Na Stella Aron JamhuriMedia
Suala la afya ya uzazi lina mchango mkubwa sana katika kutimiza ajenda ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka 2030.
Suala hii linaenda sanyari na idadi ya watu, rasilimali zinazohitajika na hata mustakabali wa uchumi na maendeleo ya jamii.
Kwa kutambua mchango wa sula hilo Umoja wa Mataifa umekuwa ukisisitiza lipewe uzito kuanzia ngazi ya chini kwa vijana. Serikali na mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yameitikia wito kwa kutoa elimu ya afya ya uzazi
Afya ya uzazi ni suala ambalo ni muhimu katika jamii yoyote, lakini upatikanaji wa huduma hii hukabiliwa na changamoto mbalimbali na hivyo kuwaweka wasichana na wanawake katika mazingira magumu.
Nchini Tanzania juhudi za Serikali zinasaidia kulinda wasichana na wanawake katika kupata huduma muhimu za afya ya uzazi lakini pia mashirika yasiyo ya kiserikali yanaziba pengo ambalo linasalia.
FAIDA ZA ELIMU YA AFYA YA UZAZI
Kuna faida nyingi zitokanazo na elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ikiwemo ya kuepuka mimba za utotoni, kuepuka changamoto za uzazi, kuepuka ndoa za utotoni na magonjwa
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na bingwa wa magonjwa ya wanawake, Profesa Andrea Pembe, anasema kuwa elimu ya afya ya uzazi inasaidia kuzuia mimba zisizotarajiwa na utoaji wa mimba usio salama.
Akizungumza katika mahojiano mara baada ya kumalizika kwa katika Kongamano la wadau wa masuala ya Afya ya Uzazi lililoandaliwa na Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), anasema kuwa ili kusaidia kupunguza changamoto zitokanazo na mimba zisizotarajiwa ni vyema sasa elimu ya afya ya uzazi ikatolewa mapema kwa vijana.
Anasema kuwa elimu afya ya uzazi ianze kutolewa kabla ya watu hawajaanza kushiriki tendo la ndoa ili kuepuka mimba za ujanani lakini pia kuepuka kushiriki kwenye utoaji wa mimba usio sahihi.
“Kipindi hiki cha sayansi na teknolojia kuna masuala mengi ambayo yanakuja na vijana wetu wanajifunza na ndio maana vijana wengi wanapata mimba zisizotarajiwa na mwishowe huchukua maamuzi mabaya ya kushiriki kutoa mimba.
“Tuna amini kuwa kama vijana watapa taarifa sahihi ya masuala ya afya uzazi kujikinga na huduma dhidi ya Virusi vya UKIMWI, kujikinga na mimba za utotoni katika umri mdogo na masuala ya ukatili wa kijinsia, masuala lishe na magonjwa ya kuambukiza, afya ya kili, vijana wa kiume na kike kuendelea na masomo na masuala ya kuwezeshwa kiuchumi na kinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi,” anasema.
Anasema,mimba zisizotarajiwa zinazuilika hivyo ni muhimu elimu ya masuala ya afya ya uzazi na kujitambua itolewe mapema ili kuzuia wimbi la mimba za utotoni na utoaji mimba usio salama.
“Elimu ya afya ya uzazi, iliyotolewa zamani ni tofauti na elimu ya sasa kutokana, maendeleo ya sayansi na teknolojia, yamesababisha kugundulika kwa dawa na vimelea mbalimbali ambavyo hapo awali havijulikani” anasema.
Profesa Pembe anasema kuwa kuna madhara mengi ambayo mtu anayeshiriki katika utoaji mimba kiholela yupo hatarini kukumbana nayo ni kifo,ugumba au figo kushindwa kufanya kazi.
“Tanzania suala zima la utoaji mimba lipo juu kama nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kati,wakina mama 36 kati ya 1,000 wanatoa mimba hivyo bado suala hili linahitaji elimu ili kupunguza changamoto hiyo,” anasema.
Anasema kuwa ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030 kwa wa nachama wa Umoja wa Mataifa ikiwamo Tanzania inatambua kuwa huduma ya uzazi wa mpango ni haki ya kila mtu binafsi na mume na mke bila kujali mahali au namna wanavyoishi, au wana pato la kiasi gani.
