Mahakama Kuu kanda ya Tanga, inatuhumiwa na familia ya Ramadhan Athuman Mohamed, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kula njama na kusafirisha dawa za kulevya katika Basi la Tawakal, kuwa haikumtendea haki.
Familia ya mfungwa huyo ambaye alihukumiwa kifungo Mei, 2015 kwa kosa la kula njama na kusafirisha dawa za kulevya, inasema ndugu yao ameonewa kwa kiwango kikubwa na kuituhumu idara ya mahakama kwamba haikumtendea haki Ramadhani Mohamed katika hukumu hiyo.
Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Amour Khamis, Mei 29, 2015. Katika hukumu hiyo, Jaji anasema kosa la kwanza lilikuwa kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu, sambamba na kifungu cha 22(a) na 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2002.
Familia imejipanga kukata rufaa kuhakikisha shauri hilo linaitishwa upya na kusikilizwa na mahakama ya rufani, ingawa inasema inafanyiwa mizengwe hata kupewa nakala ya hukumu kutokana na mfanyabiashara mwenye masilahi na kesi hiyo.
Familia ya Ramadhani Mohamedi, ambaye alikuwa dereva, inalalamikia hukumu hiyo, kwa kitendo cha kutomhusisha mmiliki wa magari ya Tawakal, ambaye gari lake lilihusika kubeba dawa za kulevya aina ya heroini kilo 2.984 zilizokuwa na thamani ya Sh milioni 134.
“Upande wa mashitaka ulishindwa kutoa ushahidi wa kuthibitisha madai ya kula njama …alisema kitendo cha kutokuwapekua abiria kabla ya kupanda Basi, inakuwa ngumu kwa kuhusisha dawa hizo za kulevya na dereva, maana zinaweza kuwa ni bidhaa za abiria yoyote,” ananukuliwa wakili wa Ramadhani Mohamedi katika hukumu hiyo.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo ambayo JAMHURI, imepata nakala yake, wakili wa mtuhumiwa, amenukuliwa akisema, kama ambavyo upande wa mashitaka umeweza kuiambia mahakama kwamba dawa za kulevya zilikutwa chini ya kiti cha dereva, anajenga hoja pia kulikuwa na keki na biskuti katika kiti cha dereva, anahoji kwamba ina maana hivyo vyote vilikuwa ni mali ya dereva?
Familia ya dereva huyo aliyefungwa kwa makosa hayo mawili, inasema kumekuwa na hujuma dhidi ya ndugu yao. Wanasema hapakuwa na mkataba baina ya Ramadhan Mohamed na kampuni ya mabasi ya Tawakal, huku wakituhumu kwamba hata mkataba uliopelekwa makahamani kama sehemu ya uthibitisho ulikuwa umeghushiwa.
“Inawezekanaje kunakuwa na mkataba ambao unaelekeza majukumu ya mwajiliwa huku ukikaa kimya kuhusu stahiki zake? Lakini cha ajabu hata Ramadhan anasema kwamba hajawahi kusainishwa mkataba na kampuni yake hiyo,” anasema mwanafamilia mmoja.
Anaongeza, “Haiingii akilini kwamba gari lililokuwa limebeba dawa za kulevya amerudishiwa mwenye nalo, kitendo ambacho ni kinyume na sheria. Lakini pia kumekuwa na jitihada zinazofanywa na wamiliki wa kampuni hiyo ya mabasi kuhakikisha kwamba sisi hatuendi kokote katika kutafuta haki za ndugu yetu,”
Katika hukumu hiyo ambayo Ramadhan Mohamed alifungwa miaka 20, pia anapaswa kulipa faini Sh milioni 402 akimaliza kifungo.
Juhudi za kuupata uongozi wa makama kuzungumzia ukimiya wao katika upande wa mmiliki wa gari na kuizunguza familia kupata nakala ya hukumu hazikuzaa matunda baada ya kuambiwa na afisa mmoja wa Mahakama Kuu kuwa “ikiwa kumetokea upungufu katika hukumu, familia ikate rufaa.”