchaguzi Mkuu 1995 kuhusu uwezo wa vyama vya upinzani kushinda katika chaguzi kuu za mwaka 1995 hadi 2010. Leo tunaendelea…

Mwaka 2000 katika Uchaguzi Mkuu wa pili wa vyama vingi, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Kapteni Ukiwaona Ditopile Mzuzuri (marehemu), katika kampeni za kukinadi Chama chake Cha Mapinduzi (CCM), na kuwapigia debe wagombea urais, ubunge na udiwani, katika Mkoa wa Lindi, alivielezea vyama vya upinzani kuwa ni vichanga na kuvifananisha na watoto wadogo, ambao hawawezi, wala hawajui kitu.

 

Mara kadhaa katika mikutano ya hadhara ya CCM vijijini na mijini Kapteni Ditopile alisema kuwa vyama vya upinzani vina umri wa miaka minane (8) na CCM ina miaka 23. Aliwauliza wananchi, msichana au mvulana wa miaka 8 anaweza kupewa mume au mke? Wananchi walijibu hapana.

 

Aliwauliza tena, kijana wa kike au wa kiume wa umri wa miaka 23 unaweza kumpa mume au mke? Walijibu ndiyo. Basi, aliwataka wananchi kuipa kura CCM kwa vile kina umri wa miaka 23 na kuvinyima kura vyama vya upinzani vyenye umri wa miaka 8, ni watoto bado. Wanachoweza ni kucheza ‘madanga na matipwi’. Lugha hizo ziliwafurahisha sana wana-CCM na kuwakera mno wapinzani. Watanzania tumeendelea kuona vyama vya upinzani vikikosa nafasi za kushika dola katika chaguzi zilizopita. Je, sababu bado ni vichanga au watoto?

 

Mwaka 2005 vyama vya upinzani vilikuwa na umri wa miaka 13. Mwaka 2010 vilikuwa na umri wa miaka 18 ni vijana, wameweza kupiga kura, lakini hawakupata nafasi ya kushika dola. Mwaka 2015 vitakuwa na umri wa miaka 23, wanaweza kupewa mume au mke? Na CCM itakuwa na miaka 38. Kama hivyo ndivyo hali itakuwaje?

 

Nimetoa kauli mbili za viongozi — Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kapteni Ditopile — kutaka kuonesha falsafa na mantiki za kauli hizo na hali halisi ya mwenendo wa vyama vya siasa hapa nchini. Mwalimu Nyerere alikuwa na maana gani aliposema chama cha upinzani hakiwezi kushinda na kushika dola, ‘labda labda mwaka 2015?’ Ditopile alikuwa na maana gani aliposema vyama vya siasa bado ni watoto?

 

Leo tuna vyama vya siasa zaidi ya 20 lakini vinavyosikika na kukitikisa Chama Cha Mapinduzi ni vile vilivyopo bungeni. TLP, UDP, NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema. Malumbano hasa ya kisiasa yako  kati ya CCM kwa upande mmoja, CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi kwa upande wa pili.

 

Malumbano haya nilitazamia yangekuwa ya kisiasa zaidi kuhusu itikadi na sera ili kutoa changamoto kwetu na wananchi wakati wa uchaguzi kura zetu tuzipeleke kwa nani. Je, hali itakuwaje 2015?

 

Mwalimu Nyerere alisema kuwa vyama vya upinzani visingeweza kushinda chaguzi kuu za kuanzia 1995 hadi 2010. Labda, labda 2015 kwa sababu ni vichanga na havina weledi wala tajiriba katika medani za siasa.

 

Kapteni Ditopile alisema kuwa vyama hivyo bado ni watoto, visingestahili kupewa madaraka kwa sababu havijui na haviwezi kitu. Alivifananisha na msichana au mvulana mdogo kupewa mke au mume ambaye asingeweza kumtunza.

 

Viongozi hao walikuwa sahihi na wa kweli katika kauli zao walizozitoa 1995, na 2000 katika vipindi vya uchaguzi. Vyama vya upinzani vilikuwa vichanga havikuwa na viongozi wazoefu katika medani za siasa na havikuaminika.

 

Wapiga kura wengi walikuwa wale waliotaka chama kimoja cha siasa — Chama Cha Mapinduzi. Sababu hiyo na nyinginezo ziliwakosesha kupata ridhaa ya kushika Serikali.Mwaka 2010 vyama vya upinzani vilifikisha miaka 18. Ni vijana. Ujana wao haukuweza kufanya muamala kwa Watanzania, zaidi ya kufanya mambo kwa sifa, pupa, mbwembwe na vurumai kwa wapiga kura.

 

Watanzania tulishuhudia mikasa, viroja na vituko kadha wa kadha, hata baadhi ya wapinzani wenyewe na wananchi walipatwa na madhara mbalimbali ya kupigwa, kujeruhiwa na kutiwa mahabusu.

 

Leo baadhi ya vyama vinatweta na vingine vinapumua. Pamoja na kasoro zote hizo, viko ngangari kupambana na CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015. Lengo lao ni kutaka kuiondoa CCM madarakani na wao kushika dola, hata kama CCM kuna weledi, na uzoefu na sifa ya kutawala