Watanzania tunakinyanyasa,
tunakibeua Kiswahili – 7
Sina budi kutoa shukrani kwa wale wote walioniunga mkono katika mada hii ya Watanzania tunakinyanyasa na kukibeua Kiswahili. Ni dhahiri Watanzania wanatambua na wanajali lugha yao ya Kiswahili. Asante. Baadhi ya Waswahili wanasema kuwa lugha ya kaya, kabila, rika, masikani na vijiweni, na hata sehemu zetu za kazi, au michezo zisiwe ni vigezo kuwa Watanzania hawakithamini Kiswahili. Hizo ni lugha za msimu tu.
Ni lugha zinazojenga na kutia hamasa katika mawasiliano yao ya kuelewana, wakati wanapokuwa kazini, michezoni au vibarazani katika simulizi zao.
Wengine wanakuja na msimamo kuwa lugha hizo za msimu vijiweni zisipewe mashiko kama ndiyo lugha sanifu. Kuna hatari ya kuamini, ‘kura chakura’ ndiyo sahihi badala ya ‘kula chakula’ au ‘masaa’ saba tangu awasili mjini badala ya ‘saa’ saba tangu alipowasili mjini.
Pamoja na maelezo hayo machache, Waswahili hao wanakiri upo unyanyasaji, upotoshaji, ubeuaji hata hali ya kukebehi lugha wakati wa matumizi ya maneno ya Kiswahili na kuchanganya maneno katika kutoa maana halisi.
Kwa mfano, Mswahili mwenye simu namba HYPERLINK “tel:0787%20780190”0787 780190 amenitaka nitoe ufafanuzi wa maana ya maneno mhanga na mwathirika. Ni kweli maneno hayo mara kadhaa yametumika visivyo katika taarifa mbalimbali.
Mhanga ni mtu anayejitolea/anayejitosa kufanya kitendo au tukio la kuhatarisha akitambua atapata madhara. Kwa mfano, mtu anayejilipua na bomu na kufa. Huyu ndiye mhanga.
Juma amejitoa mhanga kupambana na simba. John amejitoa mhanga kupambana na watu wenye silaha kuokoa maisha yake.
Mwathirika ni mtu anayekumbwa na athari nzuri au mbaya. Kwa mfano, Mary ameathirika akili kutokana na milipuko ya mabomu kule Mbagala mwaka juzi. Pengo ameathirika na utamaduni wa watu wa Ulaya Magharibi, kwa maana anapenda utamaduni wa watu hao.
Mtu anayefikwa na maafa si mwathirika bali ni mgharimu. Kwa mfano, wanakijiji wa Tupendane ni Wagharimu wa mafuriko yaliyotokea mwezi uliyopita. George na Asha ni wagharimu wa maambukizo ya virusi vya UKIMWI tangu mwaka jana.
Baada ya ufafanuzi wa maana ya maneno mhanga, mwathirika na mgharimu, sasa tuangalie la msingi tufanye nini kulinda, kukienzi na kukisambaza Kiswahili duniani. Hii ndiyo changamoto iliyopo mbele ya kila Mswahili.
Magwiji wa Kiswahili nchini, wanadai na wanatetea dhahiri kuwa Kiswahili kina misamiati ya kutosha kukidhi semi mbalimbali kwenye taaluma za biashara, siasa, uchumi, sheria, ufundi, sayansi na teknolojia.
Vyombo vyenye dhima ya kukuza, kuendeleza na kuhifadhi lugha ya Kiswahili vina miswada mbalimbali iliyochapwa baada ya tafiti na makubaliano ya majopo kadhaa yaliyokutana na kupitisha rasimu hizo.
Hadi sasa, Baraza la Kiswahili Tanzania, Baraza la Kiswahili Zanzibar na taasisi za kuendeleza lugha ya Kiswahili zinasubiri kauli na uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuweka utambuzi wa kisheria kuwa Kiswahili ni lugha ya Taifa na ya kufundishia tangu shule za msingi hadi vyuo vikuu hapa nchini.
Takriban ni miaka 40 sasa Serikali bado ina kigugumizi kuweka kisheria lugha ya Kiswahili. Tatizo ni nini? Kadiri miaka inavyopita ndivyo Kiswahili kinavyosambaa duniani. Jinsi kinavyopanuka ndivyo kinavyokumba matumizi yasiyo rasmi.
Mathalani, uhalisia wa Kiswahili kupotea, utamaduni wa Kiswahili kupuuzwa na hata matumizi sanifu katika fasihi andishi na fasihi simulizi kupotoshwa kutokana na zama hizi za teknolojia na utandawazi.
Tayari nchi kadhaa katika mabara ya Afrika, Amerika, Ulaya na Asia baadhi ya vyuo vyao vikuu vinafundisha Kiswahili kama lugha ya mawasiliano. Je, tuna uhakika gani mafunzo yao yanazingatia kanuni na utamaduni wa lugha ya Kiswahili?
Ndipo hapo tunapoandikiwa na kuzungumziwa Kiswahili cha Ulaya. Kwa mfano, Kamata basi – to catch a bus. Kiswahili fasaha ni kupanda basi kwa maana ya kusafiri kwa basi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Vivyo hivyo, tunapoambiwa kuosha nguo – to wash the clothes – badala ya kufua nguo. Tunaandikiwa ni vizuri mtoto kuosha uso – to wash the face – badala ya kusema Kiswahili fasaha ‘kunawa uso’.
Katika mifano niliyotoa, sentensi hizo ni tafsiri sisisi ya Kiingereza katika Kiswahili. Kuna mifano mingi ya aina hiyo. Ndiyo kusema utamaduni wa lugha ya Kiswahili upo katika dalili ya kupotezwa.
Nahitimisha makala haya kwa kuiomba na kuisisitiza Serikali kukipa uwezo wa kisheria Kiswahili ndani ya Katiba ya nchi. Kama nchi jirani zimeweza, kipi kikwazo kwa wenyewe wa lugha ya Kiswahili kutoweza?
Ninaaga kwa wito wa bingwa na mpenzi wa Kiswahili, Sheikh Shaaban Robert (marehemu), alioutoa katika ubeti ufuatao:
Kiswahili kwa dhahiri, kimo ndani ya msitu,
Hili nimelifikiri, kwa muda wa siku tatu,
Na sasa nalihubiri, afahamu kila mtu,
Hima pakutane, au tutaihasiri.