Kumekuwa na matukio ya mauaji ya watu mara kwa mara katika wilaya za Urambo na Kaliua mkoani Tabora, yanayofanywa na baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola, hali inayoendelea kutishia maisha ya watu, huku ikionesha kuwa hakuna hatua za kuridhisha zinazochukuliwa kukabili tatizo hilo.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mkazi wa Usinge wilayani Kaliua, Kipara Issa, ameuawa baada ya kupigwa kwa muda mrefu na watu wanaodaiwa kuwa ni maofisa wanaoendesha operesheni ya kusaka silaha haramu na kulinda misitu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Tukio hilo lililotokea hivi karibuni, ambapo maofisa hao wakiwa katika magari ya operesheni hiyo, waliokuwa wamevalia sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, maofisa Usalama na Maliasili wanadaiwa kufika nyumbani kwa mtu huyo kwa nia ya kutaka kumfanyia upekuzi baada ya kumshuku anamiliki silaha kinyume cha sheria.
Wakiwa katika upekuzi huo, walikutana mke wa Kipara, Tabu Maganga, ambaye ni askari polisi katika kituo cha Usinge na kuanza kumhoji kuhusu mumewe na shughuli anazozifanya, huku wakidaiwa kumpiga hadi akapoteza fahamu mara kadhaa.
Hali ilivyokuwa
Wakati mke wa Kipara, Maganga, ambaye ni askari polisi mwenye nambari WP 6985 akiendelea kupata suluba kutoka kwa maofisa hao waliokuwa na bunduki na rungu, watoto wa umri wa kati ya miaka 13 na 17 waliokutwa nyumbani hapo pamoja na bibi yao nao walishambuliwa.
Mama mzazi wa Kipara, Magreth Kajoro, akielezea mkasa huo, alisema wakati amekaa nyumbani kwa mwanaye huyo alishangazwa kuwaona maofisa hao walivyofika na kuanzisha tukio hilo la kinyama, na kwamba alipojaribu kuhoji walianza kumpiga.
“Walinikamata na kuniingiza ndani wakanilazimisha nioneshe silaha ambayo walidai inatumiwa na mtoto wangu, lakini baya zaidi mmoja wao ambaye alikuwa kavaa mavazi ya Jeshi la Wananchi aliniwekea bunduki kichwani huku wakiniambia nisali sala yangu ya mwisho,” alieleza Magreth.
Aliendelea kueleza; “Baada ya muda mfupi nilisikia kishindo kikubwa na baadaye kufuatiwa na kauli ya amri ya kukatazwa kufyatua risasi, ndipo Kipara akafika hapo nyumbani akipigwa huku akiambiwa aoneshe bunduki anayofanyia uhalifu, jambo ambalo lilikuwa ni geni sana kwetu hapo nyumbani.”
Katika upekuzi huo, maofisa hao ambao imedaiwa kuwa walipata taarifa za uhalifu zilizowahusisha watu wanane wa maeneo ya Wilaya ya Kaliua akiwamo Kipara kwamba mbali ya kumiliki silaha haramu, ilidaiwa alikuwa anamiliki sare za JWTZ ambazo huzitumia kufanyia vitendo vya kihalifu na akizihifadhi ndani ya magunia ya mahindi na mpunga nyumbani kwake.
Askari hao wa operesheni maalum wakati wa kusaka silaha na sare za JWTZ kabla ya kumwadhibu Kipara hadi akafariki dunia, walimwaga unga wa mahindi na mpunga wakiamini kwamba watakuta silaha na sare hizo za jeshi hilo bila mafanikio.
Watoto Said Auma (14), Anthony Gabriel na Said Kalungumya, walijikuta wakipata adhabu kali ya kubebeshwa milango ya nyumba ambayo ilikutwa ndani kwa ajili ya biashara huku wakipigwa hadi kupata majeraha makubwa katika maeneo mbalimbali ya miili. Hata hivyo, baada ya kutekeleza unyama huo, askari hao wa oparesheni hiyo waliamua kuondoka na Kipara, lakini wakati huo alikuwa na hali mbaya kutokana na kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na kipigo kikali.
“Nilimshuhudia kaka yangu wakati wanamtoa ndani akiwa amelowa damu nyingi baada ya kukosa hiyo silaha waliyokuwa wakitafuta, wakampakiza kwenye gari wakaondoka naye,” alisema Maneno Issa.
Muda mfupi baadaye familia hiyo iliamua kwenda kituo cha Polisi Usinge kufungua kesi wakiwa na mke wa Kipara, Tabu, ambaye inadaiwa kuwa wakati akipata kipigo alidhalilishwa kwa kuvuliwa nguo akiamuriwa na maofisa hao wa operesheni kugaragara kwenye maji machafu.
