Mawaziri wa Mambo ya Nje wa DRC Congo na Rwanda wamekubaliana kuanza mazungumzo ya kurejesha amani Mashariki mwa DRC  Congo.

Uamuzi huu umekuja  baada ya kufanyika  kikao maalum huko Luanda nchini Angola kilichohudhuriwa na wawakilishi wa pande hizo mbili Thérèse Kayikwamba Wagner wa Kongo, Olivier Nduhungirehe kutoka Rwanda na mwenyeji wa kikao Tete Antonio kutoka Angola.

Katika kikao hicho, Rwanda na DRC, wamesema wako tayari kuanza mazungumzo hayo wiki hii na watahakikisha mazungumzo hayo yamalindwa na chombo cha pamoja cha ufuatiliaji wa masuala ya usalama kati ya Rwanda na Congo.

Rwanda imeendelea kusema kuwa ina nia ya kumaliza mzozo huo na kurejesha amani ya kudumu katika Mashariki mwa DRC Congo.

Huku Congo inaendelea kuishutumu Rwanda kwa kuhusika kuwasaidia wapiganaji wa M23, ambapo Rais Félix Tshisekedi ameendelea kusisitiza kuwa hatazungumza na wapiganaji wa M23.

Hadi sasa Rwanda bado inaendelea kukana dhidi ya shutuma hiyo ya kuhusika kuwasaidia  wapiganaji wa M23.