UMUHIMU WA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA
Kukosa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ni miongoni mwa sababu inazosababisha kuendelea kwa vitendo vya ukatili ndani ya jamii.
Afisa Mradi kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Dodoma (DOYODO), Lilian Mwaluka, anasema kuwa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ni muhimu kwani huwasaidia katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Anasema kuwa kama kijana akiwa na uelewa juu ya afya ya uzazi kuna uwezekano wa kupunguza kushiriki matukio ya kikali.
“Kuna matukio mbalimbali ya kikatili ambayo chanzo chake huwa ni mahusiano pindi mimba isiyotarajiwa ikitokea hivyo ni vyema sasa vijana wakapata elimu ya afya ya uzazi,’ anasema.
MATUMIZI YA NJIA ZA UZAZI KWA SIRI
Mratibu wa Taasisi ya Tupange Pamoja, Kylie Gyubi,anasema vijana wanapaswa kujitambua na kutambua afya zao, kwa kutembelea vituo vya afya na kukutana na wataalamu wa afya ya uzazi salama ili kupima na kupata ushauri juu ya afya ya uzazi.
“Vijana wengi wamekuwa wakitumia njia za uzazi wa mpango kwa siri na bila kufuata ushauri wa wataalam wa afya, jambo linawasababishia kupata madhara kiafya lakini chanzo kikiwa ni kukosa kukosa taarifa sahihi sahihi juu ya dawa hizo” anasema Gyubi.
Hata hivyo anasema kuwa vijana wamekiri kuwa na taarifa zaidi za uzazi wa mpango kuliko afya ya uzazi, kutokana na ukweli kwamba mara nyingi, huduma hiyo hutolewa kwa vijana ambao tayari wamepata watoto na kuanza kuhudhuria kliniki.
“Tumegundua kuwa vijana wengi hawana elimu ya afya ya uzazi badala yake wamekuwa wakitumia dawa za uzazi wa mpango bila ya kuwa na elimu na kutumia ndivyo sivyo.
“Tunaamini kuwa afya ya uzazi ni zaidi ya uzazi wa mpango, inayomuwezesha kijana kutambua mabadiliko ya mwili wake jinsi ya kuishi na kuyamudu mabadiliko hayo,” anasema mratibu huyo.
Kijana Juma Saidi mkazi wa Chalinze,amesema kuwa kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi za afya ya uzazi kwa vijana, vijana wengi wamejikuta wakiingia kwenye mgogoro wa malezi ya watoto bila kujipanga,huku wasichana wakikatiza masomo kwa ajili ya mimba, kutokana na uelewa mdogo juu ya afya ya uzazi kwa vijana.
“Vijana wengi wamejikuta wanalazimika kuoana kwa kuwa tayari wameshapeana mimba, na kuanza majukumu ambayo hawakuwa wamejipanga jambo ambalo, linasababisha ndoa kuvunjika na kuingia kwenye migogoro mikubwa na kuwa na ongezeko kubwa la watoto wa mitaani” amesema kijana huyo.
Anaongeza kuwa, vijana wengi hufundishana wenyewe na kuanza kushiriki tendo la kujamiiana, huku wengi wakiamini kuwa, kushiriki tendo hilo ndani ya dakika tano, hauwezi kupata maambukizi ya UKIMWI, taarifa ambayo si za kweli, tendo la kujamiiana linaweza kuambukiza magonjwa ya ngono, kansa ya shingo ya kizazi na ugonjwa wa UKIMWI.
Naye Mwanaisha Matela mkazi wa Kibaha jijini Dar es Salaam anasema kuwa ni vyema elimu ya afya ya uzazi ikawa endelevu kwa vijana ili kubadili fikra potofu ambazo zimekuwa zikiwasababisha changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kifo.
“Kabla ya kupata elimu ya afya ya uzazi tulikuwa tunafahamu kuwa unapotumia njia za uzazi wa mpango kwa mwanamke huharibu umbile lake lakini kwa sasa nimegundua si kweli kwamba njia za uzazi wa mpango haziwezi kuharibu umbile la mwanamke badala yake inamkinga na mimba zisizotarajiwa na magonjwa” anasema Mwanaisha.
mwisho