Vijana, kujiajiri ni kujitegemea

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amewataka vijana wamalizapo masomo yao shuleni au vyuoni wajiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa na Serikali au asasi mbalimbali nchini.

Wito huo hauna budi kuungwa mkono na viongozi wote wa Serikali, vyama vya siasa, dini na wanaharakati wa haki za binadamu kwa sababu wito huo unakusudia kuwatoa vijana wetu kutoka kwenye unyonge na ulofa na kuwapeleka kwenye furaha na kujikimu. Wito huo umenipa dalili kuwa Serikali inakusudia kurudisha uhai wa vijana na heshima ya nchi katika kujenga na kuendeleza maendeleo ya wananchi na ya Taifa kwa njia ya kujitegemea.

 

Kujitegemea ni njia safi na bora ya kuleta maendeleo ya vijana, hata watu wazima na wazee ambao bado wana nguvu za kufanya kazi na kupata riziki endelevu katika maisha yao, badala ya ombaomba kutoka kwa ndugu, majirani au jamii nyingine. Nimesema wito wa Rais Kikwete unanipa dalili ya kurudisha uhai wa vijana na Taifa letu katika kujitegemea kwa sababu katika koo, kabila au jamii ya Taifa lolote hutegemea sana nguvu, uwezo, fikra na mawazo pevu ya vijana katika shughuli za maendeleo.

Kwa mfano, wakati wa harakati za kupinga kutawaliwa na wakoloni, vijana walifanya mapambano hayo chini ya busara za wazee. Utawala ule wa kikoloni na huu wa wananchi huru uliendeshwa na vijana. Vijana ndiyo alfa na omega wa Taifa lolote katika kujenga na kudumisha maendeleo ya nchi.

Kabla na  baada ya nchi yetu kupata Uhuru wa bendera, vijana wa kiume na wa kike ndiyo waliokuwa watendaji wakuu wa shughuli za kilimo, ulinzi na usalama, uchungaji mifugo, ujenzi wa majengo, ufundi wa aina mbalimbali, upishi na uchotaji maji kutoka mtoni, ziwani na kisimani.

Katika kipindi chote cha 1960 hadi  1990, kauli za viongozi wa siasa, Serikali na wengine ziliwafanya vijana wajitambue na kujikita katika kuweka fikra zao kwenye kujiajiri katika kazi za kilimo, useremala, uashi, ushonaji, utengenezaji nguo (za batiki), ufugaji, uchungaji mifugo na kadhalika, kazi ambazo ziliwaingizia kipato kikubwa hata kumudu kuendesha maisha yao.

Sera ya elimu ya kujitegemea, siasa ni kilimo, viwanda vidogo vidogo, Jeshi la Kujenga Taifa na Azimio la Arusha ziliwahamasisha na kutoa misukumo kwa vijana kujenga tabia ya kujiajiri. Ama hakika maendeleo ya vijana na Taifa yalipatikana. Vijana walijiona huru katika nchi yao, na baada ya kazi zao walijishughulisha katika michezo na matamasha mbalimbali na kuweza kulipatia sifa Taifa letu katika mashindano ya michezo ya mpira wa miguu, riadha na ngoma kitaifa na kimataifa.

Baada ya mwaka 1990, baadhi ya kauli za viongozi wa Serikali, siasa na wasomi wa taaluma mbalimbali zilipuuza sera ya siasa ya kujitegemea kwa mtazamo kuwa ni mambo ya Siasa ya Ujamaa, jambo ambalo si sahihi. Siasa ya Ujamaa na Siasa ya Kujitegemea ni dhana mbili tofauti.

Kujitegemea ni kuleta maendeleo ya watu kwa kutumia rasilimali ya nchi, juhudi na uwezo wa wananchi wenyewe. Msingi wake ni wananchi kujiamini kwamba wana uwezo wa kujiendeleza bila ya kuombaomba misaada mingi nchi za nje. Jambo la msingi katika nguvu za uzalishaji ni watu wenye uwezo wa kufanya kazi na wanaotumia uwezo huo kufanya kazi.

Lakini, upo uhusiano kati ya ujamaa na kujitegemea kwamba ujamaa lazima uambatane na  kujitegemea kwa sababu kujitegemea kuna kanuni ya kuendeleza nguvu za uzalishaji. Lengo la ujamaa ni kujenga uchumi wa kitaifa unaotosheleza mahitaji ya jamii. Lengo hilo linaweza kufikiwa tu kama kuna mapinduzi ya kudumu ya nguvu za uzalishaji.

 

Watanzania tunaweza kujenga Tanzania yetu inayoongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na utawala wa sheria, kujitegemea na isiyokuwa na dini (Rasimu ya Katiba 2013 – utangulizi). Ni vizuri, Watanzania tukashirikiana katika kuwahamasisha vijana wetu kujenga tabia ya kujiajiri katika nyanja za ufundi, biashara, michezo, utawala na kadhalika.

Wito wa Rais Kikwete wa kuwataka vijana wajiajiri, upigiwe chapuo, lele na nderemo kuanzia serikalini, vyama vya siasa, shuleni, vyuoni na kwenye kambi za mafunzo ya vijana kwa kaulimbiu ya “KUJIAJIRI NI KUJITEGEMEA”. Ndiyo njia pekee ya kurudisha utu, heshima na hadhi ya Mtanzania.

Vijana wetu wengi nchini  wana elimu ya juu ya fani mbalimbali, vipaji na uwezo wa kufanya kazi, lakini hawana kazi. Wanasubiri kuajiriwa na  Serikali wakati haina uwezo wala nafasi ya kuwasitiri vijana  wake wote.

Nakamilisha mada yangu na kuhoji, ikiwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanaweza kuhamasisha vijana kuunda vikosi vya kijeshi, kufanya maandamano hasi, kutaka kuzunguka nchi nzima kuhamasisha wananchi mgomo (Civil Disobedience) dhidi ya utaratibu wa taasisi ya Bunge na Rais, inakuwaje washindwe kuhamasisha vijana kwamba kujiajiri ni kujitegemea?