Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dodoma
Mpango wa matumizi bora ya ardhi vijijini ulirasimishwa miaka ya hivi karibuni ikiwa ni moja ya mikakati katika mchakato wa kuleta maendeleo endelevu.
Utekelezaji wa mpango huu hauna budi kuwa mikononi mwa wanavijiji wenyewe kwa kiasi kikubwa katika kugawa ardhi yao kwa matumizi mbalimbali ya kujikimu kimaisha kwa sasa na siku za baadaye na kuwa na uhifadhi endelevu wa mazingira.
Mpango wa matumizi bora ya ardhi vijijini unasaidia kusimamia na utatuzi wa migogoro ya matumizi
ya ardhi, maji na uhifadhi wa mazingira.
Joseph Mafuru ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Matumizi ya Ardhi, Joseph Mafuru amesema kuwa ushirikishwaji wa wadau ni muhimu katika kuyalinda mazingira na kutekeleza kwa urahisi mipango ya matumizi ya ardhi nchini.
Akizungumza na waandishi waliotembelea Ofisi za Tume ya Matumizi ya Ardhi mjini Dododma hivi karibuni kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), katika mradi wa Tuhifadhi Maliasili chini ya ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), amesema kuwa katika suala uhifadhi linapaswa kushirikisha sekta biafsi, wananchi, taasisi za wanyamapori na wengineo katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kisha kusimamia kwa pamoja ili kurahisha utekelezaji.
“Ili uweze kuwashirkisha wadau kama JET, inafaa kuanza kuandaa mipango ya ardhi kwa pamoja na kisha ikasimamiwa kwa pamoja na utekelezaji wake unakuwa rahisi sana.
“Usipowashirikisha wadau utekelezaji wake utakuwa mgumu sana, kwa hivyo kuna haja ya wadau wote kushiriki kwa pamoja kuhakikisha zoezi hilo linafanyika na kufanikiwa,” amesema .
Mafuru amesema kuwa kama Tume ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanapambana kupata wadau wa kutosha ili kuhakikisha wanaongeza kasi ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi. Vijiji vilivyoandaliwa mipango kwa sasa ni vichache sana ambapo ni vijiji 3000 tu kati ya vijiji 13,000 na hii maana yake bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
“Tukiongozwa na Serikali ikifuatiwa na wadau wengine kwenye masuala ya uhifadhi mazingira na wanyamapori, tunapaswa tuhakikishe tunatengeneza mipango ya kutosha. Kwani kadri tunavyozidi kuchelewa kutengeneza maana yake tunaendelea kutengeneza migogoro kati ya wanyamapori na binadamu, hivyo ni heri tukaifanya mapema hiyo mipango ili kuepusha migogoro hiyo,” amesema.
Amesema kuwa kama Tume wameweka kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha unaoendelea wa 2024-2025, ambapo wametenga bilioni tano na zaidi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kazi hizo zinafanyika kwa ufasaha zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Uzingatiaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi , Joseph Paul amesema, mipango ya matumizi ya ardhi imesaidia wanakijiji kutokuingia maeneo ya hifadhi lakini pia imesaidia kuongoa mapito ya wanyama na kuwafanya wapite kama ambavyo wanapaswa kupita.
“Kimsingi tunafahamu wanyama kama tembo huwa hawasahau njia zao, kwa kupitia Serikali za vijiji lakini pia wazee ambao wana uzoefu na maeneo hayo wamesaidia kuainisha maeneo ambayo yana umuhimu wa uhifadhi kuyatenga kwa matumizi rafiki ambayo hayatazuia wanyama kupita lakini shughuli za kibinadamu kuendelea,” alisema Paul
Paul amesisitiza kuwa mfano wa hilo ni upande wa Kaskazini ambapo mpango wa matumizi ya ardhi umesaidia katika kupanga matumizi nyanda za malisho kwa jamii ya kule.
Alisema kimsingi Tume ya Taifa ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi imeratibu na kusaidia uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi katika ngazi ya kanda, mkoa, kwa mfano ukanda ambao ni muhimu kwa uhifadhi kama mkoa wa Mara, mpango umeendelea kuandaliwa ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi sahihi ya ardhi.
“Lakini pia tumegundua kwenye tafiti zetu kwamba ili tusaidie kusiwe na muingiliano wa kimatumizi kuna umuhimu wakuboresha maisha ya wananchi wenye maeneo yao. Moja ya njia za kuboresha ni kuhakikisha kwamba wana uhakika wa umiliki wa ardhi, kwahivyo tume imewezesha uandaaji hati miliki za kimila zaidi ya 20,000 kwa maeneo yenye umuhimu wa uhifadhi.
