Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilimanjaro

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kushirikiana na mkandarasi wa kusambaza mabomba PANYU CHU KONG STEEL PIPE (PCK) wametoa ufadhili wa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa vijana 80 wa Kitanzania yatakayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), lengo ikiwa ni kuwapa ujuzi katika fani mbalimbali pamoja na fursa za ajira katika ujenzi wa mradi huo.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango huo, iliyofanyika katika Chuo cha VETA Moshi mkoani Kilimanjaro, Meneja wa Maudhui ya Ndani (Local Content), Bi. Neema Kweka amesema ufadhili huu ni kielelezo cha kujitolea kwa mradi wa EACOP katika kutekeleza sera ya maudhui ya ndani kwenye mradi (Local Content) kwa kuwapa fursa fursa wazawa.

Meneja wa Kuijengea Uwezo Jamii kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP), Bi. Martha Makoi (kulia) akizungumza na wanufaika wa ufadhili wa mafunzo yatakayotolewa kwa vijana 80 wakitanzania yaliyofadhiliwa na kampuni ya PANYU CHU KONG STEEL PIPE (PCK) ambayo ni mkandarasi wa kusambaza mabomba katika mradi wa EACOP, wakati wa hafla fupi ya uzinduzi iliyofanyika katika Chuo cha VETA Moshi mkoani Kilimanjaro jana. katikati ni Meneja wa Maudhui ya Ndani (Local Content) kutoka EACOP, Bi. Neema Kweka na kushoto ni Bw. Adonis Kimbembe ‘ Package Manager’ kutoka kampuni ya PCK.

“EACOP tunaendelea kutekeleza sera hii kwa kununua huduma za ndani, kutoa ajira, kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo wazawa, ikiwemo kuwapa nafasi ya kupata ujuzi kupitia mafunzo na wakandarasi wa kimataifa waliopo katika mradi,” .

“Na ndio maana mkandarasi wetu, PCK wamefadhili mafunzo haya kwa vijana 80 kutoka vituo vya VETA Moshi, Shinyanga na Kilindi, amesema Bi. Kweka.

Amesema Programu hiyo ya mafunzo itatolewa kwa muda wa miezi kumi na mbili (12) ikiwa na mada mbalimbali zitakazofundishwa ikiwemo Ufungaji wa Mabomba na Mafunzo ya Mitambo ya Boiler, Ujenzi na Ufyatuaji wa Matofali, Ufungaji wa Umeme, ufundi Chuma na uendeshaji wa Mitambo.

“Baada ya mafunzo haya, wahitimu watapewa vyeti vitakavyowawezesha kukubalika katika soko la ajira la kimataifa, ikiwemo kufanya kazi katika mradi wa EACOP, miradi ya kimkakati ya Serikali na hata kujiajiri wao wenyewe,” alisema Bi. Kweka.

Mwalimu wa Umeme kutoka chuo cha VETA Moshi Bw. Salimu Mgonja (kulia) akifafanua jambo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango wa ufadhili wa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa vijana 80 wa kitanzania yatakayoendeshwa katika vituo vya VETA Moshi, Shinyanga na Kilindi kwa kipindi cha miezi kumi na mbili (12), wapili kulia ni Package Manager Bw. Adonis Kimbembe kutoka kampuni ya PANYU CHU KONG STEEL PIPE (PCK) ambayo ni (mkandarasi wa kusambaza mabomba mradi wa EACOP), (katikati) ni Bi. Gloria Njau Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Idara ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na (kushoto kwake) ni Mkuu wa Chuo cha VETA Moshi, Mhandisi Lupakisyo Mapamba na wapili kushoto ni Meneja wa Maudhui ya Ndani (Local Content) kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP), Bi. Neema Kweka

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Idara ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Bi. Gloria Njau ameushukuru mradi wa EACOP kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha Watanzania hususani vijana wanapata ujuzi wa fani mbalimbali kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi.

