*Awapongeza kwa kushusha gharama za uagizaji mafuta
* Asisitiza EWURA kudhibiti vitendo vya urasimu na rushwa mahali pa kazi
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka Watendaji na Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuzingatia maslahi ya Watanzania na maslahi ya nchi katika kazi zao za Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ili Watanzania wapate huduma bora na kwa unafuu mkubwa.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati akifungua Kikao cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kilichofanyika tarehe 8 Novemba, 2023 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemalira Rutatinwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Bi. Ziana Mlawa.
“Tambueni kuwa Taifa lina mategemeno makubwa na ninyi, hivyo fanyeni kazi zenu kwa weledi na ubunifu mkubwa unaoendana na kasi ya teknolojia na maendeleo ya dunia; kanuni na miongozo yenu mnayotumia katika utekelezaji wa majukumu iundwe katika mifumo rafiki kulingana na hali iliyopo ili ilenge kuleta matokeo chanya kwa ustawi wa Taifa na hivyo Watanzania waendelee kupata huduma bora na kwa gharama stahiki.” Amesema Dkt. Biteko.
Pia amewataka Watumishi wa EWURA kuweka mkazo kwenye kudhibiti vitendo vya urasimu na rushwa mahali pa kazi, kutoangalia maslahi binafsi wakati wa kutenda kazi ili kuepusha kuwaumiza Watanzania walio wengi, na ametoa wito kwa wafanyakazi hao kumkemea mtu yeyote anayeonekana kuwa na vitendo vya rushwa na ubinafsi katika eneo la kazi.
Vilevile, amewasisitiza Wafanyakazi wa EWURA kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao kwa kuhakikisha kuwa Watoa Huduma wanafanya ushindani wenye tija na ufanisi wa kiuchumi, kulinda maslahi ya Walaji na mitaji ya kifedha ya Watoa Huduma pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma kwa makundi yote ikiwemo ya watu wanaoishi vijijini.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu ameipongeza EWURA kwa kupitia upya gharama za uagizaji wa mafuta ambazo amesema kuwa, awali zilikuwa kubwa na zilikuwa zikipelekea athari mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa gharama katika Sekta ya Usafirishaji na Uzalishaji.
“Gharama hizi za uagizaji mafuta zilikuwa kubwa mno huku kukiwa hakuna sababu ya kuwa kubwa kwa kiasi hicho, niliwapa maelekezo mkazitazame upya, nashukuru mmeziangalia na ninafurahi kwamba zimeshuka na hivyo kupunguza makali kwa watumiaji.” Amesema Dkt. Biteko.
Vilevile Naibu Waziri Mkuu ameiagiza TUGHE- Taifa kueleza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuhusu masuala ya Wafanyakazi akitolea mfano upandishwaji madaraja wa mseleleko kwa watumishi ambao hawajapanda madaraja kwa muda mrefu. Amewataka pia kuwashirikisha wanachama wao ili kuisaidia Serikali katika kupeleka maendeleo kwa wananchi na pia kuikumbusha Serikali kutimiza wajibu wake kwa Wafanyakazi.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile alisema kuwa, Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi lengo likiwa ni kuhakikisha Huduma za Nishati na Maji zinapatikana kwa uhakika, kwa kutosha, kwa uendelevu na kwa gharama ambazo wananchi wanazidumu.
Alimshukuru, Dkt. Biteko kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Taasisi hiyo na miongozo anayotoa ambayo inafanya EWURA iendelee kuboresha utendaji wake katika kuhudumia Watanzania.
Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa EWURA kinachoendelea jijini Dodoma kimelenga kujadili masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa Bajeti ya EWURA kwa mwaka 2022/2023 na Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za EWURA za mwaka 2022/23.