Miaka 50 hakuna maendeleo! -3
Katika makala mbili zilizotangulia nimeandika kuhusu kichwa cha habari hapo juu. Kwa maana kuwa baadhi ya viongozi na wananchi wa kawaida wanathubutu, tena bila haya, kupiga la mgambo kuwa eti miaka 50 hakuna maendeleo huku wanaendelea kuhamisha na kuiba mali na rasilimali za nchi kama kuwa ni haki yao na kupeleka nchi za nje.
Wenzetu hao ni wale tuliowaamini na kuwapa madaraka au kutuongoza kuelekea kwenye maendeleo ya kweli, na kufuata masharti ya maendeleo ya juhudi a maarifa.
Ili sote tufike kwenye kilele cha maisha bora; kwa kutunga kaulimbiu ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania inawezekana”, inawezekana kwa sababu mali, rasilimali, ardhi, watu na msingi wa kutufikisha huko tunayo, lakini tunakwama kwa sababu ya choyo, inda, tadi na ubinafsi, wa watu tuliowaamini na sisi wengine kujaa woga.
Moja ya falsafa ya Mwalimu Julius Nyerere inasema woga ni adui wa maendeleo. Kwenye jambo lolote la maendeleo kunahitaji kutumia juhudi na maarifa zikisukumwa na ujasiri. Ujasiri, nguvu na msimamo ni misingi ya maendeleo . Hata Azimio la Arusha ambapo sasa halipo, linaweza kuwa maendeleo ya nchi huletwa na watu.
Wenzetu kwa kutambua kuwa maendeleo ya nchi huletwa na watu na si ya vitu, waliamua kwa makusudi kufanya yafuatayo: kwanza kutupilia mbali siasa safi na uongozi bora ili wananchi wasishiriki katika kufikiria kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.
Pili, wameua Siasa ya Ujamaa ambayo ni imani na demokrasia, ambayo ni imani na demokrasia ya kweli ya kuwapeleka wananchi katika maisha ya huru na haki, na kuwaongoza katika shughuli zote za umma kwa maana ya kujikomboa kiuchumi, kuanzia vijijini hadi mijini kwa kufuata miongozo ya Ujamaa na Kujitegemea.
Tatu, wamejitahidi kuwaaminisha wananchi katika mambo ya:
- Kuwapa wananchi fedha kama zawadi kuendesha mipango yao ya maendeleo,
- Kuwapa wananchi fedha kama mkopo kwa ajili ya kazi zao za maendeleo zikiwa na masharti yake ya kulipia katika muda wa kulipa na kima cha faida,
- Kuwaaminisha katika rasilimali ya kibiashara ambayo fedha ya watu au kampuni zinazotaka kuja katika nchi yetu kuanzisha shughuli mbalimbali za uchumi kwa manufaa yao wenyewe.
Misimamo hiyo iliua kabisa maendeleo yaliyopatikana kiuchumi katika kuendeleza shughuli za mazao ya kibiashara kama vile pamba, tumbaku, mkonge, chai na korosho. Kwa upande wa viwanda kama Mwatex, Mutex, Tanelec, Ufi, Mgololo na Baiskeli vilikufa kifo cha mende na kuwapa wageni mali za nchi.
Kilimo cha mazao ya chakula, mahindi, mpunga, ngano, maharage na karanga kilianza kupungua na mkazo ukawekwa katika kuomba ngano na mahindi kutoka Marekani, mchele kitumbo kutoka Japan na nchi za Kiarabu, na India kutuuzia mafuta ya kula badala ya sisi eti kushindwa kuzalisha kwa wingi mafuta ya karanga, mawese, nazi na alizeti.
Wamefuta na kupoteza historia ya nchi kwa kutunga na kuandika vitabu vya Ali Nacha badala ya vitabu vya elimu na maarifa. Wanaendelea hadi leo kutia mkazo katika kupata kwanza fedha badala ya juhudi na maarifa ambayo ni masharti ya maendeleo.
Wanauza elimu ya tiba kwa bei ghali ili kutupumbaza akili zetu na kudhoofisha afya ya mtoto wa mkulima na mfanyakazi, asiwe na uwezo wa kufuta ujinga na kutokomeza misaada na kukopa fedha, ndiyo njia hasa ya kuleta maendeleo ya nchini na watu baada ya kuwaelimisha juu ya kilimo cha mazao tunachohitaji kwa chakula na fedha.
Wanawatelekeza na kuwaaminisha vijana kuwa utunzi wa nyimbo na (filamu hasa za mapenzi), ubebaji na upelekaji wa dawa za kulevya ndani na nje ya nchi pamoja na mashindano ya ulimbwende, ni kashata zitakazowapa nguvu na afya nzuri katika kupambana na vikwazo vya maisha badala ya kuwapa maarifa ya kilimo, ufundi na ajira ya uhakika na ya kudumu katika fani.
Sisemi hata chembe napinga vipaji na mageuzi wala fasihi za vijana kutambuliwa, la hasha, la hasha mara elfu. Ninachosema kwanza vijana wapewe elimu na maarifa ya kutosha katika kazi na fani mbalimbali na hivyo vipaji viendelezwe sanjari kama upendeleo (hobby).
Leo tunasikia na kuona wala si siri wananchi huko vijijini wananyang’anywa maeneo yao ya ardhi na kupewa wageni. Tunashuhudia vijana wetu hawapati elimu stahiki tangu shule za msingi hadi vyuo vikuu. Magereza yamejaa vijana wanotuhumiwa ni vibaka, wezi na wahalifu wa mambo mbalimbali.
Ni juzi tu tumeambiwa vijana wetu wapatao 500 wapo magerezani nchini China, Hong Kong na Thailand kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya. Wahusika na biashara hiyo haramu wanatanua nchini na duniani.
Narudia kusema maendeleo yamepatikana na yapo – yawe ya kwenda mbele na kurudi nyuma – yote ni maendeleo na hasa ya kwenda mbele. Yapo maendeleo ya watu ya kustaarabika katika malazi, chakula na mavazi. Yapo maendeleo ya vitu ya majengo, barabara, tiba, lugha, mawasiliano na kadha wa kadha. Kumbuka yote ni maendeleo. Jadili.