Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewazawadia wahitimu wawili bora wa Chuo cha Maji, Florence Theonist na Emmanuel Nyaki, kompyuta mpakato na fedha taslimu shilingi milioni sita (milioni 3 kwa kila mmoja) kama sehemu ya kutambua juhudi zao katika masomo na kuwahamasisha vijana wengine kujiunga na kozi za zinahusu masuala ya maji.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (Mb), amewakabidhi wahitimu hao, zawadi hizo wakati wa mahafali ya 48 ya Chuo cha Maji yaliyofanyika Novemba 13, 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Waziri Aweso alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo.

Florence Theonest, amehitimu Stashahada ya Uhandisi wa Ugavi wa Maji na Usafi wa Mazingira, na Emmanuel Nyaki, Stashahada ya Teknolojia ya Maabara ya Ubora wa Maji katika Chuo cha Maji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA baada ya hafla hiyo, David Linda, Mhandisi Mwandamizi wa Maji na Usafi wa Mazingira alibainisha kuwa lengo la zawadi hizo ni kuhamasisha vijana wengi kujiunga na kozi za sekta ya maji ili kuwa na wataalamu wengi watakaosaidia katika kutoa huduma bora na kuchangia maendeleo ya sekta hiyo.

“EWURA, kama mdhibiti wa sekta ya maji, inatambua umuhimu wa kuwa na wataalamu wa kutosha ili kutoa huduma bora. Moja ya malengo endelevu ya dunia (SDGs) ni kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wote. Hili halitowezekana kama hatutakuwa na wataalamu wa kutosha. Ndio maana EWURA iko mstari wa mbele kushirikiana na Chuo cha Maji ili kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kufanikisha lengo hili,” alisema Linda.

Florence Theonest, mmoja wa wahitimu waliotunukiwa, aliishukuru EWURA kwa zawadi hiyo na kueleza kuwa kompyuta aliyopokea itamsaidia katika kazi za kiufundi, hasa ikizingatiwa kuwa shughuli nyingi za uhandisi wa maji zinategemea programu mbalimbali za kiteknolojia.

Kwa upande wake, Emmanuel Nyaki alitoa mwito kwa wanafunzi wanaosoma kozi zinazohusiana na sekta ya maji kuongeza juhudi katika masomo yao, akisisitiza kuwa ujuzi wa kitaalamu ni muhimu kwa maboresho ya sekta ya maji nchini.