Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umefikia hatua muhimu kwa kufanikisha upatikanaji wa sehemu ya kwanza ya ufadhili wa nje, hatua inayoweka msingi madhubuti kwa uwekezaji mkubwa zaidi wa miundombinu katika kanda hii. Ufadhili huu, uliopatikana kutoka kwa muungano wa taasisi za kifedha, unaonesha imani kubwa katika ufanisi wa mradi huu na uwezo wake wa kuleta mageuzi katika sekta ya nishati ya Afrika Mashariki.

Washirika wa kifedha wanaounga mkono mradi huu ni pamoja na benki mashuhuri za kikanda kama African Export-Import Bank (Afreximbank), The Standard Bank of South Africa Limited, Stanbic Bank Uganda Limited, KCB Bank Uganda, na The Islamic Corporation for the Development of the Private Sector (ICD).

Ahadi hii kutoka kwa taasisi hizi za kifedha inaonesha uungwaji mkono mkubwa kwa maono ya EACOP na nafasi yake muhimu katika kufanikisha usafirishaji wa mafuta ya Uganda kwenye soko la kimataifa.

Maendeleo ya mradi wa EACOP katika picha.

Kukamilika kwa sehemu hii ya kwanza ya ufadhili ni hatua muhimu kwa EACOP na wanahisa wake: TotalEnergies (62%), Uganda National Oil Company Limited (UNOC 15%), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC 15%), na China National Offshore Oil Corporation (CNOOC 8%). Ushirikiano wao wa pamoja unahakikisha kuwa mradi huu unasonga mbele kama mfumo wa kipekee wa kusafirisha mafuta, ambao utaongeza maendeleo ya kiuchumi kwa Uganda na Tanzania.

Ujenzi wa bomba hili lenye urefu wa kilomita 1,443, likijumuisha kilomita 296 nchini Uganda na kilomita 1,147 nchini Tanzania, umepiga hatua kubwa. Kufikia mwezi machi mwaka 2025, maendeleo ya mradi yamefika asilimia 55%, huku kipaumbele kikiwekwa kwenye usalama, uendelevu wa mazingira, na ushirikishwaji wa jamii za wenyeji.

Zaidi ya raia 8,000 kutoka Uganda na Tanzania wameajiriwa katika mradi huu, huku zaidi ya saa 400,000 za mafunzo zikitolewa kwa wafanyakazi ili kuwajengea ujuzi wa msingi.

Hadi sasa, zaidi ya dola milioni 500 za kimarekani zimesambazwa katika uchumi wa ndani kupitia ununuzi wa bidhaa na huduma, jambo linalodhihirisha athari chanya za kiuchumi za mradi huu.

Mradi wa EACOP ukikamilika, bomba hili litakuwa na uwezo wa kusafirisha hadi mapipa 246,000 ya mafuta ghafi kwa siku kutoka Kabaale, wilaya ya Hoima nchini Uganda, hadi kwenye rasi ya Chongoleani, Tanga nchini Tanzania.

Bomba hili limeundwa kwa teknolojia ya kisasa, likiwa na mfumo wa bomba lenye upana wa inchi 24 lenye insulation na lililozikwa ardhini, vituo sita vya kusukuma mafuta, na vituo viwili vya kupunguza shinikizo. Eneo la usafirishaji wa mafuta baharini lililopo Tanzania litajumuisha mtambo wa umeme wa jua wa 3 MWp, kuonyesha dhamira ya mradi wa kutumia nishati mbadala.

Kwa kuzingatia viwango vya juu vya mazingira na kijamii, mradi wa EACOP umejipanga kufuata miongozo ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) na Kanuni za Equator, kuhakikisha utekelezaji wake unazingatia uwajibikaji wa kijamii na uendelevu wa mazingira. Aidha, mradi huu umeunganishwa na gridi za kitaifa za umeme, ambazo zinategemea nishati ya maji, ili kupunguza athari za kaboni.

Mradi wa EACOP unawakilisha zaidi ya bomba la kusafirisha mafuta; ni alama ya ushirikiano wa kikanda, maendeleo ya kiuchumi, na ustawi wa viwanda. Uwekezaji katika mafunzo, ajira, na ununuzi wa ndani unahakikisha kuwa jamii zinazopitiwa na bomba hili zinanufaika na fursa za kiuchumi za muda mrefu.

Kwa msaada wa taasisi kuu za kifedha na dhamira ya maendeleo endelevu, EACOP imejizatiti kuwa kichocheo cha mabadiliko ya kiuchumi Afrika Mashariki.

Kadri mradi unavyoendelea kuelekea kukamilika, unaendelea kuthibitisha kuwa miundombinu ya nishati endelevu inaweza kupatikana kwa njia ya ushirikiano, uvumbuzi, na kufuata viwango vya kimataifa. Kwa msingi madhubuti wa kifedha sasa ukiwa umekamilika, EACOP itachochea ukuaji wa uchumi, kuboresha biashara za kikanda, na kuchangia usalama wa nishati wa Afrika Mashariki kwa miaka ijayo.