Serikali ya hapa Uingereza inaandaa mabadiliko makubwa ya elimu amabko mfumo wa mitihani utakuwa tofauti. Lazima nasi Watanzania tujifunze kitu hapa kwa sababu tumekuwa na kasumba ya kubadili mfumo bila sababu zake kueleweka wazi.
Nakumbuka jinsi Serikali ya awamu iliyopita ilivyobadili mambo, ikienda tofauti na zilizotangulia. Moja ya mambo yaliyoondoshwa ilikuwa michezo. Hapa Uingereza michezo inapewa kipaumbele na hata mwanafunzi akionesha yuko safi huko, anaweza kuacha shule akishamaliza msingi wake na kuingia academy kukuza kipaji chake.
Mabadiliko haya yanakuja baada ya mfumo wa uchumi wa dunia kubadilika na Uingereza yenyewe kuwa tofauti na ile ya zamani, wakati maisha yalikwenda tu kama utelezi. Hapa sasa watu wanahenya kupata mkate wao wa kila siku. Mzungu sasa anaingia kupiga kila aina ya kazi, ilimradi mwisho wa mwezi pesa iingie benki apate mahitaji yake na wanaomtegemea.
Wenzetu hawa wanafanya mambo yao kwa utaratibu na hatua kwa hatua, maana mara ya mwisho kubadilisha mfumo ilikuwa miaka ya 1980.
Hivi sasa wametazama wakachakata na kuridhika kwamba matunda yake hayaendani na kizazi cha sasa na kijacho, hivyo wabadilishe. Elimu mpya itakayoanza rasmi mwaka 2015 na mitihani yake kufuata mwaka 2017, itahakikisha wanafunzi wachanga wanaandaliwa kwa ajili ya dunia ya kazi mbalimbali za kujiajiri na kuajiriwa.
Mpango uliowekwa ni kutoa elimu pana inayohusisha kwa undani stadi za kazi, utamaduni na michezo. Imesisitizwa wanafunzi waendelee kujifunza hisabati na Kiingereza hadi wafikie umri wa miaka 18. Kwa taarifa tu ni kwamba kuna wanafunzi wamekuwa wakihitimu elimu ya msingi lakini hawajui kusoma wala kuandika, achilia mbali hizo hesabu.
Yaani ukweli wa wazi ni kwamba kuna watoto wanakizungumza Kiingereza cha “slang” lakini hakina hata mpangilio kisarufi, hivyo akija kupata kazi hata ya umakenika au kiwandani, inakuwa tabu. Unaona jinsi hatua hizi zinavyochukuliwa taratibu? Si waziri mmoja anasimama tu kwenye idara, wizara au bungeni na kutangaza kubadilisha mitaala na kufuta michezo shuleni.
Wanatangaza wiki hii, nadhani Jumanne hii, lakini watendaji watachakata, uchaguzi mkuu utapita mwaka 2015 ndipo kazi ianze, bila kujali chama gani kitakuwa kimeshinda. Kwa hiyo, kuanzia wakati huo kutakuwa na mbadala wa ile mitihani iliyozoeleka sana kama GCSE katika England naWales.
Kigezo kipya cha kufaulu kitajumuisha mtihani mmoja tu wa kuvuka katika kila somo, badala ya moduli na tathmini ya hatua kwa hatua kwa utendaji wa mwanafunzi. GCSE ilianza miaka ya 1980 kuchukua nafasi ya mfumo wa mitihani ya ‘O-Level’ na ‘CSE’, wakati mtihani wa kwanza wa GCSE ulifanyika mwaka 1988.
Hali hii ya mabadiliko itakwenda sambamba na ya Ujerumani inayoandaa watoto kwa kazi nzito za kujitegemea. Wao muda mwingi mtoto huwa ama kwenye familia au viwandani kufanya elimu kwa vitendo. Muda wa darasani ni mfupi na huandaliwa vizuri sana kwa ufundi wa ngazi mbalimbali. Usishangae mtoto anafikia umri wa miaka 15 ameshakuwa fundi makanika, fundi mchundo, seremala au mjenzi mzuri sana.
Hebu Tanzania nasi tuamke, tujifunze hapo wizarani karibu na Magogoni, tuondoe mlundikano wa mitaala, mafundisho yaliyopitwa na wakati na sasa twende na zama hizi za kila mtu kuwa tayari kwa kazi.