Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imeendelea na maandalizi ya mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kuanza Jumapili ya wiki hii, huko Gabon.
Katika maandalizi ya kuelekea katika mashindano hayo, timu hiyo imeshinda michezo mitatu mfululizo, imeshinda mechi mbili za kirafiki dhidi ya Gabon, mechi zilizochezwa nchini Morocco ilikokuwa imeweka kambi kabla ya kwenda nchini Cameroon.
Timu ipo nchini Cameroon tangu wiki iliyopita na tayari imeshacheza na wenyeji na kushinda bao 1-0 na baada ya mechi ya marudiano, walitoka suluhu ya bao moja.
Akizungumza na JAMHURI, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji wa timu hiyo, Charles Hillary, amesema kazi waliyokabidhiwa inaenda vizuri na kwamba Serikali na wananchi pamoja na taasisi mbalimbali wanaendelea kutoa ushirikiano mzuri kuhakikisha vijana wanapata mahitaji yote muhimu.
Amesema kamati yake imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kila Mtanzania anahamasika kuwasaidia vijana wa Serengeti Boys, ambao wengi wao wanalelewa na TFF.
“Umefika wakati kwa Watanzania tukatae kuitwa ‘kichwa cha mwendawazimu’ na hili litawezekana kwa kuwekeza katika timu hizi za vijana ambazo tayari zimeonesha uthubutu wa hali ya juu,” amesema Hillary.
Amesema kamati, kwa kushirikiana na mamlaka husika, itahakikisha uhai wa Serengeti Boys na pia timu ya soka ya Tanzania ya Vijana chini ya umri wa miaka 23, Ngorongoro Heroes, inafuzu michezo ya Olimpiki mwaka 2020 zitakazofanyika Tokyo, Japan.
“Tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha vijana wetu chini ya umri wa miaka 23 wanafuzu katika michezo ya Olimpiki 2020 itakayofanyikia Tokyo nchini Japan,” amesema Hillary.
Katibu wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine, amesema Shirikisho litafanya kila liwezekanalo kuhakikisha timu inafanya vizuri nchini Gabon.
“Changamoto iliyo mbele yetu ni gharama kubwa zinazohitajika kuhakikisha vijana wanatuwakilisha ipasavyo, ndiyo maana tunawaomba Watanzania wote kuunganisha nguvu kuwasaidia vijana hawa,” amesema Mwesigwa.
Amesema TFF kwa kushirikiana na Serikali, wadau na wapenzi wote wa mchezo wa soka, dhamira yetu kubwa iliyo mbele kwa sasa  ni kuhakikisha timu inakwenda Gabon kutoa ushindani wa hali ya juu na kurejea na Kombe.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Muhidin Ndolanga, amesema kama kuna jambo ambalo Watanzania wanapaswa kujivunia katika kipindi hiki ni timu ya Serengeti.
“Wachezaji hawa wameendelea kujijengea hali ya kujiamini kati yao sababu wamecheza dhidi ya  mwenyeji wa mashindano, na wamecheza dhidi ya timu zenye majina makubwa barani Afrika,” amesema Ndolanga.
Amesema kitendo cha kuifunga timu kama Cameroon na Gabon zote za Afrika Magharibi kimewaongezea hali ya kujiamini na hili litawasaidia wakati wote wa mashindano yaliyoko mbele yao.
Amesema Watanzania hawana budi kuiunga mkono timu  kwa kuichangia ili iweze kupata motisha ya kupambana katika mashindano yaliyo mbele yao muda wote watakapokuwa huko.
Ndolanga amesema asilimia kubwa ya wachezaji wa timu hiyo waliopo sasa wanalelewa na kutunzwa na TFF, hii ni tofauti na sehemu nyingine kote duniani ambako wachezaji wanatoka kwenye klabu.
“Katika nchi nchi nyingine chama cha soka kazi yake ni kuandaa mazingira mazuri ya timu za taifa na siyo kutengeneza wachezaji, katika hili mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni; TFF wanastahili pongezi,” amesema Ndolanga.
Amesema jambo hilo lina faida kubwa sana kwa wachezaji hawa  kukaa katika mazingira ambayo wanafundishwa soka kwa muda mwingi kutoka kwa wataalamu wa soka la vijana waliopo TFF.
Amesema mchezo wa soka kwa sasa ni miongoni mwa michezo yenye kuwapatia vijana utajiri mkubwa duniani, hasa wakati wa kununua na kuuza mchezaji, lakini pia ndiyo unaoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi duniani.
Timu hiyo ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imebadilishiwa kituo kutoka Port Gentil na sasa imepangiwa mjini Libreville wakati wa fainali za Afrika kwa Vijana.
Timu hiyo imepangwa kundi B pamoja na timu za Niger, Angola na Mali  na inatarajiwa kufungua dimba  katika  michuano hiyo Mei 15, mwaka huu,  kwa mabadiliko hayo, kundi ‘A’ lenye timu za Cameroon, Ghana, Guinea pamoja na wenyeji Gabon  litakuwa mjini Port Gentil.