Wiki iliyopita nimesikiliza kwa umakini mkubwa mjadala uliokuwa unaendelea katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimemsilikiza Mbunge wa Kuteuliwa rafiki yangu, James Mbatia, alivyokuwa aking’ang’ana na ‘Serikali Sikivu’ kuwaeleza kuwa mtaala unaofundishwa sasa unatupeleka shimoni.

Mimi nikizungumza vijana wanasema nimepitwa na wakati. Nimekuwa kisema sizielewi hata mbinu zinazotumika kufundisha, wananishangaa. Sisi wakati tunasoma hatukuwa na kitu kinachoitwa ‘tuition’. Waliku walikuwa wamakuja darasani, wanafundisha, wanatoa zoezi, tunalifanya, madafrari yanakusanywa, kisha walimu wanasahihisha.


Wakati walimu wanasahihisha madaftari, sisi wanafunzi tulikuwa tunakwenda kuwachanjia kuni kidogo, kuwachotea maji na kama kwetu – ilikuwa kama ni msimu – tunakwenda porini kuwakamatia senene, na hapa kwa ruhusa yako msomaji nitumie neno la Kihaya – kubonjela ebituzi (kuwatafutia uyoga).


Mwalimu alikuwa anaridhika. Pamoja na udogo wa mshahara, kama shida yake ni kuni sisi wanafunzi tulikuwa tunawezesha, kama ni senene tulikuwa tunamkamatia na kama ni mboga, uyoga tulikuwa tunamsogezea.


Kwa mantiki hiyo yeye alikuwa anatumia fedha zake kidogo zilizosalia kununua samaki, saruji, bati na gongo kidogo, ukiacha mwisho wa mwezi waliokuwa wanasafirsha nyota na primus kutoka Rwanda au Safari ilipoziduliwa mwaka 1977, lakini wengi walikuwa wanaishia kwenye ‘enkonyagi’ iliyokuwa inauzwa senti 10 kwa gandarefu.


Mawazo ya walimu yalitulia tuli, hawakuwaza dambwe au sh 100 ya tuition kwa kila mwanafunzi. Darasa la kwanza tulifundushwa kusoma, kuandika na kuhesabu. Masomo haya tulienda nayo hadi darasa la tatu, kisha tukaanza lugha (lakini tusisahau waliokuwa hawazungumzi Kiswahili shuleni ilikuwa wanavamishwa ekikongo (simbi). Hii ilitufanya wanafunzi kote Tanzania nzima tujue Kiswahili.


Mnyukano wa Serikali Sikivu na Mbatia umenikumbusha shairi hili:

KAMA MNATAKA MALI

Karudi Baba mmoja, toka safari ya mbali,

Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili,

Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali,

Wakataka na kauli, iwafae maishani.

Akatamka mgonjwa, ninaumwa kweli kweli,

Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali,

Naona roho yachinjwa, kifo kimenikabili,

Kama mwataka kauli, semani niseme nini.

Yakawatoka kinywani, maneno yenye adili,

Baba yetu wa thamani, sisi tunataka mali,

Urith tunatamani, mali yetu ya halali,

Sema iko wapi mali, itufae maishani.

Baba aliye kufani, akajibu lile swali,

Nina kufa maskini, baba yenu sina mali,

Neno moja lishikeni, kama mnataka mali,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali,

Baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili,

Akili yetu nyembamba, haijajua methali,

Kama tunataka mali, tutapataje shambani.

Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli,

Fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali,

Haya sasa buriani, kifo kimeniwasili,

Kama mnataka mali mtayapata shambani.

Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili,

Mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili,

Na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Fumbo wakatafakari, watoto wale wawili,

Wakakata na shauri, baada ya siku mbili,

Wote wakawa tayari, pori nene kukabili,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali,

Tangu zile za mibuni, hata zitupazo wali,

Na mvua ikaja chini, wakona na dalili,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Shamba wakapalilia, bila kupata ajali.

Mavuno yakawajia, wakafaidi ugali,

Wote wakashangilia, usemi wakakubali,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakawanunua ngómbe, majike kwa mafahali,

Wakapata na vikombe, mavazi na baiskeli,

Hawakuitaka pombe, sababu pombe si mali,

Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali,

Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali,

Walikiweka kibao, wakaandika kauili,

KAMA MNATAKA MALI, MTAYAPATA SHAMBANI.

Umelisoma shairi hili. Unalikumbuka? Unaona mantiki liliyosheheni? Leo, tunadandia treni iliyo kasi kwa mbele. Tatizo letu kubwa ilikuwa ni ujinga, maradhi na umasikini. Sheiri hili tulilofundishwa darasa la tatu, linatupa mbinu za kukabiliana na maadui hawa, kuondoa adui njaa, kujenga nyumba bora, kutogugumia pombe na kuwekeza faida inayopatikana kwa kununua ng’ombe, usafiri (baikeli wakati huo, gari kwa sasa) na kuhubiri bila aibu njia ya ufanisi. Mali inapatikana shambani.


Je, leo watoto wetu wanafundishwa haya. Hatujajiingiza kwenye taifa la kusadikika? Mtoto wa darasa la kwanza hapa nchini anafundishwa sijui Tahoma au Teknohama. Akifika Chuo Kikuu atafundishwa nini? Ndugu msomaji wasiliana nami kuchangia mjadala huu, kama tupo kwenye mkondo sahihi au tumepotea njia. Ila ukikubaliana name, unaweza pia ukashajihisha tujaribu ujinga.