Hadi kesho katika taifa letu la Tanzania bado hatujakubaliana ni lugha gani tutumie katika kufundishia. Wengine wanapendekeza lugha ya kigeni, Kiingereza; na wengine wanaipendekeza lugha yetu ya Kiswahili. Hii ni kasoro kubwa! Wataalamu wa falsafa wanatuambia kwamba, fikra na mawazo ya mtu au jamii yamo katika lugha yake.
Kwa hiyo kukomaa kwa fikra za mtu huenda sambamba na kukomaa kwa lugha yake, kwa hiyo kama wazo haliko wazi kwake, haliwezi kupata lugha iliyokuwa wazi. Kama mtu ana fikra za kisayansi, basi atakuwa na lugha ya kisayansi na kama ana fikra za kifalsafa, basi atakuwa na lugha ya kifalsafa.
Na kama fikra zake zitakomaa na hapana lugha ya kukamata fikra hizo katika sura ya wazi ya umbo, basi itabidi atafute maneno ya kukamata fikra hizo. Kwa hiyo kukomaa kwa fikra ni sharti muhimu la kukomaa kwa lugha. Na kama kuna neno jipya linaingizwa ndani ya fikra ambazo bado hazijakomaa ili kuweza kulimeza lile neno katika asili ya fikra yake, kinachotokea ni kuchanganyikiwa au kuelewa nusu nusu (Dk. Adolf Mihanjo, Falsafa na Usanifu wa Hoja Uk. 99).
Kwa hiyo kupanuka kwa mawazo ni kitu cha kwanza na lugha ni kitu cha pili. Kama huu ni ukweli, ni lazima tukubaliane kwamba huwezi kupanua mawazo kwa kutumia lugha ya kigeni! Hii haina maana ya kupinga lugha za kigeni, wala si lengo langu kuiweka Tanzania nje ya utandawazi. Hoja ni kwamba mtu ambaye amepanuka mawazo, ambaye fikra zake ni pevu anaweza kufanya uamuzi wa kujifunza lugha zozote zile kwa kuzingatia zina manufaa gani kwake na kwa jamii yake.
Jambo la muhimu ni kujenga msingi. Ukishajenga msingi, kuta zinaweza kusimama jinsi utakavyo. Mtu aliyepanuka mawazo, atahoji ni kwa nini ajifunze lugha za kigeni. Ni kutaka kupata nini? Lugha ngeni itamletea faida gani yeye na jamii inayomzunguka?
Anaweza kuweka nguvu zake zote kujifunza Kiganda, kama lugha hii ni muhimu kuendesha maisha ya siku kwa siku kwake yeye na jamii inayomzunguka, anaweza kuamua kujifunza Kiingereza kama lugha hii ni muhimu kuendesha maisha yake ya siku kwa siku kwake na jamii inayomzunguka. Dunia hii ina lugha nyingi kiasi mtu haziwezi zote, bali ni kufuata kipaumbele. Yote haya yanawezekana mtu akipata elimu isiyokuwa na kasoro kubwa.
Watanzania walio wengi bado wanataka tutumie Kiingereza katika kufundisha. Sababu kubwa ni kwa vile tulitawaliwa na Waingereza. Kama tungetawaliwa na Wafaransa, tungekuwa tunashikilia kufundisha kwa Kifaransa. Kama tugetawaliwa na Wareno, tungekuwa tunashikilia kufundisha Kireno. Hatushikilii Kiingereza kwa vile ni lugha nzuri au kwa vile ni lugha ambayo tunaifahamu vizuri. Tunafanya hivyo kutokana na historia ya ukoloni iliyoathiri akili zetu na roho zetu. Na matokeo yake ni kwamba maarifa yanabaki mikononi mwa kundi dogo la “Wasomi”.
Historia ya kukua na kupanuka kwa mawazo Ulaya inatuonyesha wazi kuwa, ni pale tu ambapo falsafa iliandikwa na kuwasilishwa katika lugha enyeji au lugha zao ndipo mapinduzi makubwa ya kijamii yalianza kuchukua kasi ya ajabu. Kipindi cha uvuvumko (Renaissance) kilitokana na hali ya nchi za Ulaya kutumia lugha zao katika kutafuta maarifa. Katika kipindi cha uvuvumko maarifa yalimilikiwa na wananchi na siyo tena kikundi cha wachache. Hii ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya maendeleo ya kifikra barani Ulaya. Wanafalsafa Locke na Hume, waliiandika falsfa kwa lugha ya Kiingereza na kuleta mapinduzi makubwa ya kifikra nchini Uingereza.
