Usiku wa Desemba 5, 2013 dunia ilipata habari mbaya. Nasema ilipata habari mbaya ambazo kimsingi zilitarajiwa, ndiyo maana sikutumia neno mshituko. Mzee wetu Nelson Madiba Mandela aliaga dunia.

Tangazo rasmi lilitolewa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini akalitangazia taifa lake na dunia kwa ujumla kuwa hatunaye tena Mzee Mandela duniani.

Kwa Afrika Kusini, mzee huyu anafahamika kwa jina la Madiba. Ukisema Madiba wanajisikia vizuri. Kwa nchini nyingi, Mandela amekuwa alama ya ushindi, alama ya upendo, alama ya maendeleo, alama ya uvumilivu, alama ya kiunganishi na nguzo ya umoja. Ndiyo maana familia nyingi katika Bara la Afrika zilichagua kuwabatiza watoto wao jina Nelson.

Hata mimi kwenye familia yetu, mdogo wangu, mtoto wa Mzee Barthazar Balile, anaitwa Nelson. Anaitwa Nelson si kwa sababu ya jambo lolote, bali alizaliwa wakati harakati za kupigania uhuru nchini Afrika Kusini zikiwa zimepamba moto, na hivyo yeyote aliyeitwa Nelson, Madiba, Mandela alionekana ni shujaa. Nchini Afrika Kusini, wamefikia hatua ya kutunga sheria kuratibu matumizi ya majina Nelson, Mandela na Madiba.

Wazazi wengi kila walipopata watoto waliwabatiza jina Nelson au Madiba au Mandela. Kwa sasa imefikia hatua kila hospitali inaruhusiwa kuita majina hayo nchini humo kwa watoto wasiozidi watano kila mwezi. Kwa mantiki hiyo, kuna uwezekano kuwa nchini Afrika Kusini karibu kila mwezi, watoto wapatao 300 au zaidi hubatizwa jina Nelson, Madiba au Mandela.

Najua msomaji umekwishasoma na kusikia mengi juu ya Mandela. Mimi nitajitahidi kujibu swali moja tu, kwa nini Mandela anatetemesha dunia kwa kifo chake. Tumeshuhudia Uingereza wakipeperusha bendera nusu mlingoti, Marekani pia wamepeperusha bendera nusu mlingoti. Tanzania imetangaza siku tatu za maombolezo na bendera kuwa nusu mlingoti. Venezuela imetangaza siku tatu za mapumziko.

Sitanii, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Mandela alipata Shahada ya Kwanza ya Sheria mwaka 1943, baada ya kuwa amesoma katika vyuo vikuu viwili kwa nyakati tofauti kutokana na kukimbia ubaguzi wa Wazungu — Fort Hare University na University of Witwatersrand.

Hata baada ya kufungwa gerezani, Mandela aliendelea kujisomea na kubobea katika sheria za haki za binadamu na uhusiano wa kimataifa.

Baada ya kujiunga na African National Congress (ANC), Mandela alianzisha tawi la Umoja wa Vijana wa ANC.

Wakati huo, alikuwa akiendelea na kazi ya uwakili kutetea wanyonge. Najua historia hii inawezekana msomaji umekwishaisoma sehemu mbalimbali, lakini imenilazimu kuitaja kutokana na hoja ifuatayo.

Kwamba Mandela alikuwa kati ya wasomi weusi wachache nchini Afrika Kusini, sawa na ilivyokuwa kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa hapa Tanzania. Afrika Kusini lilikuwa taifa linalochimba madini, na Wazungu ndiyo waliokuwa wameshikilia uchumi uliotokana na kuchimba madini. Nyakati hizo, hawa Wazungu walikuwa wakihitaji vibaraka.

Walihitaji wasomi wachache weusi wawatumie kuingia mikataba na weusi wenzao. Wazawa wengi walikuwa hawajui kusoma na kuandika. Wazungu walikuwa hawajui lugha za wazawa. Iliwalazimu kupata mtu mweusi anayejua Kiingereza, kisha anafahamu lugha za asili kama Kisukuma, Kihaya, Kinyakyusa au Kichagga, ili awasaidie kuingia mikataba nao.

