Kuongezeka kwa mawakala wa benki kwa zaidi ya mara 30 tangu mwaka 2013 kumesaidia kwa kiwango kikubwa kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi na kuifanya biashara hiyo kuwa chanzo kizuri cha ajira na mapato kwa kaya mbalimbali.
Kwa hivi sasa huduma hiyo inatolewa na benki 16, ikilinganishwa na benki nne miaka saba iliyopita wakati idadi ya mawakala ilikuwa 591 tu.
Hadi mwishoni mwa mwaka jana, idadi ya mawakala wa benki nchini ilifikia 22,481 ambayo ni mara 37 ya idadi ya watoa huduma hiyo waliokuwepo mwaka 2013, likiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 3,700.
Kutokana na ongezeko hilo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inasema sasa hivi wananchi wanapata huduma za fedha karibu zaidi kuliko ilivyokuwa zamani. Hali hii pia imechangiwa kwa kiasi kikubwa na utoaji wa huduma za kifedha kidijitali na kupitia simu za mikononi.
“Taasisi za fedha zimeendelea kusambaa sehemu mbalimbali nchini na mpaka sasa kuna benki za biashara na taasisi za fedha 61 zenye matawi 838 nchini. Aidha, Benki Kuu imekuwa ikisisitiza upatikanaji wa huduma karibu na wananchi, na hadi hivi sasa kuna jumla ya mawakala 22,481 wa benki ambao wanatoa huduma moja kwa moja kwa wananchi; na kuwa kiungo muhimu kati ya wananchi na taasisi za fedha,” Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, alisema hivi karibuni.
“Aidha, utoaji wa huduma za fedha kwa wananchi na watoa huduma umeongezeka ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa njia mbadala za utoaji huduma za fedha kielektroniki na kupitia simu za mikononi. Hivyo, kwa sasa wananchi wanapata huduma za fedha karibu zaidi kuliko ilivyokuwa zamani,” aliongeza.
Katika ripoti ya hivi karibuni ya Usimamizi wa Sekta Fedha, Prof. Luoga anasema BoT inaridhishwa na ubunifu unaofanywa na taasisi za fedha ambao umeziwezesha benki kuongeza amana kwa gharama ndogo huku zikiimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha.
Kwa mujibu wa gavana huyo, Benki Kuu itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya mifumo ya malipo ya kidijitali na mawakala wa benki kufanya kazi vizuri. Pia itazisaidia taasisi za fedha kubuni bidhaa na huduma mpya huku ikizingatia masilahi mapana ya watumiaji wa huduma hizo.
Ripoti hiyo iliyotolewa mwishoni mwa mwezi Februari inasema idadi ya mawakala wa benki iliongezeka kwa asilimia 77 kati ya mwaka 2017 na 2018 kutoka 10,070 hadi 18,827. BoT inasema pia kumekuwepo na ongezeko la miamala ya kibenki kupitia kwa mawakala na kiwango cha fedha kilichohusika.
Idadi ya miamala ya fedha zilizowekwa na wateja kupitia mawakala iliongezeka kutoka milioni 9.9 hadi milioni 18 kati ya miaka hiyo miwili, huku thamani ya pesa iliyohusika ikiongezeka kutoka Sh bilioni 4,638.55 hadi Sh bilioni 10,278.3.
Upande wa kutoa pesa, mawakala wa benki walihusika kufanyika kwa karibu miamala milioni 4.1 yenye thamani ya Sh bilioni 1,106.37 mwaka 2017 na miamala milioni 9.8 yenye thamani ya Sh bilioni 3,070.48 mwaka uliofuata.
Takwimu za BoT zinaonyesha kuwa vinara wa huduma hii kufikia mwaka 2018 walikuwa ni CRDB Bank, NMB Bank Plc, Equity Bank Tanzania Ltd na NBC Limited.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, taasisi hiyo kwa hivi sasa inao mawakala zaidi ya 14,000 ambao wamesambaa nchi nzima.
Mkoa unaoongoza kwa kuwa na mawakala wengi ni Dar es Salaam, ukifuatiwa na Arusha, Mwanza na Mbeya.