Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Handeni

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) kwa kushirikiana na mkandarasi Mkuu wa ujenzi wa bomba hilo, kampuni ya China Petroleum Pipeline (CPP) umewataka wajasiriamali/wafanyabiashara katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kuchangamkia fursa za kutoa huduma ya chakula kwa ajili ya kuhudumia takriban wafanyakazi 500 watakaokuwa wanafanya kazi katika kambi yake namba 15 (MCPY 15) iliyopo wilayani humo.

Akizungumza wakati wa mkutano huo na wafanyabisáshara katika wilaya hiyo hapo jana, Meneja wa Kuijengea Uwezo Jamii kutoka mradi wa EACOP Martha Makoi amesema lengo la mkutano huo ni kukutana na wafanyabiashaea wa sekta ya chakula wilayani humo kuwajulisha juu ya fursa za biashara zitakazopatikana baada ya kuitambulisha kampuni iliyoshinda tenda ya kutoa huduma katika kambi hiyo .

“Tumeipata kampuni ya Mamwaka Catering iliyoshinda zabuni kwa ajili ya kutoa huduma ya chakula katika kambi ya MCPY 15 hivi karibuni ambayo itahitaji mahitaji mbalimbali ya vyakula kama vile mchele, nyama na nyanya kutoka kwa wafanyabishara wa ndani,”

“Hivyo, tumetumia mkutano huu kuwakutanisha wafanyabiashara wa chakula wilayani hapa ili kukutana na kampuni hiyo na kupeana taarifa ya mahitaji yatakayokuwa yanahitaji kabla ya mchakato wa kuwapata wafanyabiashara watakaosambaza mahitaji ya chakula kwa ajili ya kulisha kambi hiyo,” amesema Makoi.

Amesema utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya maagizo ya Serikali na utendaji wa EACOP katika kuhakikisha zinapotokea fursa za ajira au kutoa huduma katika maeneo yote ya mradi kipaumbele kinatolewa kwa wazawa wa maeneo walio karibu na mradi.

“Hii ni katika utekelezaji wa sheria ya kuwawezesha wazawa ( Local Content) ambapo walio karibu na maeneo ya madi ndio wanakuwa kipaumbele cha kwanza kufikiriwa katika fursa zinazopatikana kwenye maeneo ya mradi,” amesema Ms Makoi.

Amesema utaratibu huo umekuwa ukifanyika katika kambi zote za mradi huo ambazo zimekamilika ambapo kampuni zinazoshinda zabuni ya kutoa zinafanya kazi na wafanyabishara walio katika maeneo hayo.

Meneja wa maudhui ya ndani wa CPP, Mercy Ikaji amesema kambi hiyo kupitia kampuni ya Mamwaka Catering itatoa fursa za kiuchumi kwa wafanyabishara wa wilaya hiyo.

“ Mpango huu utasaidia wafanyabiashara kuuza bidhaa zao mbalimbali za chakula kwenye kambi hii na kujiingizia kipato,”

“CPP kwa kushirikiana na EACOP tunahakikisha wakazi wazawa wanaozungukwa na mradi wanafaidika na fursa zilizopo katika maeneo yao ili kukuza kipato chao,” amesema Ms Ikaji.

Amesema katika kambi hiyo, kampuni nyingine , RADSA pia imeshinda tenda ya usafi na kutoa fursa kwa wafanyabisahara wanaojishughulisha na sekta hiyo .

Amesema kati ya kambi hizo 16, tayari kambi tatu, zikiwemo MCPY 8 ( iliyopo Igunga) na MCPY 6( iliyopo Kagera) zimekamilka na kutoa fursa za ajira kwa wazawa wa maeneo hayo kupitia huduma mbalimbali za kijamii katika makambi hayo.

Akiongea wakati akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Habib Rashid Mbota ameusifu mradi wa EACOP kwa kushirikiana na mkandarasi kwa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa wa wilaya hiyo ili kuwainua kiuchumi.

“Tupo tayari kwa ajili ya kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na mradi wa EACOP;”, amesema Bw Mbota.

Amewataka wafanyabiashara wilayani humo kuchangamkia fursa hiyo na kufanya biashara kwa uaminifu.

Kwa upande wa Meneja wa Biashara wa Halmashauri Mji wa Handeni , Mr Paulo Lusinde amesema zaidi ya wafanyabishara 100 wanaojihusisha na sekta ya chakula walihudhuria mkutano huo kwa ajili ya kuchangamkia fursa hiyo.

“Tumeweza kuwakusanya watoa huduma mbalimbali wakiwemo wauza nyama, nafaka mbalimbali, mbogamboga na wengine kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huu,”

“Utaratibu utakaotumika ni kwa wafanyabiashara waliosajiliwa kuomba kutoa huduma zilizo ndani ya uwezo wao kulisha katika kambi hiyo kupitia kampuni ya Mamwaka,” amesema Bw Lusinde.

Mmoja wa wafanyabishara Anastazia Temba amesema fursa hiyo itawasaidia kuwainua kiuchumi hasa wafanyabiashara wanawake ambao wengi wao wanajihusisha na biashara ya chakula.

“Tunapata fursa mbalimbali zinazotokea katika wilaya yetu na mradi wa EACOP unakuja kubadilisha zaidi maisha yetu,” amesema.

Mradi wa EACOP una jumla ya kambi 16 zinazopatikana katika mikoa nane inayopitiwa na mradi huo ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara, na Tanga inayojumuisha wilaya 24, kata 134, na vijiji zaidi ya 180 wanaofaidfika na fursa mbalimbali