Mahakama Kuu ya Tanzania (Divisheni ya Biashara) imeitia hatiani Ecobank Tanzania Limited kwa kumwibia mteja wake, Kampuni ya Future Trading Limited, Sh milioni 66 kutoka kwenye akaunti yake.

Fedha hizo zimeibwa kwenye akaunti hiyo kupitia huduma ya internet banking na kuziingiza katika akaunti iliyoko nchini Afrika Kusini.

Hukumu hiyo ya kesi namba 68 ya mwaka 2014, imetolewa na Jaji Barke Sehel. Inahusu wizi huo uliofanywa kwenye benki hiyo Tawi la Uhuru jijini Dar es Salaam katika akaunti Na. 0010135400019801 ya Kampuni ya Future Trading Limited.

Kwa hukumu hiyo, Ecobank Tanzania Limited imetakiwa imlipe mlalamikaji – Kampuni ya Future Trading Limited – Sh milioni 66.24 ambazo zilihamishwa kinyemela kutoka kwenye akaunti ya mteja huyo kwenda kwa mtu asiyeidhinishwa.

Pili, Ecobank Tanzania Limited imlipe mlalamikaji Sh milioni 25 ikiwa ni malipo ya fidia kwa madhara yaliyotokana na benki husika kufanya malipo bila idhini ya mteja.

Tatu, Ecobank imlipe mlalamikaji riba ya kiwango cha asilimia saba kuanzia siku ya hukumu hadi itakapokuwa imemaliza kulipa deni hilo.

Nne, mteja arejeshewe gharama za uendeshaji wa kesi hiyo.

Mkurugenzi wa Future Trading Company Limited, Abubakar Suweid, amesema licha ya hukumu hiyo, Ecobank imegoma kumlipa.

“Januari 3, mwaka huu [2018] nimeiandikia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) malalamiko yangu, lakini sijafanikiwa. Sijapata msaada wowote,” amesema Suweid.

Fedha hizo ziliibwa na wafanyakazi wa Ecobank Machi 10, 2014 kupitia mfumo wa internet banking. Jaji Sehel, amejiridhisha pasi na shaka kuwa Kampuni ya Future Trading Limited iliingizwa kwenye huduma ya Internet banking bila ridhaa yake; na kwamba hata fomu za kufunguliwa kwa akaunti ya kampuni hiyo kwenye sehemu ya huduma hiyo kuliwekwa alama ya “X” kuonyesha kuwa haikuihitaji huduma hiyo.

Walalamikaji waliripoti polisi na kufunguliwa jalada Na. IR/CD/1060/2014 na baadaye kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania (Divisheni ya Biashara).

Mahakama Kuu imethibitisha kuwa sahihi ya mkurugenzi wa Future Trading Company Limited ilighushiwa. Fomu zilizotumika kuingiza kwenye huduma ya kibenki kwa njia ya mtandao (internet banking) haikuwa na mihuri ya benki wala sahihi ya ofisa aliyeidhinisha kuingia kwenye huduma hiyo.

Fomu hazikuwa na mhuri wa kampuni, sahihi inayodaiwa kuwa ni ya mkurugenzi haifanani na sahihi zilizopo katika fomu ya kufungulia akaunti Ecobank.

Namba za simu zilizowekwa kwenye fomu mahususi za kujiunga (set up form) hazijulikani na haziko kwenye fomu iliyojazwa na Future Trading Company Limited wakati wa kufungua akaunti.

Mahakama imejiridhisha kuwa fomu hizo (set up form) pia zilikuwa na anuani ya ofisi (physical address) ambayo si sahihi.

Imebainika kuwa mwandiko uliotumika kujaza fomu hiyo si wa viongozi wa Future Trading Company Limited; na wala hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa wenye kampuni hiyo walipewa nywila (password) ya huduma ya internet banking; hapakuwapo mafunzo au maelekezo yoyote ya huduma ya internet banking, hapakuwa na maazimio ya bodi ya kuruhusu benki kuwapatia Future Trading Company Limited huduma hiyo.

