Hotuba ya Baba wa Taifa aliyoitoa March, 1967

Twajaribu Kujenga Taifa la Namna Gani?

Maana yake neno hili ni kwamba mipango ya elimu katika Tanzania haina budi kutilia mkazo juhudi ya pamoja siyo maendeleo ya mtu mmoja binafsi.

Elimu haina budi kutiliwa mkazo mawazo ya usawa, na wajibu wa kuwahudumia wengine wakati mtu anao uwezo zaidi, kama ziada hiyo ni useremala, ufugaji, au hata elimu, na hasa, mipango yetu lazima ipinge majivuno ya elimu yanayowafanya wale waliosoma zaidi wawadharau wale walio na uwezo usiohitaji kusoma, au ambao hawana uwezo maalum, lakini ni binadamu. Majivuno ya namna hiyo hayana nafasi katika nchi yenye wananchi sawa.

Lakini mipango ya elimu yetu isiwe ya kufikiria usawa tu. Lazima vile vile iwekwe mipango ya kuwaandaa vijana wetu kwa kazi watakayotakiwa kufanya katika jamii ya Kitanzania; huko vijijini ambako maendeleo yatategemea sana kazi na juhudi za wakulima.

Kusema hivi hatuna maana kwamba elimu ya Tanzania ipangwe katika namna ya kufunza wakulima wa aina mbali mbali wasiojua kufikiri, wanaofuata tu kama kondoo mipango na amri zote zinazotolewa na wakubwa.

Lazima elimu hiyo izae wakulima bora, na vile vile iwaandae watu kushika madaraka wanayostahili, wakiwa wafanyakazi, wananchi huru, katika nchi huru ya kidemokrasia, ingawa ni ya wakulima.

Hawana budi waweze kufikiri na kujiamilia mambo yote yanayohusu maisha yao; hawana budi waweze kuelewa uamuzi uliofanywa kidemokrasia katika vikao vinavyojulikana vya nchi yetu, na kutimiza uamuazi huo kwa kufuatana na mazingira ya mahali wanapoishi.

Kwa hiyo, kufikiria kwamba mipango yetu ya elimu iwe ya aina ya kufundisha madubwana tu, yanayofanya kazi kwa bidii bila kuuliza viongozi wa TANU na Serikali wanasema au kufanya nini, ni kutokuelewa haja yetu.

Maana watu ndiyo TANU na Serikali; lazima iwe hivyo. Serikali yetu, na chama chetu, lazima wakati wote viwe na wajibu kwa watu,na lazima wakati wote viwe na wajumbe walio watetezi na watumishi wa watu.

Kwa hiyo elimu tunayotoa haina budi ihimize kila raia mambo matatu. Kwanza udadisi. Pili uwezo wa kujifunza kutokana na mambo ya watu wengine, na kukubali au kuyakataa mambo hayo kwa kupima haja zake mwenyewe. Na tatu, imani katika nafsi yake mwenyewe kwamba yeye ni raia katika jamaa hiyo aliye sawa na mwingine yeyote, anayeheshimu wengine kama yeye mwenyewe anavyoheshimika, kutokana na kazi anazozifanya, wala si mapato apatayo.

Mambo haya ni muhimu kwa upande wa mafunzo ya kazi na pia kazi katika maadili ya maisha. Hata kijana akijifunza utaalamu wa kulima namna gani, hatapata kitabu kitakachompa majibu ya matatizo yote atakayoyakuta katika shamba lake mwenyewe.

Itabidi ajifunze maarifa ya ukulima wa kisasa lakini halafu ujuzi huo katika shamba, akitaka kuyafumbua matatizo yake. Kadhalika, wananchi huru wa Tanzania watapaswa wajiamulie wenyewe mambo yoteyanayohusu maisha yao.

Hakuna msahafu wasiasa, wala hautashuka msahafu, utakaotoa majawadu ya matatizo yote ya siasa ya uchumi yatakayotokea katika nchi hii katika siku za mbele. Yatakuwako mawazo na mipango itakayokubaliwa na nchi yet, ambayo wananchi watafikiria na kutimiza kutokana na fikara zao na ujuzi wao wenyewe.

Lakini mipango ya elimu katika Tanzania haitifaidia nchi ya ujamaa ya kidemokrasia kama mipango hiyo itakuwa inawafanya watu wasithamini mafunzo, mipango na imani za viongozi wao, ama wa kale, ama wa sasa. Wanaoweza kujenga taifa huru ni watu huru wanaotambua utu na usawa wao.

