Watanzania tunakinyanyasa, kukibeua Kiswahili – 4
“Hali yetu ya Kiswahili hivi sasa si nzuri. Kuna makosa mengi katika matumizi. Inaelekea ufundishwaji wa Kiswahili ni tatizo. Vipi Kiswahili kiwe tatizo wakati ni lugha ya msingi na Taifa? Taifa halijatoa umuhimu wa lugha ya Kiswahili, kifundishwe kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu. Lakini Kiswahili gani kifundishwe? Hata wanaojua Kiswahili wanakiharibu.”
Ni kauli ya gwiji la siasa nchini, mzee Kingunge Ngombale-Mwiru wakati akizindua kitabu cha historia ya Hayati Sheikh Kaluta Amri Abeid (1924-1964) kilichitungwa na Hayati Mathias Mnyampala, katika sherehe zilizofanyika Machi 12, 2013 katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Mzee Ngombale aliendelea kusema; “Unapokuwa na lugha inakupa uwezo wa fikra, dhana, rai, na kadhalika. Lugha ya Kiswahili ni muhimu kwetu na inaweza kutuunganisha watu wa Afrika Mashariki na Kati, zaidi Tanzania.”
Maneno hayo ni mazito na ni ujumbe kamili unaopaswa kuzingatiwa na kila mtumiaji wa Kiswahili, hasa Waswahili wa Tanzania ambao ni walinzi wa Kiswahili sanifu kinachotumika katika mawasiliano baina ya mtu na mtu.
Ukichambua kwa undani kauli hiyo, huna budi kutoka na hoja nzito ya Watanzania kukinyanyasa na kukibeua Kiswahili, na maswali mengi yanayohitaji majibu. Mathalani;
I. Kwa nini hivi sasa Kiswahili si kizuri sana?
II. Nani na kwa faida ya nani anayejenga na kuendeleza makosa mengi katika matumizi ya Kiswahili?
III. Je, ni kweli Taifa la Tanzania halijatoa umuhimu wa Kiswahili kutumika nchini?
Katika makala yaliyopita ya mada hii, niliwagusa viongozi wa Serikali na siasa; si wote; wanavyokibeua Kiswahili na kujali lugha ya kigeni, kwa kisingizio Kiswahili ni kigumu na hakina misamiati mingi kama vile katika fani ya uchumi, biashara, sayansi na ufundi.
Kama msemo huo ni kweli, ndipo mzee Ngombale-Mwiru anaposema kuwa inaelekea ufundishaji wa Kiswahili ni tatizo. Inakuwaje mahali ambapo vyombo vya utafiti, vya kukuza na kuendeleza na vyombo vya kufundishia vipo kisheria, lakini bado Kiswahili ni tatizo?
Ukweli vyombo vya kuratibu, kutafiti, kufundishia, kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili katika matumizi sanifu na fasaha vipo, na vyombo hivyo vinatoa vitabu na majarida mbalimbali kwa malengo hayo yaliyotajwa.
Kwa mfano, vipo vitabu vyenye mafunzo kuhusu umuhimu wa matumizi ya lugha sanifu ya Kiswahili. Kama vile; Kamusi Sanifu ya Isimu ya Lugha, Kamusi Sanifu ya Biolojia, Fizikia na Kemia, na Jifunze Kiswahili Uwafunze Wengine.
Kadhalika, yapo majarida ya matoleo ya tafsiri sanifu na lugha yetu tuisome tuijue. Kazi zote hizo na nyinginezo zinafanywa na Bakita, Tataki na Bakiza.
Kama hivyo ndivyo, bado mzee Ngombale-Mwiru anayo ya kusema. “Lugha inajengwa na uongozi.” Viongozi na jamii hatutilii maanani matumizi ya lugha yetu. Ndipo hapo unapokomelea na kusema, “Hali yetu ya Kiswahili hivi sasa si nzuri sana.”
Pili, anawausia watumiaji Kiswahili kuwa kifundishwe tangu shule za msingi hadi vyuo vikuu. Lakini bado anahoji, “Ni Kiswahili gani kifundishwe? Kwanini hata wanaojua Kiswahili wanakiharibu?”
Katika kauli hizo mzee Ngombale-Mwiru anasisitiza na kutoa changamoto kwa watumiaji Kiswahili kutumia Kiswahili sanifu na fasaha katika mawasiliano na kufundishia elimu na taaluma nchini. Anatoa indhari kwa viongozi wa Serikali na watumiaji Kiswahili kuwa kutumia Kiswahili kisicho sanifu na fasaha isiwe kigezo cha msingi kukataa Kiswahili hakina sifa ya kufundishia hadi Chuo Kikuu.
Nakubaliana naye katika rai na mawazo yake kwa sababu watumiaji Kiswahili wanaoweza kuathiriwa na kuhitilafiana katika nyadhifa zao, maumbile yao na kwa mujibu wa sehemu wanazotoka maadam kimeenea sehemu kubwa ya Tanzania.
Kutokana na kuenea huko, tuna makundi mawili ya watumiaji Kiswahili. Kundi la watumiaji Kiswahili tu, hawana lugha nyingine na kundi la watumiaji Kiswahili ambao wana lugha nyingine ya kwanza kutoka kwa mama zao.
Kundi la kwanza Kiswahili tu limeenea kuanzia Lamu na Visiwa vya Pemba, Unguja na Ngazija, na kusini, Pwani ya Kaskazini ya Msumbiji. Kiswahili chao si cha aina moja. Kuna Kimvita, Kilamu, Kiunguja, Kisii, Kimakunduchi, Kimrima, Kimtang’ata, na kadhalika.
Kundi la pili ni la watumiaji ambao wana lugha zao za asili. Katika makuzi yao wanakutana na Kiswahili shuleni na barabrani, na hao huzaa Kiswahili chenye mchanganyiko wa lugha zao za malezi. Hapa tunapata Kiswahili cha Kizaramu, Kisukuma, Kizanaki, Kihaya nk.