“Wanakijiji wa maeneo hayo wamepewa hati miliki za kimila kwa kuzingatia vigezo mbalimbali pamoja na kuhakikisha kuwa jinsia katika umiliki inazingatiwa, kwenye familia tumehakikisha mume na mke wanamilikishwa yale maeneo yao pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa ndani na nje ili kusaidia wananchi kutumia maeneo yao vizuri kwa kilimo na ufugaji wenye tija,” amesema.
Pamoja na hilo, Paul amesema kuwa ukosefu wa elimu ya matumizi bora ya ardhi bado ni changamoto kwa wanajamii, hivyo bado wanaendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa utunzaji na umuhimu wa utekelezaji mpango wa matumizi ya ardhi.
Kwa upande wake Ofisa Mkuu wa Ardhi wa Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Nyirembe Munasa amesema ili kuwe na maendeleo endelevu wanapendekeza kuwe na mipango ya matumizi ya ardhi katika mikoa yote nchi nzima, na kanda zilizopo mfano ikolojia ya ziwa Victoria, Tanganyika, Serengeti na kwingineko, inahitajika kuhifadhi maeneo ya ikolojia kwa kuzingatia matumizi ya ardhi katika ngazi za mikoa.
“Kuna umuhimu mkubwa sana kulinda mifumo ya ikolojia, lakini nchi yetu ina mifumo mingi ya ikolojia ambayo hailindwi hasa hizi shoroba ambazo wanyama hutumia kutoka kwenye hifadhi moja kwenda nyingine. Kwa bahati mbaya sana unakuta miongoni mwa hizi shoroba nyingi sana zimezibwa kwa aidha shughuli za kilomo au makazi ya binadamu jambo linalosababisha migongano kati ya wanyama na binadamu.
“Hakukuwa na mikakati au mipango ambayo ilikuwa inaelekeza namna gani hayo maeneo yahifadhiwe. Lazima tufanye uongoaji wa hizi shoroba kwa kutumia mipango shirikishi ya matumizi ya ardhi, kuwe na maendeleo endelevu sababu yana umuhimu wake kuchumi, kijamii na pia katika mambo ya mazingira na kiikolojia,” amesema Munasa.
Ameongeza, “Kuhusu shoroba ziko 66 lakini ni mbili tu ndizo zimefanyiwa kazi ikiwemo shoroba ya Ifakara. Changamoto kubwa iliyokwamisha zoezi hili ni fedha na hii ni kwasababu shoroba ziko nyingi na tunahitaji kuwa na mipango ya matumizi katika vijiji vyote vinavyopitiwa na shoroba,”.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Uzingatiaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Rehema Kishoa ameongeza kuwa kama hakuna usimamizi mzuri hizo shoroba hazitakuwepo, mipango itapangwa lakini hazitakuwepo, kwahiyo ni vyema kuangalia namna yakuwashirikisha wananchi wakati mipango inaandaliwa kwasababu wao ndio wahusika wakuu katika suala zima la kuwepo ama kutokuwepo kwa shoroba hizo.
“Tume ina wajibu wa kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi inayoandaliwa kwa ngazi zote inasimamiwa kama ilivyopangwa. Muhimu kwa wanajamii, watalaamu na wadau wengineo kushirikiana juu ya masuala ya ardhi,” amesema Kishoa.
Naye Mkurugenzi wa JET, John Chikomo aesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa na shughuli za binadamu yanasababisha usumbufu wa hatari na ulioenea katika mazingira yetu na kuathiri maisha ya mabilioni ya watu ulimwenguni, licha ya juhudi zinazofanyika kupunguza hatari hiyo.
Amesema kuwa katika mapambano dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabia nchi elimu ya mazingira na haswa uhifadhi bado inahitaji ipelekwe kwenye jamii lakini pia kusisitiza uwepo wa ushirikishwaji sekta binafsi na wizara katika masuala ya mazingira.
“Ikiwa wadau muhimu kama vile Wizara ya Maliasili na Utalii, watunga sera, waandishi wa habari na wengineo watashirikiana kwa pamoja katika maandalizi ya sera, mipango na michakato ya usimamizi wa mazingira itasaidia kulinda, kuhifadhi, kutunza na kusimamia mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadae,” amesema Chikomo.
Chikomo amesema kuwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kuwezesha uandaaji wa Mipango itakayoweka mikakati mizuri ya kutumia fursa mbalimbali zilizopo ili kupiga hatua ya kimaendeleo kwenye nyanja za kiuchumi na kijamii.