Tanzania imebadilisha sheria za kumiliki ardhi karibu mara nane katika muda wa miaka kumi na moja ili kuruhusu wananchi kuporwa ardhi yao na wageni – “kisheria”.
Uhalali wa sheria yoyote ni kutenda haki; lakini sheria zinazoidhinisha uwekezaji wa wageni katika ardhi haziwatendei haki wananchi wa Tanzania, hivyo hizo sheria si halali; ni bora zifutwe kwa manufaa ya umma.
Tuna matatizo gani Waafrika!
Namna nyingine ya kulitazama hili suala zima la uwekezaji wa waja kwenye ardhi ni hii: maendeleo ya Afrika yameanza kurudi nyuma kwa kasi baada ya Warabu na mataifa mengine yenye mafuta kuanza kutuuzia mafuta yao kwa bei za kutuumiza.
Maendeleo ya Afrika yameanza kurudi nyuma baada ya nchi za viwanda kutuuzia bidhaa zao (capital goods) kwa bei za kutuumiza. Na hakuna Mwafrika hata mmoja aliyewahi kukaribishwa kuhodhi kisima cha mafuta Uarabuni na kwingineko au kiwanda Ulaya na sehemu nyingine.
Kulikoni basi, leo viongozi wetu wanagawa bure rasilimali yetu yenye thamani kubwa kupita mafuta, dhahabu na bidhaa za viwanda, tena kwa wale wale Wazungu na Waarabu waliosababisha maendeleo yetu kudumaa kutokana na kutuuzia bidhaa zao kwa bei za kinyonyaji? Huu tuuite ni usamehevu au uzezeta? Tuna matatizo gani sisi Waafrika?
Kadhalika, viongozi leo wanatoa bure kwa wageni ardhi, ambayo thamani yake ni zaidi ya haya makaratasi yanayoitwa fedha, ziwe ni dola, yuro (euro), pauni na nyinginezo ambazo siku hizi zinachapishwa kiholela bila kuzingatia bidhaa ambazo nchi inazalisha, halafu hiyo “process” imepewa jina lenye hadhi – “quantitative easing”.
Na viongozi wetu ambao tumewapigia kura kwa heshima zote, wanakubali utapeli rejareja kama huu; hivi, tuna matatizo gani sisi?
Miaka ya 1970 Idi Amin Dada, aliyekuwa mtawala wa Uganda alipomwambia Gavana wa Benki Kuu ya Uganda kuwa nchi haiwezi kuishiwa na fedha, chapisha zaidi; alibezwa na wanasiasa na wachumi wa nchi zilizoendelea: “…. Mswahili mbumbumbu huyu hajui mambo ya uchumi yanakwendaje”.
Lakini leo, wao wenyewe na macho makavu, wanafanya yale yale ambayo Amin aliyasema. Je, hii ni kuwa na kumbukumbu fupi au dharau ya kimbali?
Ninamaanisha nini ninaposema viongozi wa Afrika wanagawa ardhi bure. Sehemu nyingine duniani gharama ya kununua hekta moja ya ardhi ni kama aifuatavyo:
Uingereza ni US$26,000, Ujerumani ni $19,500, Marekani ni $16,000, Brazil na Argentina ni $8,000; wakati katika nchi za Afrika, hekta moja ya ardhi inaanzia senti 23 za dola ya Marekani ($0.23). Kwa maneno mengine kikombe cha chai au kahawa Marekani na Ulaya kina bei kubwa kupita hekta moja ya ardhi Afrika. Hiyo kama si bure, ni kitu gani? Yamkini, inakuwa vigumu kwa mtu ambaye hapendi kujidanganya kushawishika kuwa viongozi wa Afrika hawajanunuliwa.
Kwa sababu wakihojiwa kwa nini wanatoa rasilimali yetu bure, karibu wote wanajibu: “…Oooh hawa wawekezaji wa nje wataleta huduma za jamii sehemu wanazowekeza kama vile zahanati, shule, watachimba visima vya maji na kadhalika”.
Lakini hawayasemi yaliyo kwenye Memorandum of Understating (MoU) kwamba wawekezaji hao watakuwa na hiyari ya kuleta hizo huduma; yaani wasipoleta nchi haziwezi kuwadai. Hayo kama si makusudi ni nini?