Mahakama imesema uhakiki wa mtumaji wa fedha na mpokeaji kama inavyoelekezwa na BoT haukufanyika kama inavyoelekeza kwenye miongozo ya BoT ya huduma za benki za kielektroniki ya mwaka 2007.

Hatua nyingine

Kampuni ya Future Trading Ltd inasema kuwa ilibaini hali isiyo ya kawaida kwenye akaunti yao Machi 13, 2014 kwa fedha kuondolewa katika akaunti bila idhini yake.

Kiasi cha fedha kilichochotwa kwenye akaunti hiyo ni Sh milioni 66.24 na baada ya benki kuulizwa walielezwa kuwa fedha hizo zimehamishwa kwenda kwa mpokeaji aliyeko nchini Afrika Kusini kwa njia ya ‘telegraphic transfer’, ikidaiwa kuwa ni maagizo ya Kampuni ya Future Trading Company Limited.

Kampuni hiyo ilikana madai hayo ya kuagiza fedha hizo kuhamishwa na kuitaka benki izirejeshe.

Kati ya mambo ambayo mlalamikaji aliomba mahakama iamue ni kulipwa Sh milioni 66.24; kulipwa faini ya Sh milioni 50 kutokana na kushindwa kutunziwa akiba yao katika benki hiyo, sambamba na usumbufu waliosababishiwa kutokana na tukio hilo la wizi wa fedha zao.

Mlalamikaji aliomba alipwe Sh milioni 50 za fidia kutokana na kukiukwa kwa mkataba wa kibenki kati yake na benki; alipwe malipo ya usumbufu wa jumla kadiri itakavyoamuliwa na mahakama; na alipwe gharama za uendeshaji wa kesi.

 

Mchezo ulivyokuwa

Katika kesi hiyo, shahidi kwa upande wa mlalamikaji, Abubakar Suweid, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni iliyoibiwa, aliieleza mahakama kuwa alibaini wizi huo Machi 13, 2014.

Alisema alipigwa butwaa baada ya kubaini Sh milioni 66.24 zimehamishwa na alipoutaarifu uongozi wa benki alielezwa kuwa fedha hizo zimehamishwa na kupokewa nchini Afrika Kusini kwa njia ya ‘telegraph transfer’ kupitia maelekezo ya kielektroniki yaliyokuwa yakitolewa na barua pepe ya mlalamikaji iliyosajiliwa katika benki hiyo.

Suweid amesema kwamba hakuna popote ambako alisaini kuidhinisha uhamishaji huo wa fedha na wala hakutumia mfumo wa kielektroniki kufanya mawasiliano.

Amesema pamoja na malalamiko yake, benki hiyo iligoma kurejesha fedha hizo.

Akaiambia mahakama kuwa kampuni imeshindwa kuendesha shughuli zake na kupoteza fursa nyingi za kibiashara na muda.

Katika mahojiano na wakili mahakamani (cross examination), shahidi namba moja upande wa mlalamikaji alikiri kwamba wakati akifungua akaunti katika benki hiyo alitoa anuani ya barua pepe rasmi kwa ajili ya mawasiliano.

Alisema hakutoa nywila kwa benki hiyo kuweza kuingia kwenye akaunti yake, bali aliwapa namba yake ya simu kwa ajili ya mawasiliano.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank, Mwanahiba Hussein, ameulizwa kuhusu utekelezaji wa hukumu ya Mahakama Kuu, lakini amekataa kuzungumza kwa undani kwa madai kuwa suala hilo bado liko mahakamani.

Hata hivyo, JAMHURI limefuatilia mahakamani na kubaini kuwa hakuna rufaa iliyokatwa, isipokuwa kumetolewa zuio la muda la kutokamatwa na kunadiwa mali za benki hiyo.