Wanafalsafa Voltaire na Rousseau, waliiandika falsafa kwa lugha ya Kifaransa na kuleta mapinduzi makubwa ya kifikra nchini Ufaransa. Na kule Ujerumani, mwanafalsafa Kanti, aliiandika falsafa kwa lugha ya Kijerumani, na kuibua maendeleo makubwa ya kifikra nchini ujerumani.
Ukweli huu wa kipindi cha uvuvumko kule Ulaya unaacha akili zetu kwenye dimbwi kubwa la fikra iwapo kama matumizi ya Kiingereza katika mitaala yetu ya elimu itatuwezesha sisi kumiliki maarifa na kusonga mbele.
Martin Luther, alipojitenga na Kanisa Katoliki, alipata waumini wa kumfuata na kuweza kuanzisha kanisa lake la Lutheran, kwa vile alifanya kazi kubwa ya kuitafsiri Biblia na kuiingiza kwenye lugha ya Kijerumani. Ujumbe wa Biblia, ulioonekana kuwa ni fumbo kwa miaka mingi na kumilikiwa na mapadri na maaskofu, sasa ulimilikiwa na waumini wote. Hatua hii ilileta mapinduzi makubwa katika imani na kujenga upevu na ukomavu wa imani katika nchi za Ulaya. Hivi leo kuna Biblia ya Kiswahili kutokana na kazi kubwa ya Martin Luther.
Ngugi wa Thiong’o, aliandika vitabu vingi kwa lugha ya Kiingereza bila kuona matokeo ya mchango wake katika jamii. Pale alipoamua kuandika kwa lugha yake ya Kikuyu, ndipo alipoona mchango wake. Watu walianza kuipinga serikali iliyoukumbatia ukoloni mambo leo. Walianza kudai haki kwa nguvu zote, kitabu chake “Nitaoa Nikipenda” kilipigwa marufuku nchini Kenya na Ngugi aliwekwa kizuizini.
Lugha inayoeleweka kwa watu wote ikitumiwa inasaidia kujenga fikra. Lugha hii ndiyo inaweza kujenga falsafa ya nchi husika. Falsafa inayojenga ukomavu wa fikra na mawazo ndiyo imeleta maendeleo Ulaya, Amerika na Asia. Ni vigumu kuunda falsafa kwa kutumia lugha ya kigeni. Haijatokea popote duniani, hivyo ni ndoto kutokea Tanzania. Ulaya na Asia waliamua kutumia lugha zao katika kuwasilisha maarifa ambayo yanaunda akili. Sisi hapa Tanzania tunashindwa kuibua fikra mpya, tunabaki kunukuu vya wengine, tumekubali kupatiwa silaha ya kufikiri ni lazima tutabaki mateka wa wale wanaofikiri, tumekuwa mateka wa kisaikolojia wa lugha na fikra za kigeni, mathalani Kiingereza na tunaendelea kuibua hoja za kuhalalisha umateka huo.
Tukirudi nyuma na kuangalia watu wa Mashariki ya Mbali, hawa watu katika historia ya kukua kwa mawazo, walisaidiwa sana na epistemolojia (Falsafa inayohusu elimu ya mawazo au inayotoa uchambuzi juu ya chanzo cha mawazo) na walitumia lugha zao! Shenkara kule India, falsafa ya Hinduism, falsafa ya Confucius kule China, falsafa ya Taoism na falsafa ya Budhism kule Thailand. Hizi falsafa kama zile za Wagiriki zilitengeneza mazingira mazuri ya fikra.
Elimu yetu itakayoongozwa na lugha yetu ili kukomaza fikra ndiyo silaha ya pekee, hii itatufanya kuwa na uelewa wa kina wa kuoanisha uamuzi mbalimbali wa kijamii, na mijengeko yake ya kifalsafa. Uoanishaji huu utatoa uwezo wa kuambatanisha mijengeko ya falsafa hiyo, utaarifu wake, uhalisia wa mazingira na falsafa yetu. Hii itatufanya sisi tuepe kuwa watu wa kuiga tu mambo na kufanyiwa majaribio ya mifumo ya kifikra inayoibuka huko Ulaya siku hadi siku. Aidha, itatuwezesha kuibuka na ung’amuzi wenye usanisi mpya wa kifikra unaoakisi dunia katika mazingira ya Mtanzania.