Na Dotto Kwilasa, JamburiMedia, Dodoma
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka(DPP) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imezindua mfumo wa kielektroniki wa kukusanya , kuchakata na kutunza Kumbukumbu za kesi jinai utakaoimarisha utendaji kazi.
Akizindua Mfumo huo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi na Utawala bora George Simbachawene amesema mfumo huo itasaidia kwa kiasi kikubwa utadhibiti makusanyo ya mapato ya Serikali.
Simbachawene amesema kupitia mfumo huo mpaka sasa zaidi ya kesi za jinai 17,411zimeshasajiliwa ambapo kati ya kesi hizo,7,361 zimeshafika mwisho na kutolewa hukumu huku kesi 10,050 zipo Katika hatua mbalimbali za maaumzi.
Amesema,”kiukweli,haya ni mafanikio makubwa katika kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS),lakini pia ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine za
umma zinazohusika na utoaji wa huduma kwa umma,”amesema.
Amesema dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 -2025/26), yote inatambua nafasi ya TEHAMA katika kufikia malengo ya Taifa na hivyo kusisitiza juu ya matumizi sahihi ya TEHAMA katika utekelezaji wa shughuli za Serikali na utoaji wa huduma kwa umma.
“Sera ya Taifa ya TEHAMA ya Mwaka 2016, inasisitiza juu ya Serikali kutumia fursa zitokanazo na TEHAMA pamoja na matumizi sahihi na yenye tija ya Mifumo ya TEHAMA, katika kuboresha utendaji kazi wa Taasisi unaosaidia kutatua changamoto za kiutendaji, kudhibitimakusanyo ya mapato ya Serikali, kujenga na kuboresha uwezo,pamoja na kuimarisha mawasiliano
miongoni mwa wadau wa Serikali Mtandao,”amesema.
Kwa Upande wake Naibu Waziri, Wizara ya Katiba na sheria Pauline Gekulu amesema mfumo huo ni muhimu hasa kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza matumizi yake Hali itakayo saidia kuimarisha na kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Amesema katika kupitia dhamira hiyo huduma za serikali zitatolewa kidigitali na kumrahisishia mwananchi kupata huduma kwa haraka zaidi mahali walipo.
“Sote tunafahamu kuwa haki ni Suala muhimu sana na inapaswa kutolewa kwa wakati kwani haki iliyochelewa na sawa na haki iliyonyimwa hivyo Kupitia Mfumo wa TEHAMA tunataka kuhakikisha haki zote zinatolewa kwa wakati, “amesisitiza
Amesema, Sekta ya Sheria imejiwekea malengo thabiti katika kuboresha utendaji kazi wake kwa kutumia mifumo ya TEHAMA kupitia programu ya e-justice kuwezesha kupata taarifa za kesi mbalimbali zilizoshughulikiwa na hatua zilizofikia.
“Mfumo huu umeunganishwa Katika mfumo wa ubadilishanaji taarifa serikalini (GoVESB)na Hadi Sasa tayari unabadilishana taarifa za mifumo ya Jeshi la polisi pamoja na PCCB, “amefafanua.
Naye Mkurungezi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benetict Ndomba amesema malengo madhubuti ya mfumo huo ni kuhakikisha Taasisi zote za Umma zinaenda na wakati kwa kutumia TEHAMA.
Amesema utekelezaji wa e-GA ni moja ya maeneo muhimu yanayoimarisha TEHAMA kwenye Taasisi za Umma.
Kwa upande wake Sylvester Mwakitalu Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ametumia fursa hiyo kuziasa Taasisi nyingine za Umma ambazo bado zina kiwango kidogo cha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kuongeza juhudi katika matumizi ya TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Kama jinsi Sheria ya Serikali Mtandao ya Mwaka 2019 inavyoelekeza ni wajibu wetu kuweka jitihada za Makusudi ili kuhakikisha kuwa tunafaidika na fursa zitokanazo
na matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi,”amesisitiza