Serikali isipuuze, udini upo, iudhibiti (6)
Katika sehemu ya nne na ya tano ya makala haya, nilieleza maana ya udini kama ilivyoainishwa na baadhi ya viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo.
Kwa ufupi, udini ni ubinafsi, upendeleo na dhuluma dhidi ya haki unaofanywa na mtu, kikundi au madhehebu ya dini nyingine kwenda kwa watu, kikundi ama madhehebu mengine kwa lengo la kumdhibiti na kumnyima maendeleo.
Mfumo Kristo au mfumo Katoliki na mihadhara ya dini ya Kiislamu na Kikristo, yote inalalamikiwa na wenye dini hizo kuwa inaleta udini na kuashiria uvunjifu wa amani na utulivu nchini.
Katika makala zile nilitoa mifano michache kuhusu wamisionari walivyoendesha shughuli za kutoa elimu kwa wananchi, kwa upendeleo wa dini ya Kikristo. Shabaha ni kusimika chuki, ubaguzi na kujenga matabaka – tabaka la wasio na elimu na la wenye elimu. Lengo wenye elimu kulipa nguvu Kanisa kuhusu imani ya kiroho na lipate kushiriki kikamilifu katika utawala wa Serikali na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Katika makala ya leo nitajaribu kuonesha mihadhara michache ya Kiislamu na ya Kikristo ilivyoendeshwa kabla na baada ya Uhuru wa nchi, ili tuone ni kweli inaleta chuki, kejeli, kashfa na uchochezi nchini?
Mihadhara ya Kiislamu imekuwa ikifanyika wakati wa kuadhimisha siku tukufu kama vile mazawa ya Mtume Mohamad (SAW) na siku za miraji, jitimai na mfungo wa Ramadhani.
Madhumuni mengine ni kuhamasisha Waislamu wengi mambo ya dini yao kwa wakati mmoja, badala ya kutegemea misikiti, ambayo haiwezi kuchukua watu wengi, mathalani watu laki moja au mbili kwa wakati mmoja.
Mihadhara ya Kiislamu inapofanyika daima hutoa elimu ya dini ya Kiislamu inayobeba elima mwongozo na elimu mazingira, kwa maana ya kuelewa Uislamu na fadhila zake na mambo gani Mwislamu ayafuate na kutenda.
Lakini mara kadhaa, Wakristo wamekuwa wakilalama kuwa mihadhara hiyo inayoendeshwa nchini inatoa lugha za matusi na kashfa kwa dini nyingine hasa Ukristo; kana kwamba kuamini dini tofauti ni kosa.
Kweli mihadhara ya Kiislamu inazungumzia vazi la kanzu, kilemba na kofia ni mavazi matakatifu, wala si mavazi ya shetani kama inavyohubiriwa na baadhi ya madhehebu ya Kikristo katika mihadhara yao.