Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa ukaribu na kupunguza gharama, Shirika la Viwango Tanzania(TBS)limeanza kusogeza huduma Karibu na Wateja kwa kuanzisha ujenzi wa maabara katika mikoa ya kimkakati ya Dodoma na Mwanza.
Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt. Ashura Katunzi,ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 18, 2025, jijini Dodoma.

Amefafanua kuwa kwa upande wa Dodoma, maabara zitakazojengwa zitahudumia mikoa mitatu ya Kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora pamoja na mikoa mingine ya karibu.
Aidha, maabara za Mwanza zinatarajiwa kuhudumia mikoa sita, ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.
Dkt. Katunzi ameeleza kuwa Shirika hilo limeshapata Mshauri Mwelekezi (Consultant) wa kuchora michoro ya jengo pamoja na kusimamia ujenzi wa maabara na ofisi jijini Arusha.
“Hatua hiyo ya ujenzi wa maabara itasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa majibu ya vipimo vya sampuli, ” ameeleza
Licha ya hayo ameongeza kuwa Shirika limetenga kiasi cha TZS bilioni 2.7 kwa ajili ya kuimarisha ofisi saba za kanda ambazo ni Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma na Mbeya pamoja na ofisi za mipakani .

Amezitaja ofisi hizo za mipakani kuwa ni Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili, Tarakea, Namanga, Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Sirari, Kabanga, Rusumo, Mutukula, Bandari ya Bagamoyo, bandari ya Mbweni, bandari ya Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere Dar es Salaam na Bandari ya Tanga.
“Fedha hizo zitatumika kuongeza wafanyakazi na vitendea kazi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakati na kuimarisha zoezi la ukaguzi wa mara kwa mara sokoni ili kupunguza bidhaa hafifu sokoni na hatimaye kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama, ” amesema.
Ameeleza kuwa kwa kipindi cha miaka minne Shirika limefanikiwa kuandaa viwango 1,823 vya sekta mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya soko ambavyo vitasaidia wafanyabiashara, wajasiriamali na watoa huduma kuzalisha bidhaa bora zenye kukidhi matakwa ya viwango, hivyo kuwawezesha kufanya biashara ndani na nje ya nchi, hatua ambayo italeta tija na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Amesema jumla ya vyeti na leseni za ubora 2,402 vimetolewa kwa wazalishaji, miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,066 na kwamba Serikali kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya sh. milioni 350 kila mwaka kwa madhumuni ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote.
“Leseni hizi zimesaidia wazalishaji kuweza kuzalisha bidhaa bora, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao kuweza kuaminika sokoni na pia kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa, ” amesema.
