Jumuiya ya Ulaya (EU) imetoa ripoti ya waangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hapa nchini, na kutoa mapendekezo kadhaa, yakiwamo ya kuishauri Tanzania kuruhusu kuwapo wagombea binafsi.

Pia EU wanashauri mabadiliko makubwa kwenye sheria, ili kuwapa fursa wagombea na wapigakura kuhoji ushindi wa rais mahakamani. 

Ripoti hii ya EU imetoka ikiwa ni miezi miezi saba tangu kufanyika Uchaguzi Mkuu uliokipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa mgombea wake, Dk. John Magufuli.

EU wametoa ripoti yao mwishoni mwa wiki iliyopita, wakipendekeza marekebisho na maboresho katika maeneo mengi zaidi.

Akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya wanahabari, Mkuu wa Waangalizi wa Uchaguzi kutoka EU, Judith Sargentini, ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Ulaya, anasema yanahitajika maboresho mengi ya mchakato wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kupitia upya mifumo ya kisheria ya Muungano na ya Zanzibar.

Anasema maboresho yanahitajika ili kuhakiki haki za msingi za watu na makundi, kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za kimataifa na za kikanda za uchaguzi wa kidemokrasia.  

Judith anasema mapendekezo mengi yanarejea kwenye ripoti ya waangalizi wa EU katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010. 

Anasema majadiliano kuhusu utekelezaji wa mapendekezo yafikiriwe mapema iwezekanavyo, ili kufanyia kazi upungufu uliobainika kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita. 

“Haki ya kugombea kwenye uchaguzi isiwe kwa wagombea walioteuliwa na vyama pekee…hukumu ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu itekelezwe, wagombea binafsi wawe na haki ya kugombea kwenye uchaguzi wowote wa Muungano au wa Zanzibar,” anasema Judith. 

Anasema haki ya vyama vya siasa kuunda na kusajili umoja wa kiuchaguzi na kuwa na wagombea wa pamoja inapaswa kuwekwa bayana kisheria, hususani kwa uchaguzi wa Rais wa Muungano, ambako wagombea wawili wanateuliwa kwa tiketi moja kwa nafasi za rais na makamu wa rais.

Sehemu ya ripoti hiyo inapendekeza mabadiliko kwenye katiba zote mbili – ile ya Zanzibar na ya Muungano – ili ziruhusu kupingwa kwa matokeo ya rais mahakamani.

“Haki ya kulalamikia matokeo ya Uchaguzi wa Rais inapaswa kuwapo kisheria kulingana na kanuni za kimataifa za uendeshaji uchaguzi wa kidemokrasia,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, wanasema matumizi ya baadhi ya vipengele kwenye sheria hiyo vinapunguza uhuru wa kuongea na kusababisha watu kukamatwa holela. 

Anasema taratibu za matumizi zinapaswa kuwapo ili kuhakiki matumizi sahihi na yanayotabirika ya sheria hiyo. 

“Watu wanaoshitakiwa kwa makosa chini ya sheria hii wasikataliwe haki ya kujitetea mahakamani, kwani kifungu cha 38 cha sheria hiyo kinasema kuwa usikilizaji wa utetezi utakuwa ni wa upande mmoja na wa faragha,” anasema Judith. 

Ripoti hiyo, ambayo JAMHURI imepata nakala yake, inasema jitihada za dhati zinapaswa kufanywa ili kupunguza kuhusika kwa taasisi za utendaji za kiserikali katika uandaaji na utekelezaji wa mchakato wa uchaguzi. 

“Uundwaji wa muundo wa kudumu wa NEC katika ngazi ya mkoa uangaliwe, pamoja na muundo huru usio wa kudumu katika ngazi ya jimbo kipindi cha uchaguzi, hivyo kuachana na kutegemea miundo ya kiutendaji ya mitaa…uteuzi wa makamishna wa NEC uangaliwe upya ili kuongeza imani juu ya uhuru wa NEC miongoni mwa wadau wote,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.  

Ripoti hiyo pia inatoa mapendekezo kwa vyombo vya habari kwa kupendekeza vyombo vya habari vya umma – Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) – vigeuzwe kuwa vyombo vya huduma kwa umma; vipewe uhuru kamili wa uhariri na kifedha; na visiwe tegemezi kwa Serikali. 

Waangalizi hao wanapendekeza uhuru wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) uboreshwe kisheria ili kuwe na mfumo ulio wazi wa uteuzi wa bodi na mkurugenzi, usioingiliwa na chama chochote cha siasa, na unaohusisha asasi za kiraia na vyama vya waandishi wa habari.

“Vyombo vya habari vibainishe matangazo yaliyolipiwa na vyama vya siasa kwa namna inayoeleweka ili wapiga kura wajue aina ya kipindi kinachotangazwa…muda wa bure unaotolewa kwa matangazo ya wagombea ugawiwe kwa namna yenye usawa, kwa misingi ya vigezo vya uwazi na kutofungamana,” inasomeka sehemu ya mapendekezo ya EU.

Waangalizi hao wanapendekeza taasisi za usimamizi ziangalie uwezekano wa kurekebisha Kanuni ya Huduma za Utangazaji (Maudhui), Urushaji Matangazo ya Uchaguzi ya Vyama vya Siasa, na kupunguza masharti kwa vyombo binafsi.