Mipango ya Elimu ya Sasa

Shabaha yake mipango hiyo ni tofauti sana na shabaha tunayoilenga katika mipango yetu ya sasa. Maana kuna mambo manne makubwa katika mpango wetu wa sasa ambayo yanazuia au hayashawishi kukubalika kwa wanafunzi katika vijiji watakamoishi, na ambayo yanafunza fikara za ubwana, majivuno ya elimu na kujiona binafsi kwa vijana watakaopita katika shule zetu.

Jambo la kwanza kuhusu elimu tunayoitoa sasa ni kwamba elimu hii ni ya kibwana iliyopangwa kuwafaidia idadi ndogo sana ya watoto wanaoingia shule.

Ingawa vijana wetu watakaopata nafasi ya kuingia katika shule za sekondari ni 13 kwa mia tu ya wale wanaokwenda shule za msingi, lakini hata hivyo mpango wa shule zetu za msingi ni wa kuwatayarisha watoto wetu kuingia katika shule za sekondari.

Kwa hiyo 87 kwa mia ya watoto wetu waliomaliza shule mwaka uliopita na wengine kama hao watakaomaliza mwaka huu, wanaondoka shuleni wakifikiri kwamba wameshindwa, na kukoseshwa matumaini yaliyokuwa haki yao.

Na kwa kweli, wote sisi tunasema vivyo hivyo, tunawaita vijana hawa kama ‘wale walioshindwa kuingia sekondari’, badala ya kuwaita ‘vijana waliomaliza elimu ya msingi’. Na kwa upande mwingine, wale 13 kwa mia wanaendelea kuwa na fikara ya kustahili tuzo, na tuzo wanalolitumaini wao na wazazi wao ni mishahara mikubwa, kazi za raha mijini na jina kubwa mitaani. Na hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaopanda ngazi ya juu zaidi, wakati wanapoingia Chuo Kikuu.

Ndiyo kusema kwamba elimu inayotolewa sasa ni kwa ajili ya wachache tu wenye uwezo wa mitihani kuwazidi wengine; inawafanya wale wanaofanikiwa wajione kuwa wakubwa, na kuwafanya walio wengi wakitamani kitu ambacho hawatakipata daima.

Inawafanya walio wengi wajifikirie kuwa wanyonge na kwa hiyo hawawezi kuunda wala taifa la usawa tunalotaka kulijenga wala fikara zinazoelekea kwenye taifa lenye usawa. Kinyume chake, elimu hiyo inashawishi kuundwa kwa taifa lenye tabaka. La ubwana na utwana, katika nchi yetu.

Jambo la pili ni muhimu vile vile, nalo ni kwamba elimu ya Tanzania inawatenga wale wanaosomambali na wananchi wanaowasomesha. Hii ni kweli hasa kwa shule za sekondari ambazo karibu zote ni za wanafunzi kukaa huko shuleni. Lakini ni kweli vile vile hata katika shule chache za praimari, ijapokuwa hivi karibuni tumebadili kidogo mipango yetu.

Tunawachukua watoto wakiwa na umri wa miaka 7 kutoka kwa wazazi wao, na tunawafunza masomo ya darasani saa 7½ nzima kutwa. Katika miaka michache iliyopita tumejaribu kuyafanya mafunzo haya yafanane na hali ambayo watoto wanaiona.

Lakini shule yenyewe kila mara iko mbali, siyo karibu na jamaa au kijiji. Shule ni mahali ambapo watoto huenda kwa matumaini, yao na wazizi wao, kwamba wakifanikiwa haitakuwa lazima kwao kuwa walikuma au kuishi vijijini.

Wale wachache wanaoingia shule za sekondari hupelekwa mbali na makwao, wanaishi maisha ya pekee, wakiwa na ruhusa ya kwenda mjini kujistarehesha, lakini kazi za mji au kijiji kile hazilingani na maisha yao hasa, yaani maisha wanayoishi wakawa uwanja wa shule.

Baadaye wachache huenda Chuo Kikuu. Wakiwa na bahati kuingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanaishi katika nyumba za raha, wanalishwa vizuri na kusoma sana kupata digrii zao. Watakaopata digrii hiyo wanajua mara moja kwamba watapokea mshahara kiasi cha shilingi 1,100/- kwa mwezi.Hiyo ndiyo shabaha waliyokuwa nayo, ndiyo waliyofunzwa wawe nayo.

Wanaweza vile vile kuwa na haja ya kuuhudumia umma, lakini fikara zao za huduma zinatokana na heshima na mshahara ambao mtu aliyehitimu Chuo Kikuu anaweza kuupata. Mshahara wa hadhi vimekuwa haki inayotolewa na Digrii.