“Kutengana na umaskini ni hali iliyo njema sana; na uchache wa afya kuwa katika mwili ni mashaka ambayo hayana mfano. Ubora wa ukubwa na rafiki katika Mahakama haulingani na kitu kingine chochote, na hata hushinda fedha iliyomo mfukoni ambayo haiwezi kutenda neno; na laiti machukiano yasingekuwako sisi sote tusingalikwenda katika Pepo.
“Nafsi zetu zina uchache wa amani kwa sababu ya uadui na ugomvi kama watu ambao hatuna matumaini, furaha na masikilizano. Tuna chembe ndogo tu ya imani katika ushenzi na ukaidi. Utukufu wetu hauna thamani kwa ukosefu wa maridhiano. Katika hali ya utu, ubora wetu ni kuwa na mapatano, na leo pamekuwaje na nuksani!”
Nimenukuu aya hizo mbili kutoka kitabu Kielezo cha Fasili, kilichotungwa na kuandikwa na mwandishi maarufu na gwiji wa fasihi, mashairi na lugha ya Kiswahili kushinda wote katika jamii za Waswahili kote Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Shaaban Robert.
Msomaji, nakuomba usome aya mbili hizo za utangulizi kwa utulivu ili utambue mwandishi anazungumzia nini kuhusu ubora wetu katika jamii, na ni sababu zipi zilizonikoleza kunukuu na kuelezea hali ilivyo leo ndani ya jamii yetu Watanzania. Ubora wetu naunganisha na elimu yetu.
Neno elimu limetawala mno ndani ya bongo, nafsi na vinywa vyetu, ndiyo maana tunaimba na kulia kila siku tunahitaji tupate elimu bora. Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya TATAKI, toleo la 3, mwaka 2013 inasema, ‘Elimu ni mfumo wa mafunzo yanayopatikana shuleni, vyuoni, maishani, n.k. taaluma.’
Tuna elimu katika mafunzo mbalimbali, mathalani elimu maadili, elimu magonjwa, elimu siha na kadhalika. Leo nakusudia kwa uchache kuzungumzia elimu na ubora wetu, hasa elimumaisha ambayo inakwenda pamoja na elimumaadili. Yumkini Watanzania leo tunasumbuliwa mno na elimu mbili hizo.
Naamini Watanzania kabla ya ukoloni, makabila mbalimbali yalikuwa na mfumo wao wa kuwafundisha watoto, vijana na watu wazima namna ya kuishi na kukabiliana na mazingira yanayowazunguuka. Elimu hiyo ilihusu mila na desturi, kilimo, ufundi, ufugaji, uvuvi, ujasiri, ukakamavu n.k.
Wakoloni (Waarabu, Wajerumani na Waingereza) walipoingia nchini na kututawala kimabavu, waliondoa elimu yetu na kuweka elimu yao iliyohusu mahitaji yao katika maeneo ya mijini na mashambani wakiwa na lengo la kupata wafanyakazi (makarani na wanyapara) wa kuendesha na kusimamia shughuli zao. Elimumaisha na elimumaadili hazikutolewa, waliachiwa wenyeji wenyewe.
Baada ya nchi (Tanganyika na Zanzibar) kupata uhuru, mkazo uliwekwa katika elimu za shuleni na vyuoni kwa lengo la kupata wasomi na wataalamu katika elimu, uchumi, kilimo, ufundi, sheria, utabibu n.k. Mafunzo ya elimumaisha na elimumaadili hayakupewa msukumo stahili. Imeonekana kama ni elimu za kutolewa kiziada-ziada tu kwa watakao.
Ukweli tumeweka msingi mbovu. Leo tunasikia kauli za vitisho, dharau, uchochezi zinazotolewa na baadhi ya viongozi wasomi nchini na kuambukizwa vijana vyuoni na kwenye vyama vya siasa ambao nao wanavumisha kauli hizo bila kwanza kuweka hadhari na kuangalia hatimaye itakuwa nini pindi nchi iingiapo kwenye machafuko. Cha ajabu na kushangaza hata baadhi ya wananchi wenyewe wanaunga mkono kauli hizo kwa chereko.
Wanafikiri na kuwaza kwamba kwa kauli hizo ndiyo njia njema za kututenganisha na umaskini tulionao. Bado hawajamaizi kwamba kauli chafu za uhasama, miyongo na uchochezi zinajenga uadui na magombano na kuvunja amani ambayo itatutenga na umaskini katika kufanya kazi baada ya kupata elimumaisha na elimumaadili.
Ubora wetu unategemea sana elimu mbili hizo wala si kauli za ufitini na uchochezi mbele yetu na mbele ya marafiki zao wa ndani na nje ya nchi, kuendeleza utukufu wao na wetu katika kulinda thamani ya utu na maisha yetu. Msimamo huo si wa kweli hata chembe bali ni kete takatifu ya kuweka nuksani. Hasara iliyoje Watanzania!
Mambo hayo yanatokea kwa vile viongozi hao wanaamini wao ndiyo wenye utukufu, uwezo na huruma, si kweli. Angalia, hivi sasa wanavyodhulumu haki za wenzao kushiriki katika vyombo vya uamuzi, vyombo vya sheria na vyombo vya haki. Tazama wanavyofitini wananchi wasipate huduma na misaada ya kimataifa.
Mtanzania mwenzangu, kumbuka Sheikh Shaaban Robert ametuasa kwa kutueleza kwamba, “Utukufu wetu, (Watanzania) hauna thamani kwa ukosefu wa maridhiano. Katika hali ya utu, ubora wetu ni kuwa na mapatano, na leo pamekuwa na nuksani!”
Ndugu yangu, pamoja na kuweka elimu ya shuleni na chuoni kupata wasomi wengi haitoshi. Lazima tuweke mkazo kuwashawishi na kuwaelekeza wasomi na wananchi kuwapa vijana elimumaisha na elimumaadili, kunusuru Taifa.
Uongozi ni dhima. Uongozi ni maridhiano; na hapo ndipo ubora wetu unapokuwa ni mapatano. Ni wajibu wetu kukomesha kauli chafu na kutamka kauli msumeno. Lazima tuzuie nuksani kwa kutoa elimu yenye manufaa kwetu. Taasisi za elimu, dini na jumuiya mbalimbali kufufua elimumaadili na elimumaisha ili watu watambue chembe ya amani, madaraka na mamlaka, thamani na ubora wa dola ya nchi.