Rais wa Liberia, Ellen Johnson-Sirleaf alinukuliwa akiwaambia walioporwa ardhi: (the dispossessed) “…wakati serikali yenu ikisaini karatasi yoyote na wawakilishi wa nchi za nje, jamii haziwezi kubadilisha.”
Jinsi gani kauli hiyo inawalinda wananchi wa Liberia na kwa mwendelezo wananchi wa bara la Afrika? Na wakati kwa kutumia hizo alizoiita “karatasi” nusu ya nchi inadaiwa amekwishaitoa kutoka mikono mwa wananchi kwenda kwa hao wanaoitwa “wawakilishi”!
Viongozi wengine wa Afrika wamesaini mikataba kuwa mwekezaji akiwa na kesi ya kiuwekezaji kati yake na nchi aliwekeza, basi kesi hiyo inakwenda kusikilizwa na mahakama zilizo nje ya Afrika.
Hii kweli ni mikataba yenye lengo la kulinda maslahi ya Afrika na Waafrika? Kama hao wawekezaji hawaziamini mahakama zetu, kwa nini Waafrika tuziamini mahakama zao; inakuwaje wawekezaji wanakuwa radhi kuwekeza katika nchi ambazo sheria zake hawana imani nazo?
Huku kama si kutafutana muhali na visingizio vya kutuporomoshea makombora kutoka kwenye drone zao, kesho na keshokutwa, ni kitu gani?
Ardhi ni uhuru na wawekezaji wa nje kwenye ardhi, tutake tusitake, ni wakoloni. Naomba nieleweke vema ninalolisema hapa: sisemi wawekezaji wote wa nje in wakoloni; la hasha.
Ila ninachosema ni kuwa wawekezaji wa nje katika ardhi – bila isipokuwa – ni wakoloni. Tusibabaishwe na misamiati (semantics). Swali la msingi ni hili: Inakuwaje, viongozi wa Afrika wanarudisha kwa wakoloni mamboleo, uhuru ambao si mali binafsi ya viongozi, au si mali ya Serikali zao, bali mali ya taifa bila hata kura za maoni?
Hakuna Serikali hata moja katika historia ya ulimwengu iliyopata kutoa ardhi kwa mikataba ya miaka 99 na ikafanikiwa kurudisha ardhi hiyo mikononi mwa wananchi bila vita.
Haipo; na kupitia “drones” hiki kitu kinachoitwa vita kimefutwa, nafasi yake imechukuliwa na mauaji ya upande mmoja yatakayohakikisha kushindwa kwa vizazi vyetu vijavyo na ushindi wa kishindo wa wakoloni wenye hizo “drone”; je, viongozi mnashindwaje kuliona hili?
Karne ya Afrika
Hii ilikuwa iwe ni karne ya Afrika kwa marefu na mapana, kama viongozi wangelikuwa wazalendo wenye mitazamo ya masafa marefu. Ili kuhakikisha kuwa wanafaidika kutokana na mafuta yao wenzetu waliunda kitu kinachoitwa Umoja wa Nchi Zinazouza Mafuta, “Organization of Petroleum Exporting Countries – OPEC.”
Sisi tunafahamu wazi kuwa raia wa hizo nchi zenye mafuta hawawezi kunywa hayo mafuta; wala raia wa nchi za viwanda hawawezi kula hizo “capital goods” zao, yaani mazao hayo hayawezi kuwawezesha kuishi.
Hii maana yake ni kuwa Afrika ambayo ina asilimia 60 ya ardhi yenye rutuba duniani, (na idadi ya watu inatarajiwa kufikia bilioni 9 mwaka 2050, watu ambao hawataweza kukwepa kula), basi tuna kitu bora zaidi ya mafuta na bidhaa za viwanda.
Lakini hatujasikia viongozi wetu wakiongelea uundaji wa Umoja wa Nchi Zenye Ardhi ya Kilimo, badala yake Waafrika (kama watoto) wanashindana ni nchi gani itatoa vishawishi (incentives) vingi zaidi kwa hao wakoloni mamboleo, ili kuwavuta waje, kama vile: kutoa misamaha ya kulipa kodi, kupunguza nguvu za Vyama Vya Wafanyakazi nchini (Trade Unions), Serikali kugharamia ujenzi wa barabara kutoka kwenye mashamba ya wawekezaji kwenda kwenye vituo vya kusafirishia mazao nje ya nchi, tena kimikataba, usafisirishaji ambao hauwezi kusitishwa hata mwaka ambao kuna njaa ya kufa watu nchini; ruksa ya kuhamisha faida yote na kadhalika. Waafrika tatizo letu nini?
