Tume ya uchaguzi nchini Uturuki imemtangaza Rais Recep Tayyip Erdogan kama mshindi wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika June 24.
Erdogan ambaye aliingia madarakani 2014 ameshinda muhula wake wa pili kwa ailimia 53 ya kura zote zilizohesabiwa akiepuka kuingia mzunguko wa pili huku chama chake kikishinda wingi wa viti bungeni.
Mpinzani wake mkuu Muharrem Ince kutoka chama cha CHP tayari amempongeza Erdogan katika mitandao ya kijamii licha ya kushutumu uchaguzi huo kuwa haukuwa wa haki.
Muda mfupi kabla ya kura halisi kutangazwa Erdogan alizungumza kupitia televishen ya taifa akisema taifa lake limepata taarifa nzuri za yeye kuendelea kusalia madarakani licha ya kwamba hazikua bado za uhakika.
”Uchaguzi wa June 24 umeleta taarifa nzuri kwa nchi yetu, kwa watu wetu. Kwa taarifa nilizonazo licha ya kuwa sio za uhakika ni kwamba nchi yetu imenichagua kuendela kuwa rais, licha ya kuwa sio za uhakika. Pia chama cha AK kimeshinda uwakilishi wa viti vingi bungeni, ambapo tuna shughuli za kisheria.” Alisema Erdogan.
Erdogan ambaye awali alihutubia mamia ya wafuasi wake mjini Ankara, kwa sasa atapata mamlaka makubwa zaidi chini ya katiba ya nchi hiyo ambayo itaanza kutumika baada ya uchaguzi.
Baadhi ya wakosoaji wanasema kuwa jambo hilo litashuhudia nguvu nyingi atakazokuwa nazo mtu mmoja, na kwamba Uturuki imeshindwa kuona namna maafisa wengine wa serikali wanavyopaswa wakitolea mfano kwa Ufaransa na Marekani.
Tume ya uchaguzi imesema Chama cha kikurdi nacho kimefanikiwa kupata asilimia 10% na hivyo kupata nafasi bungeni suala linalokipa wakati mgumu chama tawala cha Bwana Erdogan na mshirikishi wake MHP kufikia idadi kubwa bungeni, ingawa sasa wana uwezekano mkubwa wa kupata idadi kubwa.
Kulikuwa na wagombea wengine wanne katika uchaguzi wa urais, na hakuna hata mmoja ambaye anaonekana kuwa amepata ushindi mkubwa.
Pamoja na kukosolewa kwa uminywaji wa demokrasia, Erdogan anabaki kuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Uturuki huku ushindi wake ukipokelewa kwa shangwe pia katika mji mkuu wa kibiashara Istanbul.