Ulimi mzuri utaimarisha uchumi Tanzania

Juma lililopita nilizungumzia thamani ya faraka ya matumizi ya ulimi wa mwanadamu. Ukitumika vizuri huleta rutuba chanya ya  maendeleo, na ukitumika vibaya huleta rutuba hasi ya maendeleo, iwe ya mtu kikundi cha watu ama Taifa.

Juma hili, nimesukumwa tena kuzungumzia matumizi mazuri ya ulimi, nikiangalia tukio la ziara ya kiserikali iliyofanywa na Rais wa China, Xi Jinping, na kupokewa nchini na Rais Jakaya Kikwete.


Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano mzuri iliopo baina ya nchi ya China na Tanzania, na kutambua sera yao ya mageuzi ya uwazi ya kuukuza uchumi na biashara kati ya China na Afrika.


Suala hilo la uhusiano kati ya China na Tanzania ndilo hasa ninalokusudia kulizumgumzia. Mataifa haya mawili yana tofauti ya idadi kubwa ya watu – China ina watu bilioni 1.3 na Tanzania ina watu milioni 45. Kitu gani kinawaunganisha kujenga na kuimarisha uhusiano?

 

China ina maendeleo makubwa ya uchumi, teknolojia na maendeleo ya jamii ukilinganisha na Tanzania yenye uchumi hafifu na tegemezi, teknolojia duni na maendeleo hafifu ya watu na makazi.


Yapo mengi ya kuzungumza na kulinganisha katika uchumi wa Taifa, pato la mtu kwa mwaka, elimu, taaluma, afya, na ustawi  wa jamii, sayansi na teknolojia na miundombinu ya kilimo, usafirishaji viwanda michezo na kadhalika kati ya mataifa hayo.


Hayo si malengo yangu kuzungumzia ingawa nitakayosema yatagusa watu katika maeneo hayo. Uchambuzi wa hayo niliyotaja yatafanywa na wachambuzi wa sera na dira za siasa, uchumi, taaluma sayansi na teknolojia. Lengo langu ni kukoleza thamani na umuhimu wa matumizi mazuri na bora ya ulimi katika kubuni, kujenga na kudumisha mipango mbalimbali ya maendeleo ya mtu na hasa maendeleo ya Taifa linalopewa misaada ya fedha, nyenzo za kazi, taaluma na mbinu za ujenzi wa uchumi.


Wiki iliyopita, Serikali ya China iliahidi kuendelea kutoa misaada zaidi bila masharti yoyote ya kisiasa, kwa nchi za Afrika katika kuimarisha uhusiano wa asili ambao hauwezi kuvunjwa, kwani uchumi wa China unategemea zaidi Afrika na Afrika inategemea uchumi wa China unaokua kwa kasi.


Pamoja na ahadi hiyo, Serikali ya China imeshukuru Serikali ya Tanzania kuiwezesha China kupata nafasi nzuri ya kufanya shughuli mbalimbali kwa maslahi ya nchi hizo mbili.

Kauli hizo zimetolewa na Rais Xi alipokuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania Machi 24 hadi 25, mwaka huu.


Alichofanya Rais Xi ni kuamsha na kukoleza rai, mawazo na mitazamo ya waliokuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa China, Mao Tse Tung na Rais wa Jamhuri ya Muungno wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, walipokutana kwa mara ya kwanza nchini China Februari 1964, na kuweka misingi ya uhusiano huo ambao leo tunauzungumzia.


Katika kuamsha na kukoleza uhusiano huo, jumla ya mikataba 19 ikiwamo ya mikopo ya fedha, ujenzi, miundombinu ya kilimo, uboreshaji matangazo ya TBC, mafunzo, utamaduni na uchumi ilisainiwa.


Hayo yote yasingeweza kama ulimi wa Serikali ungekuwa wa pilipili, yaani mchafu, kwa hiyo  watendaji wa Serikali nawasihi waache lugha chafu wanapofanya kazi za miradi na mipango iliyopitiwa na serikali hizo.

 

Watendaji waandamizi wa Serikali na taasisi zake waache ufisadi na undumilakuwili (double standard), katika kusimamia na kueleza njia bora za utekelezaji wa miradi iliyotolewa.

 

Wananchi ambao ni wafanyakazi nao waache udokozi, wizi na kuhujumu miradi, na mipango itakayopangwa. Wasipofanya hivyo hawatakuwa wamezikomoa serikali hizo bali watakuwa wamejikomoa wenyewe na kujitia umaskini wa kudumu.


Wachina wanapojaribu kutusaidia kukuza uchumi wa Tanzania wao hawakusaidiwa na taifa lolote, walijiuliza na kujipanga kujinasua kutoka katika uchumi duni kwenda katika uchumi bora na wa uhakika, wa kutunga sera na kufanya mabadiliko mbalimbali kisiasa na kiuchumi.


Wiki iliyopita, China ilishiriki mkutano wao wa umoja wa nchi tano zinazokua kiuchumi huko Afrika Kusini, kuzungumzia uchumi na kusudio la kuanzisha Benki ya Kimataifa ili kuikimbia Benki ya Dunia (WB) na Shirikisho la Fedha Duniani (IMF).


Umoja huo unajulikana kama BRICS ikiwa na maana ya nchi za Brazil, Russia, India na Afrika Kusini. Una matarajio makubwa ya kuwa na uchumi bora na wenye nguvu katika nchi hizo duniani.


Watanzania mpo wapi? Na mnafanya nini?  Amkeni, huu si wakati wa watu kujilimbikizia mali za ufisadi na kujenga majumba ya fahari. Tanzania inahitaji maendeleo ya watu, umoja na mshikamano kiuchumi.


Namalizia kwa kusema ulimi fasaha, vitendo adilifu, uungwana na uzalendo ni nguzo muhimu katika kujenga na kudumisha uchumi wa Tanzania. Tanzania bila uchumi tegemezi inawezekana.