Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, wameuteka tena mji wa Kalembe, huko Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Siku ya Jumapili, M23 walichukua udhibiti wa mji huo ulioko zaidi ya kilomita 150 magharibi mwa Goma, kabla ya kusukumwa nyuma na wanamgambo wa “Wazalendo”, wanaounga mkono Kinshasa Mapigano hayo mapya yalizuka karibu saa 5 asubuhi kwa saa za mashariki mwa DRC siku ya Jumatano, Oktoba 23.

Silaha nzito na milio ya risasi ilisababisha hofu katika mji wa Kalembe, mashariki mwa DRC. Mapema mchana, waasi walifanikiwa kuudhibiti mji huo.

Msemaji wa “Wazalendo”, wanamgambo wanaoiunga mkono serikali, hajathibitishi kama kweli wamepoteza mji huo, hata kama amekiri kupoteza moja ya ngome zao.

Kwa mujibu wa vyanzo vya utawala na usalama, wapiganaji wanaoshirikiana na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) waliondoka kuelekea kijiji cha Malemo, katika eneo la kimkakati la Walikale.


Zaidi ya watu 40,000 wanaishi Kalembe. Mji ulio kwenye mhimili muhimu wa barabara, ambao hutoa ufikiaji wa amana za uchimbaji wa dhahabu, coltan na almasi, huko Walikale katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Siku ya Jumatano, waasi pia walichukua udhibiti wa kijiji cha Ihula katika eneo hilo hilo, na mapigano zaidi kati ya M23 na “Wazalendo” yaliripotiwa Kahira, eneo la Masisi.

Mapigano haya yanakuja baada ya wiki za utulivu, wakati usitishaji mapigano umeanza tangu mwanzoni mwa mwezi wa Agosti, na wakati mazungumzo yanatatizika kufanikiwa kati ya Rwanda na Kinshasa.