DC Kaliua
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Saveli Maketa, alithibitisha kupata taarifa za tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa rasmi baada ya kufanyika kwa uchunguzi, huku akibainisha kuwa anachokijua kuhusu Kipara aliyeuawa ni kwamba alikuwa mhamiaji haramu na mtuhumiwa wa ujambazi anayehifadhiwa na mke wake huyo ambaye ni askari wa Jeshi la Polisi, Usinge.
“Sasa unafikiri ndugu mwandishi hao maofisa wangeenda kufanya upekuzi hapo nyumbani kwa huyo jambazi bila kufanya kash-kash hata kidogo, lazima waende kijeshi kama walivyofanya kwa kuwa tuna taarifa rasmi kuwa anamiliki silaha,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo, hakuzungumzia vitendo vya udhalilisha dhidi ya askari huyo wa kike na kuwapiga watoto na mama mzazi wa Kipara.
Maiti ya Kipara Issa
Baada ya saa kadhaa kupita huku familia ya marehemu Kipara Issa wakishirikiana na baadhi ya wanakijiji cha Usinge, walianza harakati za kumtafuta Kipara kwa kupiga simu na kuuliza kwenye vituo vya Polisi tarafa na wilayani bila mafanikio.
Wakati mdogo wa Kipara, Maneno Issa, akifuatilia huko wilayani Urambo, alipata taarifa kuwa kaka yake amepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Urambo tayari akiwa amekufa, jambo ambalo lilimlazimu afike haraka na kuhakiki maelezo aliyoyapata.
“Niliingia mpaka chumba cha kuhifadhia maiti nikamkuta kweli ni yeye, nikajaribu kumwangalia kwa haraka haraka, lakini kilichoniuma zaidi ni kuona kang’olewa meno na uso wake ulikuwa umevimba mno,” alisema Maneno.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Tabora
Kufuatia tukio hilo ambalo lilikuwa likitafutiwa njia ya kufichwa, hatimaye taarifa zilizagaa hadi zikamfikia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora, ambaye pia ni Mkuu wa mkoa huo, Fatma Mwassa, na kuamua kufunga safari akiwa na wajumbe wa kamati hiyo kwenda kujiridhisha katika tukio hilo la ukatili.
Ujumbe huo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ulifika na kutoa pole kwa wafiwa na baadaye kuzungumza na wakazi wa Usinge, ambao walitoa kilio chao kuhusu mauaji yaliyofanywa na maofisa hao sambamba na kumdhalilisha askari wa kike na kuwashambulia watoto sita wa familia hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa baada ya kusikiliza kwa makini malalamiko ya wakazi hao dhidi ya unyama waliofanyiwa, kwa niaba ya Serikali aliomba radhi tukio la mauaji hayo huku akieleza kuwa licha ya kuwa operesheni hiyo ni halali, lakini nguvu iliyotumika si halali na hivyo kuahidi kuwa Serikali italishughulikia kwa makini na wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, matukio ya mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola katika Wilaya za Urambo na Kaliua yamekuwa yakitishia amani kwa wananchi, hasa wakati wa operesheni hizo za maliasili, ambapo wananchi wamethibitisha kuwa askari wamekuwa wakitumia mwanya huo kuwadhulumu raia badala ya kutekeleza malengo ya operesheni hizo.
RPC Tabora
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Peter Ouma, alikiri kuwepo kwa tukio hilo la mauaji na kwamba anasubiri matokeo ya uchunguzi wa timu ya maofisa aliowatuma huko Usinge.
Hata hivyo, baada ya kiongozi huyo mwenye dhamana ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kufika eneo la tukio na kuupata ukweli alijibu kama ifuatavyo:
“Ni kweli nimefika na kuangalia kilichotokea na kwa sasa siwezi kusema chochote kwa kuwa najisikia kichwa kinaniuma.
”Mei 28, 2011 saa 10 jioni eneo la Usinge ya Kati, askari polisi waliwafyatulia risasi mfululizo wananchi baada ya kukamata ng’ombe 6,301 wao, na katika tukio hilo, Juma Said (21) alipoteza maisha kwa kupigwa risasi mgongoni na wengine wanne kujeruhiwa na hakuna hatua zilizochukuliwa kwa wahusika.
Matukio mengi ya mauaji yanayofanyika kimya kimya katika maeneo hayo yamekuwa yakijenga taswira mbaya na kuonesha kuwa Serikali haichukui hatua, hali ambayo inafanya watu wengi kudhani huenda inabariki uovu huo unaofanywa na taasisi zake.