Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema kuwa takribani watu 129 waliuawa walipokuwa wakijaribu kutoroka katika gereza kuu la Makala katika mji mkuu Kinshasa siku ya Jumapili jioni, na kuongeza kuwa hali sasa imedhibitiwa, Shirika la habari la Reuters limeripoti
Katika taarifa yake iliyotumwa kwenye X mapema Jumanne, Waziri wa Mambo ya Ndani Shabani Lukoo alisema moto pia umezuka katika jengo la utawala la jela hiyo, bohari zake za chakula na hospitali.
Takribani watu 59 walijeruhiwa, aliongeza. “Jaribio la kutoroka kwa wingi katika gereza kuu la Makala lilisababisha watu kupoteza maisha na uharibifu mkubwa wa nyenzo,” alisema kwenye taarifa hiyo ya video.
Hapo awali, afisa wa magereza alisema hakuna mfungwa aliyefaulu kutoroka, akiongeza kwamba waliojaribu kutoroka wameuawa.
Serikali ilikuwa inachunguza tukio hilo. Jaribio hilo lilitokea mwendo wa 2:00 a.m. (0100 GMT) siku ya Jumapili.
Wafungwa wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wamesikia milio mikubwa ya risasi, pamoja na kelele za wafungwa waliokuwa nje.