Watanzania tunakinyanyasa, kukibeua Kiswahili – 2
Juma lililopita nilizungumzia lugha yetu ya Kiswahili. Katika makala yale tuliona baadhi ya maandishi yenye kauli zinazoonesha mashaka au wasiwasi wa kunyanyaswa na kubeuliwa Kiswahili.
Kabla ya kuangalia dosari hizo, itoshe kusema Kiswahili kilianza kutambulika na kutumika kuanzia karne ya nane na Waswahili wa pwani kama lugha ya mawasiliano katika jamii ya maeneo hayo.
Kiswahili kilitumika kuanzia ndani ya familia, koo na hata kwenye jamii nzima ya Waswahili katika maeneo ya biashara, utawala, dini, elimu, utamaduni na mambo kadha wa kadha.
Katika mtiririko huo, Kiswahili kiliambukizwa hadi kwa wageni wakiwamo Wareno, Waarabu, Wajerumani na Waingereza walioishi na kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Ni ukweli, wageni walitumia Kiswahili kuendesha na kufanikisha masuala yao ya utawala, dini na biashara na kupinga kudumisha Kiswahili kama lugha bora ya mawasiliano katika nyanja za ustawi na tamaduni za Waswahili.
Mtazamo huo wa pili ndiyo ninaouzungumzia ambao hadi leo, baadhi ya wageni na wenyeji ndugu zetu wanakipuuza, wanakikejeli hata kukidhalilisha eti Kiswahili hakina misamiati, mathalan katika fani kama za biashara, ufundi na sayansi.
Wanaosema kasumba hiyo ni wale wanaojipurukusha kuwa Kiswahili ni kigumu na hakina misamiati, ilihali hizo lugha wanazozisifu zimetohoa maneno kutoka lugha nyingine. Mathalan, Kiingereza kina maneno mengi kutoka lugha za Kirumi na Kigiriki na kufanya lugha hiyo kuwa na sura duniani.
Wageni wana sababu ya kuthamini lugha yao, ili kulinda mila na tamaduni zao na kuwapatia umaarufu wa kutambuliwa. Wao kupinga na kuthamini Kiswahili ni kudhalilisha na kuua umaarufu wa mila, tamaduni na utambulizi wao.
Wewe Mswahili una sababu gani zinazokusukuma hata ukinyanyase na kukibeua Kiswahili? Mgeni anakuwa na lugha yake. Vipi wewe mwenyeji huwashwi na lugha yako?
Mababu na wazazi wetu waliona thamani na ubora wa lugha ya Kiswahili, kama walivyorithishwa na mababu zao. Walihakikisha wanalinda na kuendeleza lugha hiyo.
Hivyo, jukumu la kulinda na kuendeleza Kiswahili ni letu Waswahili. Hii ina maana kuwa dhana ya utamaduni wa lugha ya Kiswahili ni lazima iwe na mashiko maalumu kwa ajili ya kulea Kiswahili katika maendeleo yake.
Kinyume chake tusipokilea Kiswahili, kila mmoja akaachwa afanye lile analolitaka, basi lugha hii itakuwa imeparanganyika, na hapo ni kutoa mwanya kwa wapinga Kiswahili kubembea.
Ninachosisitiza hapa, kwa mfano, tunapozungumza dhana ya utamaduni au mila ya Kiswahili kwa maana ya tuna adabu zetu, huduma zetu na uadilifu wetu katika matumizi ya maneno ya Kiswahili zilindwe.
Zipo lugha mbalimbali katika matumizi yetu, kwa mfano baba na mtoto, mwalimu na mwanafunzi, mke na mume wanapozungumza wanakuwa na lugha yao. Kutotumika vizuri lugha za makundi hayo kunasababisha lugha kunyanyaswa.
Kwa mfano, mtoto anapomwambia baba yake, “Dingi mambo vipi?” Badala ya kusema, “Baba hali gani?” Mwalimu anapowaambia wanafunzi wake, “Wazushi mmedaka hiyo?” Badala ya kusema, “Wanafunzi mmeelewa somo?” Au mke anapomwambia mume wake, “Mshikaji wangu vipi tutaanza?” Badala ya kumwambia, “Mume wangu tutakwenda?”
Mifano mingine mamlaka yenye madaraka makubwa inapokataa kutumia Kiswahili sanifu katika neno ‘digit’ na badala yake kung’ang’ania kutumia neno digitali.
Tangazo la biashara linaposema, “Si kila king’aricho…” Badala ya kusema, “Si kila king’aacho…” Je, hii si kejeli dhidi ya lugha ya Kiswahili?