Sitanii, Mandela alikataa kuuza nchi yake. Hapa kwetu tunao wanasheria waliobobea. Hawa wengi wamekuwa wakiwauza wananchi kuingia mikataba mibovu na wanaoitwa wawekezaji katika kuuza ardhi, mikataba ya madini yetu mnaona ilivyo, wanashuhudia ujenzi wa barabara mbovu kama ile ya Kilwa au isiyo na viwango kama ya Bagamoyo.

Wasomi wetu wanajenga miradi chini ya viwango kwa sababu ya ‘ten per cent’. Mandela alikataa yote hayo, hakutaka kuwa kama Rais wa iliyokuwa Zaire sasa DRC, Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Za Banga. Huyu, alitumia uelewa wake wa lugha ya kigeni kusaliti wazawa akina Patrice Emeri Lumumba. Watoto wake wakawa wanasoma shule za kutwa Ufaransa.

Mobutu alikuwa anachukua maji ya kunywa kutoka Ufaransa, akihofu kuwa maji ya Afrika si salama (contaminated). Mandela alijua kuwa wapo wengi wa aina hii, lakini akakataa kuungana na Wazungu kwenda ‘kula kuku’ kwenye hoteli kubwa kubwa, badala yake akakubali kuishi gerezani kwenye Kisiwa cha Robben akiwa mfungwa Na 46664.

Sitanii, jambo jingine, baada ya kuishi gerezani kwa muda wa miaka 27, baadhi ya Waafrika walitamani kuona Mandela akijenga magereza makubwa na kukusanya Wazungu wote wakaishia gerezani. Walitaraji Mandela baada ya kuwa Rais wa Afrika Kusini angelipiza kisasa kwa kiwango cha kutisha na kwa maneno ya Waswahili, kwamba Wazungu ‘wangeipata fresh’.

Mandela aliukataa mkondo huo. Akaazima maneno ya Yesu Kristo. Yesu alihojiwa na Walimu wa Sheria na Mafarisayo, kuwa mbona anakula na kuketi na wenye dhambi? Yesu, aliwajibu vyema. Alisema, “Wenye afya hawamuhitaji daktari, wanaomuhitaji ni walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi ili wapate kupona.”

Maneno haya yaliwashangaza wengi. Ndivyo alivyofanya Mandela. Hakuna aliyetaraji kuwa angekaa meza moja na Frederick de Klerk aliyeshiriki kumtesa. Hawakutaraji iwapo angekaa meza moja na Mzungu yeyote. Kila mara weusi walikuwa wakimkubusha awasulubu Wazungu, ila yeye aligoma. Alikataa katakata kulipiza kisasi. Baadhi walimchukia, lakini kumbe Mandela alikuwa akiishi kwa matendo maneno yake.

Alichokuwa akikipinga yeye ni ubaguzi, uonevu na unyanyasaji si kwa sababu waliokuwa wakifanya hivyo ni watu weupe — Wazungu — bali kutokana na matendo yao. Iwapo Mandela angeshiriki dhambi ya kuwanyanyasa Wazungu, basi asingekuwa na tofauti yoyote na makaburu hawa. Katika hali ya kawaida kabisa, mtu akikutukana ukamwambia asante, basi anajisikia vibaya kuliko kumjibu kwa tusi.

Sitanii, lipo somo jingine aliloifundisha dunia Mandela. Baada ya kukaa gerezani kwa miaka 27, hata kama angeamua kukaa madarakani hadi kifo chake wiki iliyopita, sidhani kama kuna mtu yeyote nchini Afrika Kusini angethubutu kumwambia mzee achia ngazi. Angeendelea kupata ushindi wa kishindo awamu baada ya nyingine, lakini yeye aliamua kutumikia awamu moja tu.

