· Yatangaza ufadhili mpya kwa miradi mitano nchini.
Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB) imeahidi kuongeza ufadhili na mikopo ya masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano baina ya Benki hiyo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa EIB, Mhe. Thomas Östros, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, katika Makao Makuu ya Benki hiyo mjini Luxembourg.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Östros alieleza kuwa uamuzi huo umetokana na kuridhishwa kwao na mafanikio yanayoendelea kupatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, hususan katika maeneo ya utawala bora, usimamizi makini wa rasilimali fedha, pamoja na ubunifu katika kuibua na kutekeleza miradi ya kimkakati yenye manufaa kwa wananchi.
Alibainisha kuwa Benki hiyo imevutiwa na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya usafiri kama barabara, reli ya kisasa, viwanja vya ndege, pamoja na uboreshaji wa huduma muhimu za kijamii kama hospitali na shule.
Aidha, Mhe. Östros alisisitiza kuwa EIB inatambua jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuhimiza matumizi ya nishati safi kama sehemu ya mkakati wa kulinda mazingira. Alieleza kuwa Benki hiyo ipo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mipya ya nishati jadidifu, ikiwemo uzalishaji wa umeme kwa kutumia nguvu ya upepo.
Miongoni mwa miradi iliyoainishwa kupata ufadhili mpya kutoka EIB ni; Awamu ya pili ya Mradi wa Maji Safi na Maji Taka jijini Mwanza (LV WATSAN), Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) – Awamu ya Nne na ya Tano, Mradi wa Usafi wa Fukwe za Bahari (COPIP), Mradi wa Maji Safi Zanzibar (Zanzibar Water Security Project), Mikopo ya masharti nafuu kwa mabenki ya biashara ili kuimarisha sekta binafsi.

Kwa upande wake Waziri Kombo ameushukuru Uongozi wa EIB kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na benki hiyo na kuhakikisha ufadhili na mikopo inayotolewa inawanufaisha wananchi.
Ushirikiano huu unaonesha dhamira ya dhati ya Benki ya Uwekezaji ya Ulaya katika kuiunga mkono Tanzania kwenye juhudi zake za kufikia maendeleo jumuishi na endelevu.
Ziara hiyo ya Waziri Kombo nchini Ubelgiji inalenga kukutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya na kujadili kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo nchini na kuendelea kukuza ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya.
Waziri Kombo yupo nchini Ubelgiji kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Aprili 14 hadi 2025.

