Marais wa Rwanda na DR Kongo wamekutana Jumanne nchini Qatar na kuelezea uungaji mkono wao kwa usitishaji mapigano, ilisema taarifa ya pamoja, siku moja baada ya mazungumzo ya amani nchini Angola kuvunjika.

Umoja wa Ulaya hivi karibuni uliwawekea vikwazo makamanda watatu wa Jeshi la Rwanda, mkuu wa wakala wa madini wa Rwanda, na viongozi waandamizi wa M23, akiwemo kiongozi wake Bertrand Bisimwa, kwa kuhusika katika mgogoro wa mashariki mwa DRC.

Kwa kujibu, M23 ilidai kuwa vikwazo hivyo vinadhoofisha juhudi za mazungumzo na kuituhumu serikali ya DRC kwa ‘kampeni ya uchochezi wa vita inayozuia mazungumzo kufanyika.

Mgogoro unaoendelea mashariki mwa DRC umekuwa mbaya zaidi tangu Januari, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na maelfu wengine kukimbia makazi yao. M23, ambalo linadai kutetea maslahi ya Watutsi wa DRC, limekamata miji mikuu kama Goma na Bukavu. Kwa mujibu wa DRC, zaidi ya watu 7,000 wameuawa, ingawa idadi hiyo haijathibitishwa kwa uhuru.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imedai kuwa Rwanda inadhibiti M23 moja kwa moja, ikiwa na takriban wanajeshi 4,000 wanaounga mkono kundi hilo kwa lengo la kunufaika na rasilimali za madini katika eneo hilo, ikiwemo dhahabu na coltan.

Hata hivyo, Rwanda inakanusha kuwasaidia waasi wa M23, ikisisitiza kuwa inakabiliwa na tishio kutoka kundi la FDLR lililoanzishwa na viongozi wa Kihutu waliokuwa sehemu ya mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.

Mkutano wa Jumanne nchini Qatar ulikuwa wa kwanza wa ana kwa ana kati ya Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa DRC Felix Tshisekedi tangu M23 ilipozidisha mashambulizi yake. Ingawa mkutano huo ulielezewa kuwa wa kawaida na usiokusudiwa kuchukua nafasi ya juhudi za amani zilizopo, viongozi hao wawili walikubaliana kuendeleza mazungumzo yaliyoanzishwa Doha.