Ilipotimu mwaka 1999, Mzee Mandela akasema imetosha, akastaafu urais, akamwachia urais Naibu wake, Thabo Mbeki. Alitumikia awamu moja tu. Mwaka 2004 Mandela akastaafu tena maisha ya kijamii (public life), akawa anaishi nyumbani kwake kucheza na wajukuu. Mtu mwingine, angependa kuendelea kupanda ndege kuzunguka dunia nzima kutoa midahalo, maana watu walikuwa bado wanampenda.

Sitanii, kwa Afrika Kusini na dunia kwa ujumla Mandela anamaanisha upendo, mshikamano, msamaha, maendeleo na kila kiwacho. Alilenga kuhakikisha wazawa nchini Afrika Kusini wanashikilia uchumi wa taifa lao. Kwa mfano, Sheria ya Uwekezaji ya Afrika Kusini inasema kila mzawa anapata asilimia 40 ya mradi wowote unaofanywa na mwekezaji wa kigeni.

Hii anamaanisha, kwa mfano, mwaka 2010 yalipofanyika mashindano ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, kila uwanja uliojengwa asilimia 40 ya fedha zilizotumika zilikwenda mfukoni mwa kampuni ya mzawa iliyoingia ubia na kampuni za kigeni. Hapa kwetu, mwaka 2004 tulijaribu kuanzisha Sera ya Kuwezesha Wazawa, chini ya Iddi Simba aliyeipigia debe, lakini hadi leo imekufa kifo cha asili.

Rais Jakaya Kikwete akaja na mpango wa mabilioni ya Kikwete mwaka 2006, leo uniulize umeishia wapi? Kwa sasa nchi yetu inafanya makosa. Akina Mandela na Mwalimu Nyerere waliona mbali. Walipigania ujenzi wa miundombinu ya kudumu hasa reli na umeme. Kwetu sisi, tumeweka kando suala la reli tunawekeza kwenye barabara na kuruhusu wakubwa kuendelea kumiliki malori yenye kuharibu barabara.

Mandela na Mwalimu Nyerere walikuwa wanapigania elimu, afya, maji na miundombinu ya usafirishaji, lakini leo nikiuliza tunapiganiaje vitu hivyo ambavyo ni nguzo ya kilimo cha kisasa, sina uhakika kama nitapata majibu. Kifo cha Mandela kimegusa wengi kutokana na ukombozi uliozaa uhuru wa mawazo.

Leo wafanyakazi wa migodi wanaandamana nchini Afrika Kusini, wawekezaji wanakaa nao chini na kuwasikiliza, kama ingekuwa miaka ya 1976 yangekuwa mauaji makubwa sawa na yaliyofanywa Soweto, mwaka huo. Ila kutokana na mapambano aliyofanya Mandela leo wafanyakazi wa migodi wanasikilizwa, badala ya kupuuzwa na kuuawa.

Mandela amesimamia uandishi wa Katiba mpya ya Afrika Kusini (1996) iliyojengeka katika misingi ya uhuru wa kutoa mawazo. Kwa nchini Afrika Kusini vyombo vya habari vina haki ya kupata habari, uhuru wa vyombo vya habari uko juu na wananchi wana haki ya kufika katika ofisini yoyote ya Serikali kwa kufuata utaratibu wa kisheria uliowekwa wakadai na kupata habari.

Tanzania tupo kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya. Kikwete unayo nafasi ya kuhakikisha kuwa haki ya kupata habari inapatikana kwa kila mwananchi. Unaweza kuwezesha uhuru wa kupata habari ukatambulika kikatiba sawa na alivyofanya Mandela, na kwa kufanya hivyo, utaingia katika historia.

Sitanii, nasema kalale pema peponi Mzee Madiba. Tulikupenda ila Mungu amekupenda zaidi. Mbegu uliyoacha umeipanda, nakuhakikishia vijana tupo, tutahakikisha haiozi. Waasisi mlifanikisha ajenda ya kupata uhuru, ni wajibu wetu tuliosalia kuhakikisha sasa tunapata uhuru wa kiuchumi.

Mungu ailaze Mahala Pema Peponi roho ya Mzee Madiba (95).