SERIKALI imewataka Watendaji wanaosimamia zoezi la usajili wananchi kwa ajili ya vitambulisho vya taifa kufanyakazi kwa umakini, uzalendo na kwa ushirikiano na jamii ili kuepuka kuandikisha na kuwapa watu wasio stahili vitambulisho vya raia.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Tabora na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt.Mwigulu Nchemba wakati uzinduzi wa zoezi la usajili wananchi kwa ajili ya vitambulisho vya kitaifa mkoani humo.

Waziri huyo wa Mambo ya Nchi alisema kuwa miaka ya nyuma ambapo Watanzania walikuwa hawana vitambulisho vya Uraia, wapo wageni kutoka katika baadhi ya nchi waliweza kutumia mwanya huo kunufaika na huduma za jamii kama vile elimu ambazo zilipaswa kutolewa kwa Watanzania.

Alisema watu hao walipomaliza masomo walirudi kwao na kunufaisha nchi zao huku wakiwa wametumia pesa za Watanzania kujinufaisha wao na nchi zao na kusema zoezi hilo linahitaji umakini na uaminifu ili kubaini wageni na raia kwa ajili ya kuhakikisha kila kundi lisajiliwe kwa hadhi yake.

Dkt. Nchemba alisema kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake na kuhakikisha hakuna mgeni anayepenya kupewa Kitambulisho cha uraia kwa njia za udandanyifu. Aidha Waziri huyo alisema zoezi la uandikishaji na utoaji wa vitambulisho hivyo ni bure , mwananchi hapaswi kulipa chochote wakati wa ufuatiliaji na kuongeza kuwa isitokee mtua akalipa pesa.

Alisema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali watendaji au viongozi watakaobainika kuwanachangisha wananchi wakati wa zoezi zima la kusajili na utoaji wa vitambulisho vya uraia. Dkt.Nchemba alitoa wito kwa wananchi waliofikia umri wa miaka 18 na kuendelea kujitokeza mapema kwa wingi katika muda ulipangwa ili wasajiliwe na kupewa vitambulisho vya uraia.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Andrew Massawe alisema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa kufikia Desemba mwaka huu zoezi hilo liwe limekamilika nchi nzima ili wananchi waweze kuanza kunufaika huduma hiyo.

Alitaja faida ya vitambulisho vya uraia kuwa ni pamoja na kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi, wananchi kutambulika haraka pindi wanapofika kupata huduma mbalimbali kama vile elimu na afya.

Massawe aliongeza kuwa faida nyingine kurahisisha utambuzi wa makundi yenye mahitaji maalumu na upatikanaji wa huduma za kifedha na simu kirahisi. Aidha Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo aliwaonya wageni wote kutodiriki kujipenyeza na kujisajili kwa lengo kupata kitambulisho cha uraia ,kwani watachukuliwa hatua kali.

Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Quuen Mlozi alisema kuwa jumla ya wakazi wapatao milioni 1.3 wanatarajiwa kusajiliwa na kupatiwa vitambulisho vya uraia mkoani humo. Alisema kuwa Mkoa wa Tabora umepokea mashine 260 ambazo zimegawanywa katika Wilaya mbalimbali kwa ajili ya zoezi hilo.

Queen aliwataka Wakuu wote wa Wilaya na Watendaji kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa umakini ili kuepuka kuingiza watu wasio stahili katika zoezi hilo kutokana na mwingiliano ulipo na wageni katika baadhi ya maeneo. Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa Serikali haitamvulia mtendaji au mwananchi yoyote atakayehujumu zoezi hilo na kusababisha watu wasio na sifa kuingiza na kupata vitambulisho vya uraia.