Na Mwandishi Wetu,Iringa

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Leo 11 Nov 2022, wamezuru Hifadhi ya Wanyama Ruaha kujionea vivutio mbalimbali na kuchangia ukuaji wa mapato yatokanayo na utalii
nchini.

Wajumbe hao ni miongoni mwa wadau walioshirikiana na uongozi wa Mkoa wa Iringa kufanya ziara hiyo iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Halima Dendego kwa lengo la kuhamasisha watanzania kujiwekea desturi ya kutembelea hifadhi hiyo na vivutio mbalimbali vinavyopatikana mkoani humo.

Akizungumzia  wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa EWURA, ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Modestus Lumato amesema wajumbe wa Baraza wameona ni vyema kuunga mkono jitahada za Mkoa wa Iringa na za Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha na kutangaza utalii.

“Sisi wajumbe wa Baraza baada ya kutembelea hifadhi hii ya Ruaha, tutakuwa mabalozi katika kutoa hamasa kwa wenzetu tuliowawakilisha ili hata wasipokuja wakiwa kazini, waweze kuja na familia zao hapa,” ameeleza Mhandisi Lumato.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe,Halima Dendego, amesema “Niwaeleze tu kwamba, mkoa wetu wa Iringa kwa kushirikiana na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini tumejipanga na kujizatiti kufungua utalii wa ndani, hivyo niwaombe watanzania wenzetu tuunge mkono kwenye hili.”

Naye Mjumbe wa TUGHE Tawi la EWURA Bi .Stephania Bachubire, ameeleza kufurahishwa kwake na ziara hiyo na ametumia fursa hiyo na kuiomba Menejimenti ya EWURA kuandaa ziara kama hiyo kwa wafanyakazi wote.

Hifadhi ya Ruaha ina uoto asili wa kuvutia, ikiwamo mto Ruaha wenye viboko wengi na mamba sanjari na wanayama wengine kama tembo, chui, simba,nyati, ngiri,twiga, pundamilia, na wanyama jamii ya swala.

Wajumbe wapatao 60 wa Baraza la Wafanyakazi wa EWURA pamoja na wajumbe wa TUGHE wameshiriki ziara hiyo.