Watanzania tunakinyanyasa, kukibeua Kiswahili -3

Katika makala mbili zilizotangulia, niliandika kuhusu hofu na mashaka walionayo baadhi ya magwiji wa lugha ya Kiswahili, katika matumizi na malezi ya lugha hiyo kutokana na Waswahili kuonesha wazi dalili za kuipa umuhimu lugha ya kigeni katika matumizi.

Nirudie kusema lengo la makala haya si kutoa elimu au mafunzo ya lugha ya Kiswahili. Lengo na nia ni kuwakumbusha na kuwazindua Waswahili wasipende kushabikia lugha ya kigeni na kuzira lugha yetu iliyotukuza.

 

Ikumbuke kabla ya Uhuru wa nchi yetu, Kiswahili kilitumika katika shughuli zote za mawasiliano – ziwe za utawala, biashara, dini, au elimu, lakini bado kilikosa hadhi kama lugha ya Taifa.

 

Baada ya Uhuru, mwasisi wa taifa letu, Rais wa Kwanza wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, alipohutubia Bunge la Tanganyika kwa mara ya kwanza Desemba 10, 1962, alitumia lugha ya Kiswahili.

 

Kitendo hicho kilikuwa ni ishara ya kukienzi na kukipa hadhi Kiswahili; na kukitambulisha kama lugha ya Taifa. Ukweli wa jambo hilo ni pale Mwalimu Nyerere alipounda rasmi Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962.

 

Katika mchakato wa kukienzi na kukipa umuhimu Kiswahili, kilianza kutumika rasmi Bungeni mwaka 1963, na mwaka 1964 Serikali ya Tanzania ilitangaza rasmi Kiswahili kuwa lugha ya Taifa.

 

Si hivyo tu, baada ya kuundwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, vyombo kadhaa viliundwa kwa nia ya kusaidia wizara hiyo. Navyo ni Taasisi ya Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili (TUKI sasa TATAKI) mwaka 1964, na Chama Cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA) mwaka 1965.

Katika kutilia mkazo Kiswahili kilianza kutumika rasmi kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi, na kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), likiwa na jukumu la kukistawisha Kiswahili kama lugha ya Taifa.

 

Wakati wa harakati za kukuza na kuendeleza Kiswahili, wazo la kuandika Kamusi mpya lilibuniwa mwaka 1964 na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, likafanyiwa kazi na kukamilika Juni 1978, na mwaka 1981 tukawa na Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la kwanza na toleo la pili mwaka 2004.

 

Watunzi mbalimbali wa vitabu vya fasihi, riwaya, kiada na diwani walichomoza katika kukuza Kiswahili. Waandishi kadhaa wa majarida na magazeti wametoa machapisho yao kwa kutumia lugha sanifu na fasaha ya Kiswahili. Lengo na madhumuni ni kukuza, kuenzi na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

 

Watunzi wa mashairi, ngonjera, tenzi na nyimbo, muda wote wametumia lugha sanifu na falsafa kufikisha fikra, rai na maoni mbalimbali kwa walengwa wao.

 

Waghani na waimbaji wa mashairi, tenzi, ngonjera na nyimbo muda wote wamelinda istilahi na lafidhi za misamiati mbalimbali ya lugha ya Kiswahili bila kupotosha wala kutusi.

Watunzi wa nyimbo wamelinda urari na kuepuka lugha kali zenye matusi na kejeli za waziwazi. Wamepata kuonesha uwezo na upeo wa utunzi wao bila kunasibisha na tunzi za lugha nyingine, kwani kwao ni kichefuchefu.

 

Leo viongozi wa Serikali na wanasiasa hupendelea kutoa hotuba zao kwa lugha ya kigeni. Baadhi yao wanadai eti hawawezi kuandika hatuba kwa Kiswahili. Ni kigumu, ila hiyo lugha ya kigeni ni rahisi kwao.

 

Hii ni kasumba, utumwa wa mawazo na ulimbukeni wa lugha kama si kujipendekeza na kujishaua. Ukweli, anapoandika hotuba hiyo, ana kamusi mkononi ya lugha hiyo. Ili asije andika makosa ya kisarufi.

Swali: Kama wewe ni mpevu wa lugha hiyo, vipi uweke kamusi ya kisarufi pembeni mwako?