Licha ya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufana, dosari na vituko kadhaa vimechukua nafasi katika mkutano huo unaofanyika kwenye ukumbi wa Kizota, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Dosari
Dosari kubwa iliyojitokeza ni ile ya baadhi ya wanachama wa CCM kusambaza vipeperushi kushinikiza Mwenyekiti wa Taifa wa CCM asiendelee kuwa na kofia mbili (Urais na uenyekiti).
Wanachama hao wanataka Rais awe mwanachama wa kawaida na kuachia nafasi ya uenyekiti wa Taifa ichukuliwe na mwana CCM mwingine. Kwamba dhana ya Rais kuwa na kofia mbili inampa ugumu wa kuzitumikia kwa ukamilifu kwa wakati mmoja.
Kulijitokeza pia dosari ya baadhi ya wajumbe wa mkutano huo kutoka mikoa mbalimbali kukosa vyumba vya kulala kwenye nyumba za wageni mjini Dodoma licha ya kuahidiwa kwamba wameandaliwa malazi.
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, jana aliwaamuru makatibu wa chama hicho wa mikoa mbalimbali kuondoka katika ukumbi wa mkutano kwenda kutafuta vyumba vya kulala kwa ajili ya wanachama hao. “Hili siyo jambo la dharura,” alisema Kikwete.
Pia ilijitokeza dosari ya baadhi ya wajumbe kukiuka taratibu za uchaguzi kwa kuwashangilia na kuwapigia makofi baadhi ya wagombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM walipotokea kujieleza na kuomba kura.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisikika mara kadhaa akikemea tabia hiyo. Wagombea walioshangiliwa zaidi walipotokea kujieleza ni Stephen Wasira, Januari Makamba na Mwigulu Nchemba. “Kushangilia hakuruhusiwi.” Rais Kikwete alisisitiza mara kadhaa maneno hayo.
Ilijitokeza pia dosari ya muuzaji wa magazeti ya Uhuru katika banda la Uhuru ndani ya eneo la Kizota kuuza mara kadhaa magazeti ya toleo la Novemba 11-17, 2012 kwa bei ya Sh 1,000 kwa kila gazeti wakati bei haslisi iliyoandikwa ukurasa wa kwanza ni Sh 700.
Baadaye ilibainika kuwa mteja aliyekuwa na Sh 700 aliuziwa gazeti na waliouziwa kwa Sh 1,000 ni ambao walikosa Sh 700 ‘zilizochenjiwa’, ambapo muuzaji alikuwa akidai hana chenji ya sarafu (Sh 300) ya kumrudishia mteja aliyekuwa na noti ya Sh 1,000 na kuendelea.
Vituko
Baadhi ya wagombea ujumbe wa NEC walifanya vituko mbalimbali vilivyowavunja mbavu wajumbe wengi mkutanoni.
Mgombea u-NEC upande wa Zanzibar, Bhaguanji Mbarawa, wakati akijieleza na kuomba kura kwa wajumbe alisema, “Naombeni kura zenu, mimi ndiye baniani pekee kutoka Zanzibar (katika kundi la wagombea u-NEC Zanzibar).” Kauli hiyo iliwasababisha Rais Kikwete na wajumbe wengi kucheka kwa muda huku wakitikisa vichwa.
Naye Kidawa Hamid Saleh, mgombea u-NEC Zanzibar, yeye alipotokea kujieleza aliwasalimia wajumbe kwa kusema, “Shikamoooni woooote, naombeni kura zenu.” Wajumbe wakacheka sana.
Kwa upande wa wagombea u-NEC Tanzania Bara, Wasira alisababisha karibu wajumbe wote zaidi ya 2,000 kuvunja mbavu na kumshangilia baada ya kusogelela kipaza sauti na kusema pamoja na mambo mengine, “Naombeni mnichague nipeleke kilio kwa wapinzani wetu, hasa Chadema.”
Naye Mwigulu Nchemba alisisimua wajumbe wa mkutano huo hasa aliposema, “Maisha bora yanapatikana kwa Yesu, kwa Mtume Mohammed na kwa CCM.” Wajumbe walishangilia kwa sauti kubwa.