“Programu hii italeta matokeo makubwa, sio tu kubadili maisha ya vijana, bali pia kuzalisha wataalamu watakaotumika katikia ujenzi wa nchi,”

“ Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo, hivyo mpango huu wa mradi wa EACOP utazalisha wataalamu wengi katika fani mbalimbali na kuwa tegemeo katika ujenzi wa nchi,” amesema.

Mkuu wa Chuo cha VETA Moshi, Mhandisi Lupakisyo Mapamba (kushoto) akielezea namna EACOP ilivyowasaidia kupata mitambo ya kisasa inayotumika kufundishia vijana katika kada mbalimbali ikiwemo Ufungaji wa Mabomba, Umeme na Uendeshaji wa Mitambo, wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mafunzo kwa vijana 80 kumalizika, iliyofanyika katika Chuo cha VETA Moshi mkoani Kilimanjaro jana. (kushoto kwake) ni Bw. Adonis Kimbembe kutoka kampuni ya PCK, (watatu kulia) ni Meneja wa Maudhui ya Ndani (Local Content) kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP), Bi. Neema Kweka.

Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Moshi, Mhandisi Lupakisyo Mapamba amesema kupitia ufadhili huo, Chuo cha Moshi pekee kimeweza kutoa vijana 50, wavulana 41 na wasichana tisa , ambao watapewa mafunzo katika sekta ya Mafuta na Gesi.

“Tunathamini ushirikiano uliopo baina yetu na EACOP na PCK. Kwani kupitia ushirikiano huu , tunatarajia kuona mabadiliko chanya kwa vijana hawa kitaaluma na kiuchumi,” amesema Mhandisi Mapamba.

Amesema ufadhili huo wa masomo umehusisha vituo vya VETA, kikiwemo chuo cha VETA Moshi chenye wanafunzi 50, VETA Shinyanga ( wanafunzi 20) na VETA Kilindi chenye wanafunzi 10 pekee.

Mmoja wa wanufaida wa ufadhili huo, Bi. Habiba Omary mbali ya kuishukuru mradi wa EACOP kupitia mkandarasi wake PCK, amesema mchakato wa kuwapata washindi ulikuwa wa wazi na wahaki hivyo kupitia ufadhili huo, ana imani kuwa wataalamu wengi wenye sifa za kimataifa watapatikana na kuleta tija katika sekta mbalimbali ikiwemo ya ujenzi, gesi na mafuta.

Naye Bw. Emanuel Msangi ambaye pia ni mnufaika wa ufadhili huo, amesema zaidi ya vijana 1849 walishiriki kwenye usaili, lakini waliofanikiwa kupata nafasi ya ufadhili huo ni 80 pekee.

Wafanyakazi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanufaika wa ufadhili wa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa vijana 80 wa kitanzania yatakayoendeshwa katika vituo vya VETA Moshi, Shinyanga na Kilindi kwa kipindi cha miezi kumi na mbili (12), punde mara baada ya hafla fupi ya uzinduzi wa mafunzo hayo kumalizika, iliyofanyika katika Chuo cha VETA Moshi mkoani Kilimanjaro jana.

Mbali na kutoa mafunzo, mradi wa EACOP pia umekuwa ukisaidiai uboreshaji wa miundombinu katika vyuo vya ufundi stadi hapa nchini na kununua vifaa na teknolojia vinavyotumika kufundishia kwa nadharia na vitendo.

Mradi wa EACOP una urefu wa kilomita 1,443 kuanzia Hoima nchini Uganda hadi Peninsula ya Chongoleani katika Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kusafirisha mafuta ghafi kwenda kwenye soko la kimataifa.

Washirika wa mradi ni Total Energies, yenye asilimia 62, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC), kila moja ikiwa na asilimia 15, na Kampuni ya China National Offshore Oil Corporation (CNOOC), inayoshikilia asilimia 8.