Ombaomba ni unyonge wa Mwafrika

“Unyonge wetu ni wa aina mbili, unyonge wa kwanza ulio mkubwa zaidi ni unyonge wa moyo; unyonge wa roho. Unyonge wa pili ndiyo huu wa umaskini wa kukosa chochote. Ni kweli hatuna chochote, hatuna nguvu.” Haya ni maneno ya Mwalimu Nyerere alipowahutubia walimu katika Sherehe za Vijana kwenye  Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Mei 30, 1969.

Nimenukuu maneno haya  kutaka kukumbusha unyonge wa Mwafrika. Unyonge huu haujaisha, upo. Leo nchi zote za Africa zimejitawala, baadhi zina miaka zaidi ya 50 na nyingine si chini ya miaka 30, lakini zote bado maskini na hazina nguvu. Sababu ni unyonge tu.

 

Watanzania walio waumini wa Ujamaa na wanaokiri kuwa Azimio la Arusha ni dira yao ya kuwapeleka kwenye Ujamaa ambao sasa haupo, wanatambua unyonge wao ni jambo la ukweli. Hata vijana wa sasa tunakiri ni wanyonge.

 

Pamoja na kuelezwa ndani ya Azimio la Arusha, “Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha, na ni unyonge wetu ndiyo uliofanya tukaonewa, tukanyanyaswa, tukapuuzwa. Sasa ni lazima tufanye mapinduzi ya kuondoa unyonge wetu ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na tusipuuzwe tana” bado ni wanyonge.

 

Kauli hiyo ni kubwa na muhimu sana katika kuondoa unyonge wa Mwafrika. La kusikitisha viongozi wetu wameipuuza na kuitupilia mbali. Leo bado tunaendelea kuombaomba na kujikomba tena kwa wale wale waliotuonea, waliotunyonya na kutupuuza.

 

Ni dhahiri shahiri Waafrika tumeshindwa kufanya mapinduzi ya kuondoa unyonge. Na tumeshindwa kutambua kwamba hakuna usawa duniani kama kuna unyonge. Kwa hiyo, Waafrika tusiamini wala kujipa matumaini kuwa tunaweza kusafiri pamoja na wenzetu (si Waafrika) katika safari ya historia ya binadamu, ikiwa sisi tutabaki wanyonge; lazima tutakokotwa!

 

Historia inatuambia huu ni unyonge wetu sisi, babu zetu hawakuwa nao na wala hawakuwa na sababu ya kuwa nao, walipinga na walipigana na mataifa ya nje kukataa unyonge huo wa moyo na umaskini. Lakini maarifa, silaha na nguvu zao hazikutosha kuyaondoa mataifa moyo (wakoloni).

 

Historia ikajirudia pale mababu zetu walipopata maarifa, hekima na busara mpya, walifanikiwa kuyaondoa  mataifa hayo chini ya vyama vya siasa vya ukombozi.

 

Pamoja na juhudi zote hizo, baada ya kujitawala wenyewe, viongozi wetu walianza mapambano ya wenyewe kwa wenyewe ya kutaka kuridhisha nyoyo na roho zao, eti  wawe kama wale watawala wetu wa zamani!

 

Wakaanzisha Afrikanaizesheni na kujipa utukufu huku wakiwakoga akina tata Kabwela, ambao ndiyo hasa waliokuwa mstari wa mbele kupigania uhuru na ukombozi wa Mwafrika.

 

Si hivyo tu, viongozi hao na vibaraka Waafrika wenzetu wachache waliratibu na kuanzisha mapigano ya kikabila, kisiasa na ya kidini kwa madai kuwa ni mapinduzi badala ya kuyaita maasi, ili washike madaraka na kustarehe kama mabwana zao wakoloni. Walisahau kabisa kwamba tulikuwa na sifa ya pili ya unyonge wetu, umaskini.

 

Mwafrika akaingia vitani kujipiga mwenyewe, huku akisaidia kuhamisha mali na maliasili za nchi yake, kupeleka kwa mabwana wakoloni; na kuharibu rasilimali za taifa na kubomoa miundombinu ya uchumi wake. Matokeo yake akabaki kwenye lindi la umaskini na kutembeza bakuli kuombaomba misaada kutoka mataifa yale yale yaliyomnyonya, yaliyomwonea na yaliyomnyanyasa.

 

Hivi majuzi tumeshuhudia kwa mara nyingine tena mataifa ya China na Marekani yakipigana vikumbo katika nchi za Afrika kutaka kuwekeza na kuendeleza uhusiano uliyopo kati yao na Afrika, huku wakijenga hoja za kuinua uchumi, kuanzisha biashara, kuboresha maisha ya Mwafrika na kulitoa Bara la Afrika katika kiza.

 

Ni kweli Marekani na China ni mataifa  makubwa kiuchumi, je, ni kweli biashara itafanyika kwa haki na usawa kati ya matajiri na maskini? Je, ni kweli dhamira yao ni kuitoa Afrika katika kiza na lindi la umaskini? Au wana nia ya kupora tena mali ya Afrika kwa njia ya ustaarabu, huku wakitumia nadharia na falsafa ya utawala bora, sayansi na teknolojia?

 

Kwa vyovyote iwavyo, maswali kama haya na mengineyo, yenye majibu chanya au hasi bado Mwafrika, na hasa Mtanzania ni mnyonge.  Watanzania tuwe waangalifu na makini zaidi katika utendaji wa shughuli zetu za kila siku, madhali viongozi wetu wameshakubali hoja za mataifa hayo na kusaini mikataba ya maendeleo.

 

Tunaingia ndani ya msitu na nyika uliotanda kiza na wanyama wakali wenye hila na mbinu kongwe za uwindaji. Uvukaji wa msitu huo unategemea sana viongozi bora, wanataaluma waadilifu na wafuasi welevu, makini na watiifu. Kinyume na hayo ndoto zetu za kutaka maisha bora kwa kila Mtanzania zitakuwa ndoto za mchana!

 

Tangu Rais Xi Jinping wa China na Baraka Obama wa Marekani walipotembelea nchi yetu na kutia saini mikataba ya miradi mbalimbali ya maendeleo na Rais wetu Jakaya Mrisho Kikwete, Watanzania wamegawanyika makundi matatu. Kundi lenye matumaini ya kuvuka msitu. Kundi lenye imani ya kutovuka msitu na kundi lililokata tamaa ya kuwa na maisha bora.

 

Makundi hayo yametokea na sababu zile za unyonge wa Mwafrika. Tumeshindwa kufanya mapinduzi ya kuondoa unyonge wa moyo; wa roho na umaskini. Kwa vile historia ina tabia ya kujirudia tayari mataifa ya nje yameanza kuingia nchini kwa misingi ileile ya uporaji na unyonyaji.

 

Watanzania saa ya ukombozi imefika. Tubadilike tuwe wapya na wa kisasa. Tusahau kushindwa kwetu katika kilimo cha kufa na kupona na siasa ni kilimo. Madhali tunaanza na mapinduzi ya Kilimo Kwanza, basi kisiwe kilimo cha mlimia dole. Tulime hasa mashamba makubwa na viongozi muwe wakweli, kilimo kishamiri tusiwe ombaomba.

 

Aidha, tuwe jeuri na wenye kujiamini kwani tulikwishafanya makosa ya kutelekeza suala la kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo vidogo na kuuza viwanda vikubwa kwa bei ya kutupa. Lazima tuamue nini tunachotaka cha kutunufaisha na mipango yetu ielekezwe katika shabaha.