Mmiliki wa duka la nyama linaloitwa Edwin Butcher la Rwamishenye, Bukoba, amejitokeza na kusema kuwa bucha yake haina uhusiano wowote na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Bukoba, Dk. Anatory Amani, au udini kama ilivyodaiwa na baadhi ya watu.

Katika toleo lililopita, gazeti hili liliorodhesha tuhuma zinazosambazwa dhidi ya Meya Amani, kuwa alichangia ufunguzi wa bucha hiyo kama sehemu ya kuchochea udini kwa wakazi wa Mji wa Bukoba wasinunue nyama kwenye maduka ya Waislamu wa mji huo.

 

Mmiliki wa bucha hiyo, Edwin Pastory Bankobeza, amewasiliana na JAMHURI kwa njia ya simu na kusema madai hayo ni uvumi unaopaswa kupuuzwa kwani bucha hiyo aliianzisha yeye bila mkono wa Dk. Amani.

 

“Nimefungua bucha mwenyewe na nimeandika jina langu kutangaza biashara yangu. Wala sitangazi biashara ya kidini wala nini, haimuuzii Mwislamu wala Mkristo, ni bucha ya jamii nzima iliyonizunguka.

 

“Namuuzia mtu yeyote aliyeumbwa na Mungu. Hata mwenyewe Amani huyo simjui, namuona kama meya tu, hata ukimwambia Amani nenda uniitie Edwin hanifahamu… bucha yangu haina uhusiano wowote na Meya Amani,” Bankobeza ameiambia JAMHURI.

 

Katika kuthibitisha hilo, alisema hata hiyo bucha amepangishwa nyumbani kwa Mwislamu. “Anayenipangisha ni Bashiru Ali, Mwislamu. Halafu mimi nifungue bucha ya kidini nyumbani kwa Mwislamu kweli? Inaingia akilini hiyo? Watu waache kutuchonganisha bure,” alisema.