Na Prudence Karugendo
Ni jambo la kushangaza kwamba Tanganyika changa, kabla haijaungana na Zanzibar kuwa Tanzania, wananchi walikuwa waelewa wa elimu ya uraia.
Na kama alivyokuwa akisema mara kwa mara Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni kwamba jambo hilo lilisaidia kuharakisha uhuru wa Tanganyika.
Wananchi walielewa haraka nini maana ya kujitawala kutoka mikononi mwa wakoloni. Walijua umuhimu wa kuwa na Rais waliyemchagua, walielewa maana ya kuwa na mwakilishi, mbunge anayewawakilisha bungeni na kuwasemea matatizo, kero na changamoto zilizowakabili kwenye maeneo yao.
Elimu ya uraia kwa kipindi hicho ilikuwa kubwa, japo sidhani kama ilifundishwa mashuleni! Wananchi walikuwa nayo tu pengine ya ‘kuzaliwa’ nayo.
Jambo la kushangaza ni kwamba kipindi hiki ambapo elimu ya uraia inafundishwa kutoka darasa la kwanza, inaonekana kupotea kabisa, watu wakibaki wanayachukulia mambo kadiri kila mmoja anavyoona inafaa, ilimradi tu ni raia!
Katika awamu hii ya tano, ambapo Rais John Magufuli anajitahidi kuhakikisha kila mwananchi anafaidika na rasilimali za nchi, hali inaonekana kwenda kombo kwenye elimu ya uraia!
Kumbuka nchi ina zaidi ya nusu karne tangu ijitawale, tungetarajia elimu ya uraia iwe imepanda zaidi ya wakati ule wa kujitawala, lakini bahati mbaya kwa sasa inaonekana kushuka au kupotea kabisa!
Tatizo hilo nimeanza kuliona wakati wa ziara ya Rais Magufuli mkoani Kagera. Ziara iliyokuwa mahususi kwa mambo mawili makubwa – uzinduzi wa uwanja wa ndege wa mjini Bukoba na uzinduzi wa barabara ya Kyaka hadi Karagwe.
Pamoja na mambo hayo mawili, Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kupata maelezo yanayohusiana na kero za wananchi katika maeneo aliyoyatembelea.
Wakati akiwa Bukoba Mjini katika uzinduzi wa uwanja wa ndege, alisikiliza kero mbalimbali za wananchi na kutoa kauli yake.
Ninaweza kusema ‘songombingo’ ikaanzia hapo. Baadhi ya wananchi, hasa wa Bukoba Vijijini, wakaanza kulalamika kwamba mbunge wao, Jason Rweikiza, hakuzungumzia matatizo ya baadhi ya barabara zao!
Ukosefu wa elimu ya uraia ya kutosha unawafanya baadhi ya wananchi waelewe kwamba kama matatizo ya barabara yangetajwa hapo, Rais angetoa fedha palepale na kusema kwamba barabara hizo zianze kutengenezwa muda uleule!
Wanashindwa kuelewa kwamba mbunge wao anapaswa kuyasemea masuala hayo bungeni, maana kule ndiko mahala pake. Mle bungeni kuna waziri anayeshughulikia masuala ya barabara ambaye Rais kamteua kwa ajili ya kumsaidia kwa upande huo. Huyo ndiye anayebanana na wabunge kuhusu jambo hilo.
Siyo tena kazi ya Rais kupita kila eneo akisema kwamba barabara fulani ikatengenezwe namna hii au namna ile. Isipokuwa, anaitwa kuzindua inapokuwa tayari.
Jambo jingine ni kwamba Rais hatembei na bajeti ya nchi, kiasi cha kutaka kitu kifanyike na kufanyika palepale hata kama hakijawekwa kwenye bajeti ya nchi.
Mambo ya aina hiyo yanatakiwa yapitie bungeni na siyo njiani ambako Rais anakuwa anasalimiana na wananchi.
Haikatazwi Rais kusikiliza kero za aina hiyo akiwa amewatembelea wananchi katika maeneo yao, ila siyo mahala pa kumlaumu mbunge kuwa hakusema hiki wala kile. Ieleweke kuwa mbunge ni mwakilishi wa jimbo lake bungeni na siyo mitaani anakopitia Rais.
Mfano, tuliona jinsi Rais Magufuli ‘alivyowachachafya’ wakurugenzi walioshindwa kumpa majibu mwafaka, ilikuwa sahihi kabisa sababu walikuwa kwenye maeneo yao kiutendaji. Rweikiza ni mtu wa mhimili tofauti.
Nilipomwambia jambo hilo, Rweikiza akashangaa akisema kwamba waliolilalamikia ni watu wa sehemu moja, ila ukweli ni kwamba jimbo zima lina malalamiko ya aina hiyo, malalamiko ya ubovu wa miundombinu.
Barabara iliyolalamikiwa kuwa mbunge hakuisema kwa Rais ni ya Kanazi- Izimbya-Katoro. Lakini Rweikiza akazitaja barabara nyingine za Bukoba-Rubafu, Bukoba-Kanyangereko, Katerero-Kyenyabasa-Kasharu, Ibwera-Butakya na kadhalika. Akasema hizo zote ni barabara zinazohitaji kuboreshwa.
Kwa hiyo sidhani kama angezisema hizo kwa Rais zingeweza kutengenezwa palepale. Hata Rais angeweza kumshangaa kwa vile Rais, mtu aliyewahi kuwa mbunge kwa kipindi kirefu, anaelewa kuwa pale siyo mahala pa mbunge kusemea kero za jimbo lake, sehemu yake ni bungeni akiwa amezielekeza kwa waziri husika.
Jingine linalopaswa kueleweka, kama elimu ya uraia inazingatiwa ni kwamba mbunge hachaguliwi ili akatoe pesa yake mfukoni kufanyia mambo ya jimbo. Kazi yake ni kusema tu kero zilizoko jimboni mwake kunakohusika ili pesa ya walipakodi ikatumike kutatua kero hizo.
Kama nilivyosema wakati fulani, Rweikiza siyo mtu wa maneno mengi, yeye ni mtu wa kutenda. Anaweza akasema maneno mawili akatenda kumi, tofauti na mtu anayeweza kusema maneno mia asitende hata moja! Wapo wengi wa aina hiyo tunawaona.
Ndiyo maana, kutokana na Serikali kutokuwa na uwezo wa kutimiza kila linalotakiwa katika kila jimbo, Rweikiza anatumia juhudi binafsi kuonesha yale ambayo yangepaswa kufanywa na pesa za walipakodi. Na yanakidhi haja sawa na yale yaliyofanywa kwa kutumia pesa ya walipakodi, wananchi wanafurahi.
Lengo la makala hii ni kuwataka wananchi wawe kwenye mwelekeo wa elimu ya uraia, wasiwe watu wa kulalamikia vitu ambavyo haviendani na malalamiko yao.
Walalamike wakielewa kwamba wanachokilalamikia kipo kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, elimu ya uraia inatakiwa ifanye kazi ipasavyo.