Miaka 50 hakuna maendeleo! (1)
Mengi yanasemwa, yanaimbwa na hata kubezwa eti hakuna maendeleo tangu nchi yetu ipate Uhuru wa bendera. Hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana kuinua maisha na mazingira bora ya mwananchi. Mtazamo huo una sura mbili kutokana na asili ya mazungumzo ya watu wanaosema, wanaoimba na wanaobeza. Sura ya maendeleo ya kwenda mbele na sura ya maendeleo ya kurudi nyuma. La msingi nani anazungumza na sababu gani ya kuzungumza.
Sitanii hata chembe, kusema kweli wanaosema, wanaoimba na wanaobeza ni baadhi ya wanasiasa na wasomi uchwara; na wananchi wenye hulka ya kupinga jambo lolote la faida au hasara. Ni maumbile yao. Makundi hayo mawili usiku na mchana ndiyo yanayosema hakuna maendeleo.
Neno maendeleo kwao ni kufaidika wao. Kinyume cha mafanikio yao si maendeleo. Maendeleo kwa maana ya mafanikio ya kijamii, kiuchumi, kielimu na kisiasa kwao si maendeleo. Ndiyo maana leo tunapata tabu kupambana na mafisadi, majangili, matapeli na majahili ndani ya vyama vya siasa, Serikali na vyombo vyake, na sekta mbalimbali za umma na watu binafsi.
Baada ya Tanganyika kupata Uhuru Desemba 9, 1961, viongozi wa TANU na wa Serikali wakati huo chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, waliapa kwa Mungu kuleta maendeleo ya Watanganyika katika ustawi wa jamii, uchumi, elimu afya na utamaduni. Waliahidi baada ya miaka 10 ya Uhuru wangemwita Mwingereza kuja kuona maendeleo, kweli walimwita na aliona.
Serikali ya Tanganyika huru ilidumu muda mfupi tu kati ya Desemba 9, 1961 hadi April 26, 1964, ilipotiwa kwapani ndani ya muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar kupata Tanzania. Leo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ndiyo inayoonekana.
Lakini viongozi wale wale wa Tanganyika na dira yao ya maendeleo ya nchi bado waliendelea nayo katika Serikali ya Muungano, walifanya mengi kumnyanyua mwananchi kiuchumi.
Kwa kufuata Azimio la Arusha lililotangazwa Februari 5, 1967 mjini Arusha, kati ya mambo yake ya maendeleo ya wananchi iliangazia vitu vinne vya kuleta maendeleo.
Limesema, “Msingi wa maendeleo yote ya Watanzania ni Watanzania wenyewe; kila Mtanzania; na hasa kila mzalendo na kila mjamaa… Ili tuendelee tunahitaji vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.”
Awali, ilikubalika bila mashaka kuwa watu, ardhi na siasa safi havina mjadala. Uongozi bora ndiyo mushkeli. Kadiri mambo yalivyokwenda ikabainika hata siasa safi nayo ni tatizo. Siasa ya Ujamaa ikapata misukosuko na kufa kiainaaina.
Kuyumbayumba kwa siasa safi na uongozi bora bado wananchi walipata maendeleo katika elimu, afya, kilimo na uchumi. Shule na zahanati nyingi zilijengwa. Watoto na watu wazima walielimika na kupata matibabu bila shida. Kilimo kilishamiri na chakula bora kilitokomeza njaa na utapiamlo.
Viwanda, majengo bora ya kisasa na barabara nzuri vimejengwa kuinua uchumi, kupanua ajira na kurahisisha usafiri na usafirishaji. Mashirika ya reli, ndege, uchukuzi na mawasiliano yaliboreshwa na kuendelezwa. Mapato ya wananchi hayakupitana sana. Hakika maendeleo yalipatikana na wananchi walifurahi.
Nasikitika leo sitakwenda ndani sana kutoa takwimu mbalimbali za maendeleo kutokana na muda nilionao. Inshallah penye majaaliwa nitazitoa siku zijazo. Lakini kwa mtazamo wa nje, nina hakika wananchi wengi wanakubali maendeleo yamepatikana na yanaonekana.
Cha ajabu, baadhi ya viongozi na wasomi waliozaliwa, kulelewa na kusomeshwa ndani ya maendeleo ya Azimio la Arusha ndiyo walio mstari wa mbele kwa makusudi kuteteresha, kuvunja na kutupilia mbali dhana na nadharia ya siasa safi na uongozi bora, na kusababisha maendeleo yaliyopatikana kufifia na Ujamaa kufa.
Ardhi na watu ndiyo vitu vilivyosalia na ndivyo vinavyoshamiri na kuzua majanga tele. Wizi, utapeli, ujambazi, ujangili, ujahili na ufisadi. Dhuluma inatawala na kuzima haki kutendeka. Siasa safi na uongozi bora ambavyo ni dira na mwongozo havipo. Huu ni msiba mkubwa!
Viongozi, wasomi na wananchi walioua Azimio la Arusha ndiyo walio mstari wa mbele kuhamasisha baadhi ya wananchi na vijana kukariri na kuimba wimbo ‘hakuna maendeleo’, maskini vijana, hawatii tafakuri juu ya wimbo huo zaidi ya kuimba. Wanatumiwa kama vyombo vya kufanya vurugu, maasi, ulinzi na vyombo vya uchumi na burudani.
Itaendelea