Wakati viongozi wa Afrika wanachangamkia kuwapa ardhi yetu wakoloni wapya wanaojivisha magwanda ya “wawekezaji”, itakuwa ni bora kuzingatia mambo muhimu yafuatayo: kwanza, ukweli wa hizi “drones”; pili, kweli ya kuwa katika uhusiano wa kimataifa (international relations) amani, haijapata kuwa, si, na wala haitakuwa lengo.
Madhumuni ya uhusiano wa kimataifa ni kulinda na kuendeleza maslahi muhimu ya kitaifa (vital national interests). Na inapobidi vita kuvikia lengo hilo, basi nchi huwa hazisiti kwenda vitani.
Hivyo basi, kesho na kesho kutwa hii ardhi ambayo inatolewa bure leo, watakuja kugeuza kuwa mali yenye maslahi muhimu (vital interest) yatakayowalazimisha kwenda vitani dhidi yetu ili kuyalinda. Tatizo ni kuwa hiyo kesho kupitia “drones” haitakuwa ni vita bali mauaji (massacre).
Tatu, katika diplomasia, nchi hazina rafiki; taifa linaweza kuwa na maslahi ya pamoja na taifa jingine (mutual interests) hivyo likalazimika kushirikiana kudumisha maslahi hayo; huo si urafiki. Leo, viongozi wetu wanaendesha bara kana kwamba huko nje kuna mataifa “rafiki” lukuki ambayo yapo yatari kuzisaidia nchi zao; haya kama si makusudi, basi ni siasa za chekechea.
Kwani hakuna nchi inasaidia nchi nyingine kwa lengo la kusaidia bali kama matokeo (by-product) ya kujisaidia yenyewe.
Jambo jingine ambalo Waafrika inabidi tujikumbusha ni kweli ya kuwa wakoloni walipoingia Afrika na kuvamia ardhi hawakulipa fidia hata senti moja kwa wenyeji waliowakuta kwenye hiyo ardhi.
Lakini walipoambiwa ondokeni tunataka ardhi yetu wote walidai fidia; wakati wakoloni wanavamia nchi zetu kulikuwa hakuna majadiliano ya aina yoyote na wenyeji, lakini walipoambiwa nendeni wakadai hiari ya kuuza hayo mashamba, kwa mifumo ya “willing seller, willing buyer”.
Haya ndiyo matatizo ambayo vizazi vyetu vijavyo tunawajengea kupitia uwekezaji wa waja katika ardhi. Matatizo yenyewe yatakuja kufumuka wakati viongozi karibu wote wanaolala kwenye Ikulu za Afrika leo watakuwa wamekwishachukuliwa na faradhi; labda hili ndilo linalowafanya wasijali, ambao ni usaliti.
Mababu na Mabibi zetu walipambana na wakoloni na walijitolea uhai wao ili sisi tuwe huru leo. Viongozi wa Afrika wanachokifanya sasa ni kutupilia mbali uhuru huo na kuwaweka wajukuu na vitukuu vyetu kwenye ukoloni na utumwa wa kudumu. Na drones ndiyo zitakuwa mihuri za hatima hiyo.
Karne ya 19 wakoloni waliwatambia mababu na mabibi zetu: “… vyovyote itakavyokuwa, tuna mzinga wa maxim, na wao hawana.” Kesho na kesho kutwa vilembwe na vining’ina vyetu vitakuja kutambiwa: “… vyovyote itakavyokuwa, tunazo drones/UACVs, na wao hawana.”
Manyanyaso, masimango na utumwa huo utakuja kutokana na choyo na uroho wa viongozi wanaokabidhi ardhi kwa hawa wanaojiita “wawekezaji katika ardhi.” Hii ni zaidi ya aibu, ni fedhaha na usaliti ambao hauna kipimo.
Harid Mkali ni mwandishi wa habari, mchambuzi anayetumia nafasi hizo kuandika vitabu. Ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI kupitia tovuti ya www.jamhurimedia.co.tz. Anaishi jijini London, Uingereza. Anapatikana kupitia simu: +447979881555; barua pepe: [email protected] na tovuti yake: haridmkali.com