Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
TUME ya Ushindani (FCC) imetoa wito Kwa wananchi pamoja Wakulima kuyatumia maonesho ya Nanenane kupita katika Banda lao kupata elimu itakayowasaidia kuepukana na kujishughulisha na bidhaa bandia na vitendo vingine ambavyo haviruhusiwi na Sheria ya ushindani.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa FCC, William Erio wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya maonesho hayo yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.
“Tume ya Ushindani ndicho chombo kinashughulikia masuala ya ushindani wa kibiashara, ina jukumu muhimu la kutoa ushauri kwa kampuni zinazoshindana katika soko ikiwemo kujitambulisha kwa Soko, kulijua soko vizuri pamoja na mahitaji ya wateja.
“Pia tunajukumu la kuhakikisha mfanyabiashara anatambua nafasi yake katika soko ili kuboresha bidhaa na upekee, ili kuwa na tija,” amesema.
Amefafanua kuwa, kila mfanyabiashara anapaswa kuhakikisha bidhaa zake zinakidhi viwango vya ubora vinavyotambulika na vya kisheria kwani ubora wa bidhaa unaweza kuwa kipande muhimu katika ushindani.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi na wafanyabishara kwa ujumla kuepuka bidhaa hasa zile za kuagizwa.
“Kwenye kilimo kuna suala zima la pembejeo hivyo ni wakati sahihi wa wakulima kuja na kupata elimu ya ufahamu ya pembejeo feki lakini pia kwa upande wa wavuvi wanahitaji elimu wanapataje nyavu sahihi bila kusahau vifungashio viwe venye kukidhi viwango,” amesema.
Akizungumzia kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura, Erio amewataka Wafanyabiashara na wakulima kwa ujumla kujiandikisha kwenye Daftari la Mpiga Kura ili kupata nafasi ya kuwachagua viongozi wanaowataka.
“Niwaombe wafanyabiashara mchague viongozi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko…Viongozi wenye mtandao mzuri na uhusiano na wanaweza kusaidia kufanikisha ushirikiano wa kibiashara, kupata ruzuku, na rasilimali nyingine za maendeleo.
“Viongozi wanapaswa kuwa na uwezo wa kusimamia na kuboresha huduma za kibiashara na kilimo kwa kujumuisha usimamizi wa ardhi, maji, na miundombinu ya kilimo,” amesisisitiza.