Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Morogoro
BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA CCC) kwa uwezeshwaji wa EWURA limefanya mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe 150 wa Kamati za Watumiaji wa Nishati, Maji na Gesi asilia za Mikoa 26 ya Tanzania bara ili kuboresha utekelezaji wa majukumu ya kuwatetea watumiaji.
Mafunzo hayo yanayofanyika mkoani Morogoro yanalenga kuwajengea uwezo wajumbe hao kulifahamu Baraza na majukumu yake, taratibu za uendeshaji wa Ofisi za mkoa, majukumu ya Kamati za mikoa pamoja na udhibiti kwenye sekta ya Nishati na Maji.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu,Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji Dk. James Andilile,Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki Mhandisi Musira Nyirabu amewataka wajumbe hao kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao kwa kujitoa kwa dhati kufikia vipaumbele vya kiutendaji.
Ametumia nafasi hiyo kulielekeza Baraza hilo kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati hizo ili ziweze kutekeleza vyema majukumu yake na kueleza kuwa ikiwa kuna changamoto za kiutendaji Baraza linapaswa kuwasiliana na mdhibiti kuona namna ya kuzitatua.
“Kazi ya Wajumbe hawa ni kutetea watumiaji katika mikoa yao ambako ndiko watanzania wanaishi,hawa ni wawakilishi wa EWURA CCC katika mikoa yao, uwajibikaji na mshikamano wao ndiyo njia pekee itakayowezesha huduma za Nishati na Maji kuwa zenye ubora unaokubalika na watumiaji, “amesema.
Aidha amelishauri Baraza kuyafanya mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe yakawe endelevu ili kuendana na wakati kutokana na mambo mengi kubadilika akitolea mfano wa urekebishwaji wa kanuni na kwamba bila kuendana na wakati wajumbe wanaweza kujikuta wakitumia taarifa zilizopitwa na wakati na kupotosha Umma.
Pamoja na mambo mengine Mhandisi huyo amelitaka Baraza hilo kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ili kuziwezesha Kamati hizo kujipanua katika kuwafika wananchi wa pembezoni kuelewa namna ya kuwasilisha malalamiko yao pindi wanaposhindwa kupata huduma zenye ubora.
“Watumiaji wengi hawana uelewa kuhusu haki na wajibu hata wanapokuwa hawajaridhishwa na huduma wamekuwa hawaelewi pa kulakamikia, kupitia mafunzo haya ninawaagiza mkajikite kuhakikisha elimu hii inawafikia ikiwa ni pamoja na kusoma sheria, Sera, kanuni na miongozo ya usimamizi huduma za Nishati na Maji, “amesisitiza na kuongeza;
Niwasihi mkajidhatiti kutoa elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu haki na wajibu wao, hii itasaidia wao kufanya maamuzi na matumizi sahihi na endelevu ya huduma za Nishati na Maji na watachangia katika kuboresha huduma hizo nchini, kwa upande wetu sisi EWURA tupo tayari kushirikiana nanyi kwa maslahi ya watumiaji, “amesema.
Pia ametoa wito kwa watoa huduma za Nishati na Maji kote nchini zikiwemo Mamlaka za Maji, TANESCO pamoja na vituo vya mafuta ambao ni miongoni mwa wadau wakubwa wa Baraza kutoa ushirikiano wa dhati kwa Baraza na wajumbe wa Kamati za mikoa ili kutatua changamoto za wananchi kwa wakati.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa EWURA CCC Stella Lupimo amevitaja baadhi ya viashiria vya kiutendaji kwa wajumbe wa Kamati za mikoa kuwa ni pamoja na kuwajengea uelewa watumiaji kwa kutoa elimu kwa makundi 12 ya watumiaji huduma zinazodhibitiwa na EWURA kwa mwaka.
Vingine ni pamoja na kushiriki kwenye programu nne kwa mwaka za uelimishaji zenye ufadhili wa Baraza, kupokea malalamiko na kusaidia walalamikaji watumiaji angalau 20 wenye malalamiko na kuwaelekeza namna ya kulakamika, kufikia na kuelimisha wadau 1,480 kwa mwaka na kufuatilia utatuzi wa malalamiko hayo na kushiriki kuandaa taarifa za robo mwaka na kuiwakilisha kwa wakati.
Lupimo pia ametaja majukumu ya wajumbe hao kuwa ni kufanya mikutano na vikao vya kutathmini kazi, kuwa kiungo kati ya mtumiaji, baraza na Mdhibiti, kushiriki kwenye utatuzi wa malalamiko kwa mujibu wa kanuni, uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko ya EWURA na kuhamasisha Umma kushiriki na kuchukua hatua mbalimbali katika masuala ya udhibiti .
Amesema Baraza limefanikiwa kufungua Kamati 30 kwenye mikoa 26 kwa upande wa Tanzania bara, kuwajengea uwezo wajumbe wa Baraza, watumishi na wajumbe wa Kamati za mikoa, kutengeneza vitendea kazi na kufanya mikutano ya mwaka ya watumishi inayolenga kufanya tathmini ya kiutendaji na kuweka mipango kwa mwaka unaofuata.
Licha ya mafanikio hayo Kaimu Katibu Mtendaji huyo ameeleza changamoto zilizopo kwenye Baraza hilo kuwa ni utegemezi wa chanzo kimoja cha fedha kuendesha majukumu yake na kusababisha Baraza kushindwa kufungua Ofisi za mkoa kwa baadhi ya mikoa na kushindwa kuajiri.
EWURA CCC ilianzishwa chini ya kifungu Na. 30 cha sheria ya mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji, sura ya 414 ili kutetea na kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma hizo na ilianza rasmi kufanya kazi mwaka 2007 ambapo kimuundo inaongozwa na wajumbe wa Baraza wanaoteuliwa na Waziri mwenye dhamana .