Rais wa Marekani, Barack Obama, mke wake, Michelle, watoto wao, Malia na Natasha (Sasha) ni familia ya wanamichezo mahiri.

Familia hiyo ipo hapa Tanzania kwa ziara ya siku mbili, ukiwa ni ugeni ulioweka historia ya pekee kutokana na kuwekewa ulinzi mkubwa kuliko ugeni wowote uliopata kuzuru hapa nchini.

 

Marekani ndiyo nchi yenye nguvu kubwa za kijeshi na kiuchumi kuliko taifa jingine lolote duniani.

 

Wakati Obama akifahamika kama mchezaji mahiri wa mpira wa kikapu tangu utotoni, mke wake, Michelle inasadikika ni moto wa kuotea mbali katika mchezo wa tenisi, miongoni mwa michezo mingine.

 

Michezo inatajwa kuwa ni miongoni mwa vitu vilivyochangia kuwakutanisha na hatimaye wakaweza kufikia hatua ya kujenga uhusiano ambao baadaye ulizaa tunda la wao kufunga pingu za maisha (ndoa).

 

Kwa upande mwingine, watoto wa Obama na Michelle nao wamedhihirika kufuata nyayo za wazazi wao katika suala la michezo.

 

Inaelezwa kuwa watoto hao licha ya kujijengea utamaduni ya kushiriki michezo mbalimbali wamejikita zaidi katika mchezo wa tenisi, mchezo uliomtangaza zaidi mama yao ndani na nje ya Marekani.

 

Barack Obama mwenye asili ya Afrika, alizaliwa Agosti 4, 1961 huko Honolulu – Hawaii, Marekani wakati Michelle yeye alizaliwa Januari 17, 1964 Chicago – Illinois nchini humo.

 

Malia alizaliwa Julai 4, 1998 na mdogo wake, Natasha anayejulikana zaidi kama Sasha alizaliwa Juni 10, 2001 huko Marekani.