Msimu uliopita, mshambuliaji wa Atletico Madrid, Falcao, alifunga mabao 23 katika Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), hatua iliyomfanya awe wa tatu nyuma ya Cristiano Ronaldo wa Real Madrid, lakini wote wakiongozwa na mwanasoka bora wa dunia anayeichezea Barcelona, Lionel Messi.
Wachezaji walioburuzwa na Falcao na mabao yao kwenye mabano ni Gonzalo Higuain (22), Karim Benzema (20) wote wa Real Madrid, Roberto Saldado wa Valencia na Fernando Llorente wa Atletico Bilbao waliofunga 17 kila mmoja.
Wengine waliopata mabao zaidi ya 10 lakini chini ya 20 ni Arouna Kone wa Levente na Miguel Perez Cuesta wa Rayo Vallecano (15), Ruben Castro wa Real Betis (14), Alvaro Negredo wa Sevilla FC (13), Carlos Vela wa Real Sociedad, Alexis Sanchez na Miku wa Getafe ambao kila mmoja waliwapeleka marikiti makipa mara 12.
Waliofunga mabao 10 kila mmoja ni Xavi Alonso wa Barcelona, Manu wa Sevilla FC, Raul Garcia wa Osasuna, Imanol Agirretxe wa Real Sociedad, Diego da Silva Costa wa Rayo Vallecano, Rondon wa Malaga na Jonas aliyeichezea Valencia.
Kundi la wachezaji waliozitikisa nyavu za timu za wapinzani wao dimbani mara tisa ni Cesc Fabregas wa Barcelona, Santi Carzola wa Malaga aliyehamia Arsenal ya England, David Barral wa Sporting Gijon, Marco Ruben wa Vallerreal na Victor Casadesus wa Mallorca.
Michuano ya La Liga inayoshirikisha timu 20 ilihitimishwa kwa Real Madrid kuwa bingwa baada ya kujikusanyia pointi 100 kutokana na mechi 38 ilizocheza, ikashinda 32, kutoka sare mbili, kupoteza mbili, kufungwa mabao 32 huku ikitikisa nyavu mara 121.
Ilinyakua kombe hilo kutoka kwa waliokuwa mabingwa watetezi, Barcelona iliyopata pointi 91 ambazo ni tisa nyuma ya Real Madrid, ikashinda mechi 28, kupoteza saba, ikatoa sare saba, kupoteza tatu, ikafungwa mabao 29 ambayo ni machache kuliko zote na kufunga 114 yakiwa ni pungufu ya mabao saba kwa vinara wapya na mahasimu wao hao.
Timu ya Atletico Madrid anayoichezea Falcao ilishika nafasi ya tano ikitanguliwa na timu hizo mbili – kisha Valencia na Malaga. Ilijikusanyia pointi 56 baada ya kushinda mechi 17, kutoa sare 11, kupoteza 12, kufunga mabao 53 huku yenyewe ikikung’utwa 46.
Baada ya karibu timu zote kuwa zimecheza mechi nne kila moja isipokuwa chache, kama ilivyokuwa msimu uliopita, Messi bado anang’ara akiwa tayari ameifungia Barcelona mabao manne akifuatiwa na Falcao aliyemzidi bao moja. Hata hivyo, mchezaji huyo ana mabao sawa na kina Jorge Molina wa Real Betis na Tomer Hemed wa Mallorca, yale ambayo ni sawa na wastani wa bao moja kutokana na kila mechi walizocheza huku Cristiano Ronaldo akizifumania nyavu mara mbili tu.
Tofauti na wenzake, Falcao ndiye aliyeonesha uwezo mkubwa zaidi dimbani na tayari timu nyingi kubwa barani Ulaya zinataka kumng’oa kutoka Atletico Madrid, jambo linaloweza kumfanya awe mmoja kati ya wanasoka walionunuliwa kwa dau kubwa kabisa duniani.
Ronaldo ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Ureno na mmoja kati ya wachezaji nyota wanaopewa nafasi ya kubwa ya kuibuka Mwanasoka Bora wa Dunia wa mwaka 2012/2013, alitumbukiza wavuni mabao 46 msimu uliopita akizidiwa manne na Messi aliyefunga 50.
La Liga, miongoni mwa Ligi Kuu ngumu na bora zaidi duniani ikifuatiwa na ya England, Ujerumani na Italia, msimu huu inaweza kuibua ushindani mkubwa zaidi katika upachikaji wa mabao kati ya Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Falcao iwapo hatahamia Chelsea anakowindwa kwa udi na uvumba. Lakini akibaki hadi mwisho wa ligi hiyo, Falcao anatarajiwa kumchachafya vikali Ronaldo katika mbio hizo, lakini hapewi nafasi yoyote ya “kubishana” na Messi kwa “kucheka” na nyavu dimbani kwa vile nyota huyo wa Argentina bado anang’ara.