Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Jumla ya waandishi wa habari 92 wameshiriki katika kinyang’anyiro cha Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari (EJAT) 2022 ambapo jumla ya kazi 883 ziliwasilishwa kutoka vyombo vya habari vya magazeti, radio, runinga na vyombo vya habari vya mtandaoni.

Ni mara ya 14 mfululizo tuzo hizo zinafanyika hapa nchini ambapo zilianza kufanyika mwaka 2009, na zimeendelea bila kukosa hata mara moja.

Tuzo hizo zimeandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na wadau wengine mbalimbali likiwemo Shirika la Maria Stopes Tanzania (MST).

Hata hivyo kwa mwaka huu wa 2023 kimeongezwa kipengele kipya cha Tuzo ya Habari za Afya ya Uzazi ambacho kimedhaminiwa na MST ambapo wanahabari wanne wameibuka kinara wa uandishi wa habari za afya ya uzazi hapa nchini.

MST imeshiriki ikiwa ni katika kuongeza wigo kwa Waandishi wa Habari kutumia kalamu zao kuelemisha jamii kuhusu masuala ya afya ya uzazi ili kuokoa wanawake wanaopoteza maisha kwa kukosa elimu sahihi ya afya ya uzazi.

Hata hivyo Mei,2023 MCT na MST waliingia makubaliko ya ushirikiano kwa miaka miwili ili kuimarisha uandishi wenye tija na afya juu ya taarifa za afya ya uzazi.

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Miradi Pathfinder, Patick Kinemo,Mkurugenzi Mwandamizi Marie Stopes Dk. Geofrey Sigalla,Mkurugenzi Mkuu UMATI, Suzana Mkanzabi, Mkurugenzi Mkuu TAWLA,Tuki Mwambipile ,Msimamizi kitengo cha uchechemuzi na mawasiliano Marie Stopes, Oscar Kimaro, Msimamizi wa kitengo cha mawasiliano UMATI, Richard Ryaganda na Meneja Mawasiliano na Uchechemuzi Marie Stopes, Ester Shedafa, wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa utoaji wa tuzo za EJAT mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Katibu Mtendaji wa MCT,Kajubi Mukajanga amesema kuwa ni mara ya kwanza tuzo hizi kuwepo kwa kipengele cha afya ya uzazi hivyo wanawashukuru MST na pia wanaamini sasa wataanza kuziona kwa wingi habari bora zaidi za afya ya uzazi.

“Hiki kipengele cha afya awali kilikuwepo lakini kwa mara ya kwanza kipengele cha afya ya uzazi kimewekwa ambacho wenzetu Maria Stopes wamekuja kusapoti kipengele hicho cha afya ya uzazi kwa maana ya kuwawezesha washindi na kuwajengea uwezo wa kuandika kwa umahiri kuhusu habari za afya ya uzazi.

“Unapozungumzia afya ya uzazi unazunguzia maisha tangu mtu anapozaliwa, hivyo kwetu ni jambo muhimu sana, tumeshukuru sana kupata sapoti hii ya MCT katika EJAT,” amesema.

Waliojinyakulia ushindi katika kipengele hicho cha Habari za Afya ya Uzazi Peter Lugendo John (TBC Taifa),
Festo Charles Lumwe (Dar 24),Zuhura Said (Zanzibar Leo) na Dafrosa Ngailo (Azam TV).

Mkurugenzi Mwandamizi wa Marie Stopes Dr. Geofrey Sigalla amesema kuwa kuna umuhimu uandishi wa masuala ya afya ya uzazi ili kuwa na vizazi vyenye afya na taifa kunufaika na idadi ya watu wake na kuwaepusha na vifo vya akina mama vitokana na uzazi.

Mkurugenzi Mwandamizi wa Marie Stopes Dr. Geofrey Sigalla akimtangaza mshindi

“Wanahabari wana mchango mkubwa katika kukuza uelewa na kuibua changamoto mbalimbali na kupunguza mitazamo hasi juu ya afya ya uzazi.

“Pia wanahabari wana mchango mkubwa katika kufanya mabadiliko ya Kisera na Kisheria yenye lengo la kuweka mazingira mazuri ya kisera katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za taarifa za afya ya uzazi unakuwa na manufaa kwa wote.” amesema Dk. Sigalla.

Amesema kuwa pia wana uwezo wa kuchochea uwajibikaji katika eneo la afya hususani afya ya uzazi kwa kufuatilia ahadi na utekelezaji wake ili kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma.

“Tuungane kuwapongeza walioibuka na ushindi wa habari ya afya ya uzazi na kuendelea kutoa mchango mkubwa kwa jamii hivyo nitoe wito kwa wengine kuendelea kutoa kipaumbele katika kuangazia habari za afya ya uzazi ili kuendelea kutoa mchango mkubwa katika ustawi wa jamii,” amesema Dk.Sigalla.

Jopo la majaji saba, wenye utaalamu katika habari radio, runinga, magazeti na vyombo vya habari vya mtandaoni walifanya kazi kwa siku tisa ili kupitia kazi hizo.

Mkurugenzi Mwandamizi wa Marie Stopes Dr. Geofrey Sigalla, akimkabidhi tuzo mshindi

Majaji hao wakiwa chini ya Mwenyekiti, Mkumbwa Ally walifanya kazi hiyo kuanzia Juni 10 mara baada ya kuapishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu, Robert Makaramba Juni 9, 2023.

Jopo hilo lilikuwa na wajumbe ambao ni Rose Haji Mwalimu, Mbaraka Islam, Peter Nyanje, Nasima Chum, Dk. Egbert Mkoko na Mwanzo Millinga aliyekuwa Katibu wa jopo hilo.

Washindi wa tuzo hizo wametangazwa katika kilele cha mashindano hayo Julai 22,2023 kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mwandamizi wa Marie Stopes Dr. Geofrey Sigalla akikabidhi tuzo