Mchezaji nyota kutoka Ivory Coast aliyeng’ara akiwa na Klabu ya Chelsea ya Uingereza, Didier Drogba, amestaafu kucheza soka baada ya miaka 20 ya hekaheka uwanjani.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 40, ameichezea Chelsea mara mbili tofauti na kufunga jumla ya magoli 164 katika mechi 381. Pia ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu ya Uingereza pamoja na taji la Klabu Bingwa barani Ulaya mwaka 2012.
Amemalizia miezi 18 ya maisha yake ya soka nchini Marekani katika Klabu ya Phoenix Rising, ambayo yeye ni sehemu ya mmiliki. “Baada ya miaka 20 nimeamua kustaafu kucheza mpira,” ameiambia BBC.
Ilitarajiwa gwiji huyo kustaafu baada ya mechi ya fainali ya ligi ya Marekani mapema mwezi huu ambapo timu yake ilifungwa goli 1-0 na Louiville City.
“Ni njia bora zaidi ya kumaliza safari yangu kwa kusaidia vipaji vipya kunyanyuka na kung’ara,” amesema.
Drogba alisubiri mpaka alipofikisha miaka 23 kuanza kucheza mpira kwenye ngazi ya ushindani wa juu aliposajiliwa na Guingamp kutoka klabu ya daraja la pili ya Le Mans za nchini Ufaransa, Januari 2002.
Alihamia Klabu ya Marseille miezi 18 baadaye na baada ya mwaka mmoja akatua Chelsea kwa dau la pauni milioni 24, hiyo ilikuwa mwaka 2004. Nyota yake iling’ara zaidi akiwa na miamba hiyo ya London.
Drogba alishinda mataji matatu ya Ligi ya England ndani ya misimu yake minane ya awali na Chelsea, ikiwemo misimu yake miwili ya mwanzo na klabu hiyo. Pia alishinda makombe manne ya FA na mawili ya ligi.
Pia alishinda kiatu cha dhahabu kwa kufunga magoli zaidi kwa misimu ya 2006 – 07 na 2009 – 10.
Aliondoka Chelsea mwaka 2012 kwa heshima kubwa baada ya kufunga penalti ya ushindi kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich.
Kutoka Chelsea, Drogba alielekea nchini China kwa miezi sita na kukipiga na Klabu ya Shanghai Shenhua na baadaye Uturuki kwa mwaka mmoja na nusu katika Klabu ya Galatasaray.
Alirudi tena Chelsea katika msimu wa 2014 -15, ambapo alifunga mabao saba. Alishinda taji lake la nne la Ligi ya England na Kombe la Ligi kwa mara ya tatu.
Drogba ni mchezaji wa nne kwa kufunga magoli mengi zaidi kwenye historia ya Chelsea.
Mwaka 2015, alikwenda Marekani na kuchezea Klabu ya Montreal Impact na baadaye kuwa mchezaji na mmiliki wa Phoenix Rising.
Amelifungia taifa lake magoli 65 katika mechi 105, amecheza makombe ya dunia matatu na kutuzwa kama mchezaji bora wa mwaka wa Afrika mara mbili.
Mpatanishi wa amani
Mara baada ya kuliwezesha taifa lake kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 2005, Drogba aituma ujumbe wa amani kwa taifa lake ambalo lilikuwa kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe. Baada ya wiki moja mapambano yalizimwa.
“Kabla ya kuwa mchezaji, mimi ni binadamu, mwanamume. Nina maisha yangu, ninataka kuishi kwenye nchi yenye amani. Nchi yangu ilikuwa kwenye lindi la vita na fadhaa. Nchi imegawanyika na kitu pekee kinachotuunganisha ni mpira,” alisema hayo mwaka 2005.
“Nilipoamua kuichezea Ivory Coast sikujua kwamba ipo siku ningelikuwa nahodha na kuliongoza taifa kwenye Kombe la Dunia. Sikuwahi kufikiria kuwa ningefanya kitu cha kukumbukwa kwenye historia ya nchi yangu.
“Nilipata pia fursa ya kuichezea Ufaransa, lakini mafanikio niliyoyapata na Ivory Coast – na kama mwanadamu – sidhani kama ningeyafikia kwa kuchezea Ufaransa,” alisema.